Collector
Shule zakumbatia kawi safi kuhifadhi mazingira | Collector
Shule zakumbatia kawi safi kuhifadhi mazingira
LA TAIFA LEO

Shule zakumbatia kawi safi kuhifadhi mazingira

KWA muda mrefu, shule nyingi nchini Kenya zimekuwa zikitumia kuni kupika na kuandaa chakula cha wanafunzi. Hata hivyo, mfumo huo umeendelea kuwa wa gharama kubwa, kusababisha hatari za kiafya na uharibifu wa mazingira. Jikoni kulijaa moshi, wapishi wakihangaika kuwasha moto hasa misimu ya mvua, huku wasimamizi wa shule wakitumia maelfu ya pesa kununua kuni kila mwezi. Katika maeneo kame na nusu-kame (ASAL), ambako miti ni haba, mahitaji ya kuni yameongeza ukataji miti na kuathiri mazingira. Ukataji huo umechangia madhara ya mabadiliko ya tabianchi kama vile ukame wa muda mrefu, mvua zisizotabirika na uhaba wa malisho kwa mifugo. Shule zinavyozidi kuongezeka baadhi zinageukia majiko ya kisasa yanayotumia umeme na nishati ya jua. Hatua hii inasaidia kupunguza gharama, kulinda mazingira na kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula kwa wakati ufaao. Al-Huda Muslim School, shule iliyoko Majengo, Kaunti ya Kajiado, ililemewa na mfumo wa kutumia kuni. Ikiwa na zaidi ya wanafunzi 820, ilikuwa ikihitaji magari mawili ya kuni kila mwezi kwa gharama ya karibu Sh20,000, bila kujumuisha maji na matumizi mengine ya jikoni. Kwa jumla, ilikuwa ikitumia karibu Sh40,000 kwa mwezi kuendesha mpango wa lishe. Mwalimu anayesimamia mazingira na mpango wa chakula, Shaaban Iddi, anasema walikuwa wakiteseka kwa sababu Kajiado ni eneo kame lenye miti michache. “Wakati mwingine tulilazimika kuomba ruhusa kutoka kwa serikali ya kaunti kukata miti kuongeza kuni, jambo lililosababisha kuchelewa kwa chakula,” Iddi anakumbuka. Moshi kutoka jikoni pia uliathiri wafanyakazi. “Wapishi walifanya kazi kwa saa nyingi katika mazingira yenye moshi ulioathiri afya zao,” anaelezea. Lakini hali imebadilika baada ya kampuni ya EcoBora kuzindua majiko yanayotumia nishati ya jua na umeme. Sasa chakula huandaliwa haraka, kwa usafi na bila usumbufu mwingi. “Wanafunzi hupata chakula kwa wakati ufaao na masomo yanaendelea kama kawaida,” mwalimu huyo anadokeza. Iddi anasema Al-Huda Muslim School imeboresha mazingira kwa kupanda miti mingi, ikiwemo miti ya matunda kama vile maparachichi na karakara. “Isitoshe, kando na kufanya kilimo cha matunda, klabu cha mazingira kinawapa wanafunzi motisha kupanda na kutunza miti hadi wanapokamalisha masomo.” Katika Kaunti ya Kiambu, PCEA Mama Ngina Primary and Junior Secondary School, pia, imekumbatia mfumo wa kawi safi huku idadi ya wanafunzi ya shule hiyo ikikaribia 2,500. Naibu mwalimu mkuu anayesimamia shughuli za utendakazi wa shule, Rachael Ndune, anasema moshi ulikuwa tatizo kubwa kwa kuwa madarasa mengi yako karibu na jikoni. Anasema wapishi wengi walikuwa wakipata matatizo ya kiafya yanayotokana na moshi, na wakati mwingine walikosa kufika kazini. “Zamani shule hii ilikuwa ikitumia karibu Sh300,000 kwa muhula kununua kuni, huku kuni mbichi zikisababisha chakula kuchelewa kuiva,” Ndune akaambia Akilimali wakati wa mahojiano shuleni humo. Ukumbatiaji wa majiko maalum yanayoundwa na EcoBora, unaashiria kuletea shule hiyo afueni. EcoBora, ni kampuni yenye makao yake Jijini Nairobi, na kiwanda cha kuunda majiko ya umeme na nishati ya jua Kaunti ya Kajiado. Aidha, mfumo huo safi unasaidia kupunguza matumizi ya kuni majiko hayo ya kiotomatiki pia yakipunguza muda wa mapishi ya chakula. Yvonne Nyambura, mkufunzi wa wapishi kutoka EcoBora, anasema baada ya shule au taasisi yoyote ile kupewa majiko, wafanyakazi hupatiwa mafunzo ya siku tatu hadi saba kuhusu usalama, matumizi bora na kuokoa nishati. “Chakula kama githeri ambacho kilikuwa kikichukua saa tano hadi sita kwa kuni kuiva, sasa huiva ndani ya saa mbili au tatu,” Nyambura anakiri. Joy Kwamboka kutoka EcoBora anasema Kenya ina zaidi ya taasisi 92,000 za masomo, zikiwemo shule na vyuo na ukumbatiaji wa majiko rafiki kwa mazingira kutasaidia kuangazia athari za tabianchi. Anasema shule moja inaweza kutoa hadi tani 700 za hewa ya Kaboni kwa kutumia kuni. Kwa kuhamia majiko ya umeme na nishati ya jua, shule zitaokoa miti, kupunguza uzalishaji wa hewa chafu na kuelekeza fedha zilizookolewa kwa chakula cha wanafunzi hasa wale ambao wametoka kwa familia maskini au kutumika kutekeleza maendeleo mengine. “Tunatengeneza majiko ya lita 20 hadi 2,000 kulingana na oda na mahitaji ya wateja. Kila jiko lina bei yake kulingana na ukubwa wake,” Joy anasema. Kadri Kenya inavyoendelea kukumbwa na athari za tabianchi, shule zikilengwa zitaibuka kama mashujaa wapya wa kulinda mazingira. Uwepo wa majiko safi unaonyesha kuwa vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi vinaweza kuanzia shuleni, hatua ambayo itasaidia kuhamasisha watoto kulinda mazingira.

Go to News Site