LA TAIFA LEO
WILLIAM Omwansa, mhudumu wa afya ya jamii, anakusanya mayai ya mbu kutoka kwa bwawa moja eneo la Syokimau, Kaunti ya Machakos. Akiwa na vifaa maalum, ikiwa ni pamoja na kijiko cha kuchotea mayai na ndoo yenye kichujio, anazunguka pembezoni mwa bwawa hilo akitafuta ishara za mbu. Amepewa mafunzo na Taasisi ya Utafiti wa Matibabu Kenya (Kemri), ambapo alijifunza kutambua aina tofauti za mayai, kuchagua maeneo bora ya kuyakusanya na kurekodi taarifa muhimu kwa ajili ya utafiti. Kwa uzoefu wake, Omwansa anaeleza kuwa mayai ya mbu wa aina ya Anopheles huwa juu ya maji na huwa hai sana, tofauti na aina nyingine. Baada ya kuyakusanya, huwa anayahifadhi kwenye mirija yenye kemikali maalum kabla ya kupelekwa maabara kwa uchunguzi zaidi. Mbu aina ya Anopheles aligunduliwa kwa mara ya kwanza kaskazini mwa Kenya, hasa katika kaunti za Turkana na Marsabit, na inaaminika kuingia kupitia njia za usafiri kutoka Ethiopia. Asili yake ni Asia Kusini na Arabia, na iligunduliwa barani Afrika kwa mara ya kwanza nchini Djibouti mwaka 2012. Ndani ya muda mfupi, nchi hiyo ilishuhudia ongezeko kubwa la visa vya malaria. Tofauti na mbu wengine wanaopatikana zaidi maeneo ya vijijini, mbu huyu hupendelea mazingira ya mijini, hasa yale yanayotengenezwa na binadamu kama, maeneo ya kuoshea magari, mitaro ya ujenzi na vyombo vya kuhifadhi maji wazi. Hali hii inaongeza hatari ya kuenea kwake katika miji inayokua kwa kasi kama Nairobi na viunga vyake. Watafiti wa Kemri, wakiongozwa na wataalamu wa wadudu, wanazunguka katika kaunti 21 zilizotambuliwa kuwa katika hatari ili kufuatilia kuenea kwa mbu huyu. Tayari, uwepo wake umethibitishwa katika kaunti kadhaa zikiwemo Garissa, Wajir, Mandera, Lamu, Tana River na Kitui. Hata hivyo, bado haijathibitishwa kubeba vimelea vya malaria nchini Kenya, ingawa wataalamu wanaonya kuwa hilo linaweza kubadilika. Katika maabara za Kemri, Kaunti ya Kisumu, sampuli hukaguliwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa kama vile Polymerase Chain Reaction (PCR) na uchambuzi wa vinasaba ili kubaini aina ya mbu na tabia zake. Mbinu hizi husaidia wanasayansi kutofautisha kati ya aina mbalimbali za mbu na hata kubaini tofauti ndani ya spishi moja kulingana na eneo ilikotoka. Mradi wa utafiti unaoendelea, unaojulikana kama AnoSTEP Afrika, unalenga kuchunguza athari za mbu huyu katika juhudi za kudhibiti malaria barani Afrika. Watafiti pia wanachunguza jinsi shughuli za binadamu zinavyochangia kuenea kwake. Ikiwa mbu huyu ataenea mijini, Kenya inaweza kushuhudia mabadiliko makubwa katika kuenea kwa malaria. Ugonjwa ambao kwa muda mrefu umehusishwa na maeneo ya mashambani unaweza kuhamia mijini, na hivyo kuongeza mzigo kwa mifumo ya afya. “Hili linaweza kuwa tatizo kubwa ikiwa hatutachukua hatua mapema,” alisema mmoja wa watafiti. Kwa sasa, juhudi zinaendelea kuelewa tabia ya mbu huyu, maeneo anayopendelea kuishi na mbinu bora za kumdhibiti. Wataalamu wanasisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana kwa kuondoa maji yaliyotuama na kuboresha usafi wa mazingira ili kupunguza hatari ya kuzaliana kwa mbu.
Go to News Site