Collector
Kanisa Katoliki Kahama laja na mpango wa kukuza wajasiriamali | Collector
Kanisa Katoliki Kahama laja na mpango wa kukuza wajasiriamali
Mwananchi

Kanisa Katoliki Kahama laja na mpango wa kukuza wajasiriamali

Kahama. Askofu wa jimbo Katoliki la Kahama Christopher Ndizeye amesema kanisa hilo limedhamiria kutoa huduma bora za kibenki kwa kuwaibua watu wenye mawazo ya biashara na kuwatengeneza kuwa wafanyabiashara wakubwa. Askofu Ndizeye amesema kufanya hivyo ni sehemu ya uinjilishaji na kumtangaza kristo, na kwamba utakatifu unahusiana pia na kufanya kazi kwa uadilifu. Ameyasema hayo leo Mei 2, 2026, wakati wa uzinduzi wa benki ya biashara ya mkombozi tawi la Kahama, katika parokia ya Mtakatifu Karoli Lwanga, Kahama Mjini. Amesema, “Wafanyabiashara wakubwa nao walianza na mawazo, wakayafanyia kazi pengine kwa kusaidiwa na sasa wanaliingizia Taifa mapato makubwa, ninawaasa watumishi wa benki hii kuzingatia uadilifu bila kujali faida kubwa bali huduma kwa wahitaji, ili kuwasaidia wenye mawazo ya biashara.” Amewaasa watumishi wa benki hiyo kufanya kazi kwa misingi ya uadilifu, upendo na kuwajali wengine, kwa kuzingatia mfano wa Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, ili ikawe chachu ya ukuaji wa Kahama kwa kutoa huduma jumuishi za kifedha. Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Mkombozi Tanzania, Respige Kimati amesema benki yao imejikita katika kutambua na kukuza makundi mbalimbali ya wajasiriamali, kuwainua kiuchumi na kukuza shughuli za maendeleo katika jamii. Amesema, “Tumetengeneza mfumo ambao utatambua kila kundi katika jamii, tunaanza kumfikiria mwanajamii mwenye wazo la biashara, kumlea ili kumpata mfanyabiashara mkubwa.” “Kwa hiyo tuna biashara ambazo zimeanza, zingine bado, zingine zipo katikati na zingine hatua ya juu, wote hao tumewatengenezea mfumo ambao hatuwaachi kwa kutazama mazingira wanayofanyia kazi,” ameongeza. Mkazi wa Kahama Ezekia Mafuru amesema, “Tunaomba kama kweli wamedhamiria kutukwamua kwenye mikopo ya mtaani basi wafanye hivyo, maana tusiokuwa na mitaji mikubwa hatutambiliki kabisa kwenye hii mifumo ya ukopeshwaji benki.” Ujio wa Benki ya biashara ya Mkombozi Kahama, unatarajiwa kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa eneo hilo kwa kutoa huduma jumuishi za kifedha kwa watu wa kada mbalimbali bila kujali dini wala kabila.

Go to News Site