Collector
Matonya aonja uhuru baada ya wiki tatu gereza la Shimo la Tewa | Collector
Matonya aonja uhuru baada ya wiki tatu gereza la Shimo la Tewa
LA TAIFA LEO

Matonya aonja uhuru baada ya wiki tatu gereza la Shimo la Tewa

MSANII wa nyimbo za Bongo Flava kutoka Tanzania, Sefu Shabani Ramadhan, almaarufu kama Matonya, ameachiliwa huru kutoka Gereza la Shimo la Tewa baada ya kukaa kizuizini kwa zaidi ya siku 20 kutokana na madai ya ubakaji. Matonya aliondoka gerezani Jumanne jioni baada ya kufanikiwa kukidhi vigezo vya dhamana alivyowekewa na Mahakama ya Shanzu mnamo Aprili 9, aliposhtakiwa. Bw Rashid Naaman ambaye amekuwa akifuatilia dhama ya mwanamuziki huyo, alithibitisha Matonya aliondoka gerezani Jumanne jioni. Msanii huyo alikana mashtaka ya ubakaji alipofikishwa mahakamani ambapo alipewa dhamana ya Sh500,000. Alinyimwa chaguo la kutoa pesa taslimu baada ya upande wa mashtaka kuambia Mahakama kuwa si Mkenya, hivyo basi si salama kumwachilia kwa pesa taslimu. Kama sehemu ya masharti hayo, alitakiwa kuwasilisha pasipoti yake mahakamani. Pia, alipigwa marufuku kuondoka nchini Kenya bila ruhusa ya Mahakama. Aidha mahakama iliagiza idara ya uhamiaji kuweka ilani ili kumzuia msanii huyo asitoke nje ya nchi bila idhini. Kwa zaidi ya wiki tatu, Matonya aliendelea kusalia kizuizini huku wasaidizi wake wakihangaika kukamilisha vigezo vya dhamana ikiwemo kutafuta mdhamini raia wa Kenya na kuwasilisha stakabadhi zinazohitajika. Kuachiliwa kwake Jumanne jioni inajiri baada ya kukamilika na kuidhinishwa kwa taratibu zote zilizofungamana na masharti ya dhamana hiyo. Bw Naaman alisema aliwasilisha stakabadhi kadhaa zikiwemo barua zilizogongwa muhuri kutoka idara ya uhamiaji. Matonya anakabiliwa na mashtaka ya ubakaji kinyume na sheria baada ya kudaiwa kutenda kosa hilo Aprili 7, katika nyumba moja iliyo eneo la Nyali, Kaunti ya Mombasa. Pia anakabiliwa na shtaka mbadala la kutenda kitendo cha aibu kwa mtu mzima. Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena April 30.

Go to News Site