Mwananchi
Dar es Salaam. Asasi za Kiraia na Watetezi wa Haki za Binadamu wamechambua Ripoti ya Uchunguzi wa Matukio ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 huku wakipinga kuundwa kwa chombo kingine cha uchunguzi. Aidha, asasi hizo 14 zimetoa mapendekezo wakitaka kufanyiwa kazi ikiwamo kulipwa fidia kwa walioathirika wa matukio ya Oktoba 29, 2025 na kuendelea. Baadhi ya kasoro ambazo asasi na watetezi wa haki za binadamu wameziainisha ni mbinu zilizotumika kukusanya taarifa za uchunguzi, tume kushindwa kubainisha waliohusika na kusababisha yaliyotokea na taarifa hiyo kubaini uwepo wa kambi na mafunzo. Mjumbe wa Taasisi ya Transparency Forum, Dk Azaveli Lwaitama amesema hawaungi mkono pendekezo la kuundwa kwa chombo kingine cha kijinai kushughulikia masuala yaliyobainishwa na tume. "Muda umekwenda na gharama kubwa zimetumika, kwa sasa ipatikane tume huru ya kutafuta ukweli, uwajibikaji na maridhiano ya kitaifa. Tume hii iundwe na watu huru na Tume ya Jaji Chande itoe taarifa kamili yenye ukweli halisi," amesema. Dk Lwaitama amesema wanatambua kiini cha vurugu na mauaji yaliyotokea Oktoba 29, 2025 kuwa ni mgogoro wa kisiasa ambao umekuwepo Tanzania tangu nchi iliporejea kufuata mfumo wa utawala, kidemokrasia na siasa za ushindani wa vyama vingi za mwaka 1992. "Tunapendekeza wote waliohusika na mauaji na matumizi ya nguvu kama ilivyoelezwa katika taarifa ya Tume, wanapaswa kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria bila upendeleo wowote," amesema. Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk Benson Bana amesema maoni ya asasi hizo ni haki yao, akisisitiza tume imetekekeza wajibu wake kisheria huku akidokeza tangu mwanzo asasi hizo zilipinga tume hiyo ilipoundwa kwamba haikuwa huru. Kuhusu hoja ya kutoundwa chombo kingine cha kuchunguza jinai, Dk Bana aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria na Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ameungana na hoja ya asasi hizo ya kutoundwa Tume nyingine ya kijinai kuchunguza badala yake Tume ya Jaji Chande iongezewe muda na wataalamu kufanya kazi hiyo. Dk Bana amesema hayo leo Aprili 27, 2026 alipozungumza na Mwananchi, saa chache kupita tangu asasi hizo za kiraia kukutana na waandishi wa habari kuchambua ripoti hiyo ya Jaji Chande. "Nasita kuundwa chombo juu ya chombo, kinachohitajika ni kutafutwa chombo kuthibitisha yale ambayo tume imeyabaini, kwa hiyo sioni haja ya kuundwa tume ni kuwapa wataalamu tu na kuchakata taarifa na wahusika wanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria," amesema Dk Bana. Aprili 23, 2026, Ikulu ya jijini Dar es Salaam, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman alikabidhi ripoti hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan iliyoangazia masuala mbalimbali ikiwamo visababishi na athari za kibinadamu ikiwamo vifo vya watu zaidi ya 510. Ripoti ya Jaji Chande ilitoka na mapendekezo 12 ikiwamo Katiba mpya ipatikane ifikapo mwaka 2028 ili itumike katika uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa wa 2029 na Uchaguzi Mkuu wa 2030, Serikali iunde Tume ya Maridhiano na Muafaka wa Kitaifa. Pia, Serikali iunde Tume ya Uchunguzi wa Kijinai kufuatia matukio hayo. Tume hiyo itakuwa na jukumu la kupeleleza na kufuatilia masuala mahsusi yanayohitaji upelelezi zaidi ili kushughulikia tuhuma zilizobainishwa katika taarifa ya Tume. Masuala hayo ni pamoja na kubaini wahusika wakuu wa ghasia, matukio tatanishi ya vifo na majeruhi, maiti ambazo hazijapatikana na kupendekeza hatua za uwajibikaji. Baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Samia alieleza kuwa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 yameacha doa ambalo Watanzania wangetamani lisingekuwepo katika historia ya nchi. Aidha, Rais Samia alisema mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na ripoti hiyo yamepokewa huku akiahidi kwenda kuyafanyia kazi huku akiagiza majeruhi wa matukio hayo kupatiwa matibabu bure pamoja na wanaohitaji vifaa saidizi nao kufikiwa. Uchambuzi wa asasi za haki za binadamu Akielezea