LA TAIFA LEO
ZAIDI ya wakazi 440 wa Kachero, Kaunti ya Taita Taveta, wamepata afueni baada ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi kuruhusu kesi yao kusikilizwa kikamilifu. Wakazi hao wanataka kupewa umiliki wa ardhi ya aliyekuwa Mbunge wa Taveta, Bw Basil Criticos, na Mama Ngina Kenyatta, ambaye ametajwa kama mshtakiwa wa pili. Wengine waliotajwa ni Tume ya Ardhi ya Kitaifa, Mkurugenzi wa Upimaji na Ugawaji Ardhi, Msajili Mkuu wa Ardhi na Mwanasheria Mkuu. Mahakama ilisema hakuna kesi kama hii iliyowahi kuamuliwa awali, hivyo wakazi hao hawawezi kunyimwa nafasi ya kusikilizwa. Pia, ilibainisha kuwa umiliki wa ardhi na Bw Criticos si hoja kuu ya kesi hii, bali inahusu wajibu wa serikali kuwasaidia watu wasio na ardhi. “Kuwazuia walalamishi itakuwa ni kuwanyima haki yao ya kusikilizwa kuhusu masuala ambayo hayajawahi kuamuliwa na mahakama nyingine. Ombi hili litasikilizwa kikamilifu kwa misingi yake,” mahakama ilisema. Wakazi walisema hawapingi umiliki wa Bw Criticos. Wanachotaka ni kutambuliwa kwa matarajio yao ya kupewa makazi kwenye kipande cha ardhi ambacho wanadai aliahidi au alitoa kwao. “Hatupingi umiliki wa Bw Criticos. Tunataka tu ahadi iliyotolewa kwa wakazi wa Kachero itambuliwe na wapewe sehemu yao,” wakasema. Walisema kesi hii ni tofauti na zile za awali ambazo zilihusu tu kutoa hati ya muda ya umiliki wa ardhi nambari LR No. 10287/7. Kulingana nao, kesi hii inahusu haki ya makazi kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Kenya. Walitumia uamuzi wa Mahakama ya Juu kuonyesha kuwa wahusika, masuala na maombi katika kesi hii si sawa na yale ya awali. Bw Criticos, kupitia wakili wake, alipinga hoja hizo. Alisema kesi kama hiyo iliwasilishwa mwaka 2023 na mahakama tayari ilitoa uamuzi Desemba 2025, ikiamuru Msajili Mkuu wa Ardhi kumpa hati ya muda, kufuta hati zisizo halali na kuwasilisha ripoti ya utekelezaji. “Ardhi inayohusika ni ile ile, na Msajili Mkuu wa Ardhi ni mshtakiwa katika kesi zote,” alisema. Pia, alikanusha madai kwamba aliwahi kutoa au kuahidi wakazi hao ardhi. Katika uamuzi wake, mahakama ilieleza kuwa kanuni za kuzuia kurudia kesi au kusikiliza kesi zinazofanana zinatumika tu pale ambapo wahusika, hoja na madai ni sawa. “Kwamba Msajili Mkuu wa Ardhi na Mwanasheria Mkuu wametajwa katika kesi zote hautoshi kuthibitisha kuwa wahusika ni wale wale,” mahakama ilisema. Mahakama ilisisitiza kuwa kesi hii ni ya kikatiba, ikihusu haki za mali, usawa na ulinzi wa kijamii na kiuchumi. Ilibainisha kuwa kesi zilizotajwa na Bw Criticos hazifanani na kesi ya kikatiba iliyowasilishwa na walalamishi kuhusu haki ya makazi. “Mamlaka, masharti, taratibu na jinsi yanavyoshughulikiwa ni tofauti kabisa,” mahakama iliongeza. Mahakama ilihitimisha kuwa kesi ya walalamishi haiwezi kuathirika na kesi za awali ambazo zimesikilizwa. “Wahusika ni tofauti, hoja ni tofauti, na maombi yanayotafutwa si yale yale,” mahakama ilisema. Pia, iliongeza kuwa hatua za utekelezaji katika kesi zilizotajwa na Bw Criticos hazihesabiki kama kesi inayosubiriwa ambayo inaweza kuzuia ombi hili kusikilizwa. Mahakama ilifafanua kwamba maamuzi yanayotolewa katika kesi za uangalizi wa maamuzi ya Mahakama, kama vile amri za kufuta maamuzi au kulazimisha serikali kuchukua hatua fulani, ni tofauti na maamuzi yanayotolewa chini ya Katiba. Maamuzi ya kikatiba yanahusu zaidi kuwapa wananchi fidia na kurejesha haki zao pale ambapo zimekiukwa, na yana upeo mpana zaidi wa kurekebisha madhara yaliyowapata. Kutokana na uamuzi huu, mahakama iliamuru pande zote kuwasilisha majibu na kupanga tarehe ya kesi hiyo kusikilizwa.
Go to News Site