Mwananchi
Dar es Salaam. Changamoto ya ramani duni na ukosefu wa njia rafiki za dharura kwa magari ya zimamoto imeendelea kuwa kikwazo kikubwa katika uokoaji wa maisha na mali, hali iliyochochea wito wa kuboresha mipango ya miji ili iendane na mahitaji ya huduma za dharura. Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema bado kuna maeneo mengi jijini hapa yenye miundombinu isiyoruhusu magari ya zimamoto kufika kwa urahisi, jambo linalochelewesha operesheni za uokoaji wakati wa majanga. Amesema ataomba suala hilo lipewe kipaumbele katika ngazi ya mkoa kwa kushirikiana na wadau wa mipango miji, ili kuhakikisha maeneo yote yanapimwa kwa kuzingatia uwepo wa njia za dharura. “Ni lazima tuangalie ramani zetu za miji. Kuna maeneo magari ya zimamoto hayawezi kufika kwa haraka, na hii inatugharimu maisha na mali za wananchi,” amesema Mpogolo. Akizungumza Mei 2, 2026, wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Zimamoto kuelekea Siku ya Zimamoto Duniani, Mpogolo amesema changamoto hiyo imekuwa ikijirudia hasa katika makazi yasiyo rasmi na mitaa yenye msongamano mkubwa. Amesema licha ya hali hiyo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea kufanya kazi kubwa ya kuokoa maisha ya wananchi katika mazingira hatarishi. “Askari hawa ni mashujaa wa kimya kimya. Wanaingia kwenye moto, wanapanda majengo marefu na kuokoa watu bila kujali hatari wanazokabiliana nazo,” amesema. Ameongeza kuwa matukio ya moto katika viwanda na tukio la kuanguka kwa jengo Kariakoo yameonesha wazi umuhimu wa kuboresha mifumo ya ujenzi pamoja na njia za dharura. Aidha, amewataka wananchi kushirikiana na jeshi hilo kwa kuzingatia maelekezo ya usalama na kuhakikisha mazingira yao yanaruhusu huduma za uokoaji kufika kwa haraka. “Maonesho ya zimamoto ni fursa muhimu kwa wananchi kujifunza namna ya kujikinga na majanga. Elimu hii inapaswa kuanzia ngazi ya kaya hadi taasisi,” amesema. Maonesho hayo yanaendelea jijini Dar es Salaam yakihusisha mafunzo kwa wananchi, maonesho ya vifaa vya kisasa na uigizaji wa matukio ya uokoaji, kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu majanga ya moto na namna ya kuyakabili. Mnadhimu wa Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Naibu Kamishna wa Zimamoto (DCF) Taki Nguzo, amesema maadhimisho hayo ni ya kipekee kwa jeshi hilo kwani hutumika kuwaenzi askari waliopoteza maisha wakiwa kazini. “Maadhimisho haya yatafanyika kwa siku tatu, yakihusisha maonesho ya vifaa na utaalamu wa zimamoto na uokoaji. Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kujifunza namna ya kujikinga na majanga,” amesema Nguzo. Kwa mujibu wa Nguzo, kaulimbiu ya mwaka huu, “Tuchukue tahadhari leo, tuokoe maisha na mali kesho,” inalenga kuhamasisha jamii kuchukua hatua za mapema dhidi ya majanga ya moto na dharura nyingine. Amesema kaulimbiu hiyo inaendana na maboresho yanayoendelea ndani ya jeshi hilo, ikiwemo upatikanaji wa mitambo ya kisasa ya kuzimia moto, vifaa vya uokoaji na magari ya dharura. Awali, Kamanda wa Zimamoto Mkoa wa Ilala, Peter Mabusi amesema mkoa wa Dar es Salaam umeongeza vituo vya zimamoto na uokoaji hadi kufikia tisa. Ametaja maeneo hayo kuwa ni Fire, Kariakoo, Chanika, Mchicha (Tazara), Mbagala, Darajani, Stendi ya Magufuli, Lugalo na Mbweni. “Mbali na vituo hivi, tupo mbioni kufungua vingine vinne katika maeneo ya Kinyerezi, Kivuke, Masaki na Kigamboni,” amesema Mabusi.
Go to News Site