Collector
SOKOMOKO: Mbunge Kaluma ajiteua nyapara wa boma isiyo yake | Collector
SOKOMOKO: Mbunge Kaluma ajiteua nyapara wa boma isiyo yake
LA TAIFA LEO

SOKOMOKO: Mbunge Kaluma ajiteua nyapara wa boma isiyo yake

MBUNGE wa Homa Bay Town, Peter Kaluma, alijitwika nyapara wa boma isiyo yake kwa wito wake wa kutaka Katibu Mkuu wa UDA, Hassan Omar, aondolewe mara moja katika wadhifa wake akasahau kwamba yeye ni mwanachama wa ODM. Katika taarifa aliyochapisha kwenye akaunti yake rasmi ya X iliyozua joto, Kaluma alimshutumu Omar kwa kuchochea migawanyiko ya ndani katika UDA na kudhoofisha juhudi za kudumisha ushirikiano wa kisiasa kati ya UDA na ODM. Alidai kuwa mtindo wa uongozi wa Omar ni hatari na unaweza kuvuruga mipango ya kisiasa inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya vyama hivyo viwili. Kaluma alimchambua Omar kama “mwanasiasa asiye na uzoefu,” akidai kuwa historia yake katika siasa za uchaguzi na usimamizi wa chama inaonyesha hana uwezo wa kushika wadhifa wa juu wa kimkakati. Aliongeza kuwa kuendelea kwake kushikilia wadhifa huo kunaweza kuhatarisha makubaliano ya kisiasa yanayoendelea kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Mbunge huyo alitaka uongozi wa UDA kumdhibiti Omar au kumuondoa kabisa katika wadhifa huo, akionya kuwa migogoro ya ndani inaweza kuwa na athari kubwa kisiasa kitaifa. Kwa mujibu wake, mizozo ya hadharani ndani ya UDA inadhoofisha mshikamano wa chama hicho wakati ambapo uhusiano wa kisiasa unazidi kuwa muhimu kuelekea uchaguzi ujao. “Chama cha UDA kinapaswa kumzima au kumuondoa mara moja katika wadhifa huo muhimu wa Katibu Mkuu,” Kaluma alisisitiza. Kauli hizo zinajiri katika kipindi ambacho mvutano kati ya viongozi wa UDA na ODM umeongezeka hasa kuhusu ushawishi wa kikanda na ushirikiano wa kisiasa.

Go to News Site