Collector
Trump anusurika shambulizi Ikulu | Collector
Trump anusurika shambulizi Ikulu
LA TAIFA LEO

Trump anusurika shambulizi Ikulu

RAIS Donald Trump na mkewe Melania Trump waliondolewa hima katika maakuli ya Muungano wa Wanahabari wa Ikulu, White House, na maafisa wa kikosi maalum cha upelelezi mnamo Jumamosi usiku baada ya mwanamume kuwafyatulia risasi maafisa wa usalama waliokuwa karibu. Mwanamume huyo alimfyatulia risasi afisa wa Kikosi Maalum katika kituo cha ukaguzi kwenye hoteli ya Washington Hilton kabla ya kukabiliwa na kukamatwa. Trump aliwaeleza wanahabari baadaye katika kikao kilichoandaliwa upesi ikuluni White House kwamba afisa huyo aliokolewa na mavazi maalum ya kukinga risasi aliyovalia na yuko “hali shwari”. Msemaji wa Kikosi Maalum cha Ulinzi nchini Amerika, Anthony Guglielmi, alithibitisha kuwa afisa huyo aliruhusiwa kutoka hospitalini. Haikubainika papo hapo iwapo Trump alilengwa kwenye shambulizi hilo, japo alieleza wanahabari anaamini alikuwa ndiye shabaha. Rais amenusurika majaribio mawili ya kukatiza maisha yake tangu 2024, kipindi kilichoshuhudia ongezeko la hisia kali kinzani kisiasa nchini humo. Afisa wa ulinzi alimtambua mshukiwa kama Cole Tomas Allen, 31, mkazi wa California. Mengi hayajulikani kuhusu asili ya Allen, lakini machapisho kwenye mitandao ya kijamii yanaashiria alikuwa mwalimu katika shule ya Torrance, karibu na Los Angeles. Kaimu Mkuu wa Polisi Washington, Jeffery Carroll, alisema mshukiwa alijkuwa na bastola, bunduki, na visu kadhaa. Alipelekwa hospitalini kukaguliwa lakini ilikuwa mapema sana kusema nia yake ilikuwa gani, alisema Carroll. Kulingana na uchunguzi wa mwanzo, anaaminika kuwa mgeni katika hoteli hiyo Carroll alisema. Tafran hiyo kuanzia saa mbili na dakika thelathini na tano usiku wa kuamkia Jumapili ilizua maswali mapya kuhusu usalama wa maafisa wakuu nchini, wengi wao waliokuwa wamekusanyika katika ukumbi mkubwa wa hoteli hiyo. Uchunguzi wa kina huenda ukahusu ni vipi mshambulizi aliweza kupitisha kimagendo bastola katika hoteli hiyo, inayoandaa karamu ya kila mwaka ya Muungano wa Wanahabari wa White House, hafla mahsusi kwenye kalenda ya Washington. Hafla hiyo iliyojumuisha mavazi rasmi ilihudhuriwa na wanachama wengi wa baraza la Trump na maafisa wengine wakuu kukiwa na ulinzi mkali. Ni mara ya kwanza Trump alihudhuria hafla hiyo kama rais, baada ya kuisusia miaka iliyotangulia. Baadaye, Trump alihutubia wanahabari, wengi wao wakiwa bado wamevalia mavazi yao ya jioni, katika hotuba isiyo ya kawaida kwa wanahabari iliyofanyika usiku wa manane kwenye chumba cha mkutano, White House, akiwa pamoja na Makamu wa Rais, JD Vance, na mawaziri wengine. Mkewe Trump, Melania alitazama kutoka pembeni na kukimya alipomuuliza iwapo anataka kuzungumzia masuala ya jioni hiyo.

Go to News Site