Collector
Laikipia yaonyesha njia: Mikakati bunifu yapunguza vifo vya mifugo wakati wa ukame | Collector
Laikipia yaonyesha njia: Mikakati bunifu yapunguza vifo vya mifugo wakati wa ukame
LA TAIFA LEO

Laikipia yaonyesha njia: Mikakati bunifu yapunguza vifo vya mifugo wakati wa ukame

UKAME unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi unaendelea kuwa tishio kubwa kwa wafugaji nchini, ukisababisha vifo vya mifugo, kuporomoka kwa mapato na kuhatarisha usalama wa chakula. Lakini katika Kaunti ya Laikipia, simulizi inaanza kubadilika—mikakati mahususi ya kaunti ikionyesha matumaini mapya kwa jamii zinazotegemea ufugaji. Kwa miaka mingi, wafugaji katika maeneo kame na nusu-kame (ASAL) wamekuwa wakipambana na changamoto za uhaba wa malisho, maji na migogoro ya raslimali. Hata hivyo, hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Kaunti ya Laikipia zinaanza kuzaa matunda, huku idadi ya mifugo wanaofariki kutokana na ukame ikipungua kwa kiasi kikubwa. Gavana Joshua Irungu anasema kaunti imewekeza katika mbinu za kisasa za ufugaji, ikiwemo kuanzisha maeneo maalum ya kunenepesha mifugo (feedlots), kuimarisha uzalishaji wa malisho, na kuongeza thamani ya bidhaa za mifugo. Anasisitiza kuwa mkakati huo unalenga si tu kupunguza vifo vya mifugo, bali pia kubadilisha ufugaji kuwa biashara yenye tija. “Kupitia uwekezaji katika feedlots na uzalishaji wa malisho, tumeimarisha lishe ya mifugo na kuongeza uzalishaji wa nyama na maziwa. Hii imechangia kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za ukame,” alisema Bw Irungu katika mahojiano jijini Nairobi. Mbali na kuboresha lishe ya mifugo, kaunti pia imehamasisha kilimo cha nafaka kwa ajili ya chakula cha mifugo, pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mifugo. Hatua hizi zimewezesha wafugaji kuwa na akiba ya malisho hata wakati wa kiangazi. [caption id="attachment_187660" align="aligncenter" width="300"] Mbuzi wa mfugaji eneo kame. Picha|Sammy Waweru [/caption] Matokeo yake yamekuwa ya kuvutia. Kulingana na gavana huyo, miaka miwili iliyopita, karibu asilimia 60 ya mifugo ilipotea kutokana na ukame mkali. Hata hivyo, kufikia mwanzoni mwa mwaka 2026, kiwango hicho kimeshuka hadi karibu asilimia moja pekee. “Hatua tulizoweka zimeleta tofauti kubwa. Wafugaji sasa wanaweza kustahimili misimu migumu bila kupoteza mali yao yote,” alieleza. Kaunti ya Laikipia, ambayo kwa muda mrefu imekumbwa na changamoto za usalama kama wizi wa mifugo na migogoro ya raslimali, pia imeshuhudia utulivu ukiongezeka. Kulingana na Irungu, kuanzishwa kwa feedlots kumechangia kupunguza migogoro ya malisho na hata visa vya wizi wa mifugo, kwani wafugaji hawalazimiki tena kuhama kwa umbali mrefu kutafuta malisho. Mikakati mingine inayotekelezwa ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa maji, kuendesha kampeni za chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo, na kuanzisha makubaliano na ranchi kubwa ili kuruhusu wafugaji wadogo kulisha mifugo wao wakati wa ukame. Isitoshe, mifumo ya ununuzi wa mifugo (off-take) imekuwa mkombozi kwa wafugaji. “Kupitia mpango huu, wafugaji huuza mifugo yao mapema kabla ya kudhoofika, hivyo kupunguza hasara na wakati huohuo kupata kipato,” Gavana Irungu anaelezea. Mbali na juhudi za ndani, ushirikiano na wadau wa kimataifa umeimarisha zaidi sekta hiyo. Kupitia ufadhili wa Serikali ya Ufaransa, Kaunti ya Laikipia ilinufaika na mpango wa kuboresha biashara uliojulikana kama Farm’Innov. [caption id="attachment_187661" align="aligncenter" width="300"] Kaunti ya Laikipia imeibuka na mpango wa feedlots kusaidia wakazi wafugaji kukwepa hasara zinazotokana na ukame na kiangazi. Picha|Sammy Waweru [/caption] Kupitia ushirikiano na shirika la Agence Française de Développement (AFD), kampuni 14 za chakula na kilimo zilipata mafunzo ya kina ya kukuza biashara zao mwaka 2024. Wajasiriamali hao pia walipata fursa ya kusafiri hadi Ufaransa kwa wiki mbili, ambako walijifunza mbinu za kuimarisha biashara na kupanua mitandao ya kibiashara. Miongoni mwa walionufaika ni Zamzam Haji, mfugaji wa ngamia anayejihusisha na ukusanyaji na uchakataji wa maziwa ya ngamia. Anasema mpango huo ulimwezesha kuboresha biashara yake na kuongeza thamani ya bidhaa zake. “Tunashukuru kwa msaada tuliopata. Umetusaidia kuboresha uzalishaji na kufikia masoko mapya,” alisema Zamzam. Gavana Irungu anasema uimarishaji wa uchakataji wa maziwa, hasa ya ngamia, unatoa fursa mpya kwa wafugaji, akibainisha kuwa kuongeza thamani ya mazao ni nguzo muhimu ya maendeleo ya sekta ya mifugo. “Faida za uwekezaji huu zinaenea hadi kwa jamii pana kupitia ajira, ukuaji wa uchumi na mchango katika pato la taifa,” alisema. Mikakati ya Laikipia inaonyesha kuwa kwa mipango madhubuti, uwekezaji wa kimkakati na ushirikiano na wadau, inawezekana kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kadri ukame unavyozidi kuwa changamoto ya mara kwa mara, mbinu hizi zinaweza kuwa nguzo muhimu kwa kaunti zingine nchini zinazokabiliwa na hali kama hiyo.

Go to News Site