LA TAIFA LEO
MKUTANO kati ya Orange Democratic Movement na United Democratic Alliance uliofanyika ikulu jana ulifichua mvutano wa wazi, huku tofauti kali zikijitokeza kuhusu uhifadhi wa ngome za kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027. Ingawa taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Oburu Oginga ilionyesha umoja na nia ya kushirikiana, vyanzo vya ndani vinasema kulikuwa na mvutano mkali kuhusu kile kinachoitwa “kuachiana maeneo” yaani heshima ya kila chama kwa ngome za kingine. ODM inadaiwa kushinikiza kuwepo kwa makubaliano yasiyo rasmi yatakayozuia UDA kuingia kwa nguvu katika ngome zake za jadi, hasa maeneo ya Nyanza, Pwani na Magharibi. Vyanzo vinaeleza kuwa viongozi wa ODM walionya kuwa juhudi za UDA kujiimarisha mashinani katika maeneo hayo zinaweza kudhoofisha imani na kuvuruga mazungumzo ya ushirikiano yanayoendelea. “Mjadala ulilenga kuimarisha ushirikiano na kubaini maeneo ya maslahi ya pamoja,” ilisema taarifa ya pamoja ya viongozi hao wawili, ikijaribu kupunguza taswira ya mvutano. Hata hivyo, nyuma ya pazia, hali ilikuwa tofauti. Inadaiwa kuwa Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar alichochea mvutano zaidi kwa kusisitiza kuwa chama chake kitawania viti kote nchini bila vizuizi. Kauli hiyo ilionekana kugongana na msimamo wa ODM unaotaka tahadhari na heshima kwa maeneo ya kisiasa ya kila chama. Wasiwasi hadharani Viongozi wa ODM walieleza wasiwasi wao hadharani siku chache kabla ya mkutano huo, wakidai baadhi ya viongozi wa UDA, akiwemo Amason Kingi, wamekuwa wakidharau chama chao. Licha ya tofauti hizo, vyama hivyo viwili vilikubaliana kuanzisha kamati ya pamoja itakayojumuisha viongozi wa vyama, mawaziri na viongozi wa bunge ili kuratibu ajenda za serikali na kuhakikisha utekelezaji bora wa sera. Kamati hiyo inatarajiwa pia kusaidia kutatua mizozo ya kisiasa inayojitokeza huku mazungumzo ya muungano yakizidi kupamba moto. Hata hivyo, wachambuzi wanasema changamoto kubwa iko mashinani, ambapo UDA tayari imeanza kuimarisha mizizi yake kupitia uchaguzi wa ndani katika kaunti 18, zikiwemo ngome za ODM kama Kisumu, Siaya na Migori. Hatua hiyo imechukuliwa na ODM kama jaribio la moja kwa moja kuvunja nguvu zake katika maeneo hayo. Kwa upande wake, ODM imeongeza juhudi za uhamasishaji, ikiwemo mikutano ya vijana na shughuli za mashinani ili kulinda ushawishi wake. “Si suala la uchaguzi pekee, bali ni la kulinda uhai wa kisiasa,” kilisema chanzo kimoja cha ODM, kikionya kuwa kufungua milango bila masharti kunaweza kudhoofisha msingi wa chama. UDA inasisitiza kuwa kama chama tawala, ina haki ya kujiimarisha.kote nchini na haiwezi kuzuiwa na makubaliano yasiyo rasmi. Wachambuzi wanasema mkakati wa Rais Ruto unaonekana kuwa wa pande mbili—ushirikiano katika ngazi ya juu, huku ushindani ukiendelea mashinani. Hali hii inaweza kuzaa matunda kisiasa kwa UDA ikiwa itafanikiwa kupenya katika ngome za upinzani, lakini pia inaweza kusababisha mgogoro unaoweza kuvuruga ushirikiano huo. Kwa ODM, hatari ni kupoteza ushawishi wake wa muda mrefu katika maeneo yake ya jadi, huku kwa UDA, hatari ni kuzidisha mvutano na kuathiri mipango ya kisiasa ya baadaye. Kwa sasa, macho yote yako kwenye kamati hiyo mpya na iwapo itaweza kusawazisha maslahi ya vyama hivi viwili vinavyozozania ushawishi.
Go to News Site