uchambuzi waliofanya baada ya ripoti hiyo, leo Jumatatu, Aprili 27, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Programu Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Halima Sonda amesema mbinu za kukusanya taarifa za uchunguzi kutoka kwenye vyanzo rasmi yaani polisi, vituo vya afya au hospitali. Lakini akasema kuwa katika mgogoro wote, kwa vitendo vyake, polisi wanatambuliwa kama wahusika au watuhumiwa. "Tume ilipaswa kufanya uchunguzi kisayansi, kwa hiyo, kwa uchambuzi wetu tunasema kwa ujasiri mbinu ya uchunguzi iliyotumiwa na Tume kukusanya taarifa za awali (primary & secondary data) haikidhi haja ya sifa za kisayansi za kuchunguza matukio ya Oktoba 29, 2025," amesema Halima. Changamoto nyingine alisema tume imeshindwa kubainisha waliozembea kusababisha yaliyotokea kwa kuwa, muda mrefu watetezi wa haki za binadamu na masuala ya demokrasia, uchaguzi, utawala wa sheria na utawala bora wameshauri Serikali juu ya umuhimu na ulazima wa kutekeleza masuala ambayo Tume imeyaita kama vyanzo vya ghasia. "Yote yaliyotokea, kwa sehemu kubwa yamechangiwa na Serikali kutokuchukua au kutokutekeleza maoni ya wadau, kama Tume ilivyotaarifu, madai hayo yamekuwepo kwa muda mrefu katika jamii yetu lakini yamekuwa yakipuuzwa," amesema. Pia, Tume kushindwa kuwataja watu waliohusika pamoja na tume kubainisha baadhi ya vichocheo vya matukio hayo, na uwepo wa makambi na mafunzo kwa ajili ya vijana. Hata hivyo, Jaji Chande alipowasilisha ripoti yake alisema tume hiyo haikupewa kazi hiyo tu, bali tume ya jinai itakayoundwa itatoa fursa kwa watakaohusika au kutuhumiwa kuhojiwa kabla ya kutajwa kwani haki ya kusikilizwa ni takwa la Kikatiba. Jambo lingine, Halima amesema tume imeendelea kutumia hoja za kisiasa zisizo na majibu halisi kwenye ripoti yake jambo ambalo kwa maoni yao si sahihi. "Maswali muhimu yalihusu waliingiaje nchini, ni nani aliyewafadhili, na kwa malengo gani. Hata hivyo, licha ya uzito wa tuhuma hizi katika mjadala wa kitaifa, Tume haikutoa maelezo yoyote," amesema Halima. Pia, kuhusu idadi za vifo na majeruhi, Halima amesema takwimu zilizotolewa na tume zimeshindwa kubainisha ni watu wangapi waliuawa wakiwa kwenye maandamano na ni wangapi waliouwa wakiwa katika makazi yao. Jambo lingine, Halima amesema ni tume hiyo kueleza kulikuwa na miili takribani 39 iliyotambuliwa na ndugu katika vituo mbalimbali vya afya, lakini baadaye ndugu hao walishindwa kuipata na hadi leo hawajafanikiwa. "Taarifa ya tume haijaweka bayana kuhusu watu ambao miili yao haijulikana ilipo. Hii inaonesha muundo wa tume ulichangia watu wengi kuogopa kwenda kutoa taarifa na hivyo, kufanya tume kutoa taarifa huku wengi wakishindwa kwenda kupeleka taarifa zao," amesema. Katika hilo, Jaji Chande alisema hilo ni moja ya jambo muhimu ambalo tume imetoa mapendekezo ili lifanyiwe kazi mapema iwezekanavyo. Mwakilishi wa Taasisi Mwenyeji Kiutawala wa Vuguvugu la RAIA ni SiSi Tanzania (ForDIA), Buberwa Kaiza alisema msimamo wao unaendana na maoni ya wananchi wengi wanaopenyeza sauti zao kupitia njia mbalimbali. "Tunaungana na Watanzania mbalimbali kuikataa tume hii ya uchunguzi ya mauaji, kujeruhiwa na uharibifu wa mali," amesema. Dk Bana na uhalali wa Tume Dk Bana alipoulizwa juu ya uchambuzi huo wa asasi za kiraia alisema: “Tukubali tume imetekekeza wajibu wake, wamefanya kazi yao kwa ushahidi, hizo asasi zingeanzisha uchunguzi wao kupitia mbinu zao au njia zao, sasa kwa nini hawajafanya hivyo." Dk Bana amesema tangu tume hiyo ilipoanza kuundwa asasi hizo hazikukubaliana na muundo wake kwa madai kuwa haipo huru hivyo, zilipaswa kwenda mahakamani kuhoji uhalali wa tume hiyo. "Huwezi kutilia shaka ripoti ya tume, uhalali ni kufanya uchunguzi wako, suala la kutokubaliana kuundwa kwa tume nyingine lina mashiko kwa sababu tunatumia gharama nyingine," amesema. Mtaalamu huyo wa siasa amesema kuunda tume ni kufanya jambo moja mara mbili badala yake inapaswa tume ya Chande ndiyo iongezewe muda walau mwezi mmoja na kuongezewa wataalamu kufanyia kazi mapendekezo waliyotoa.
Go to News Site