Collector
Ukuzaji nduma unavyoweza kuondoa mkulima kutoka lindi la umaskini | Collector
Ukuzaji nduma unavyoweza kuondoa mkulima kutoka lindi la umaskini
LA TAIFA LEO

Ukuzaji nduma unavyoweza kuondoa mkulima kutoka lindi la umaskini

MWAKA 2018, Sammy Momanyi, 38, alirejea nyumbani kwao kijijini Mwamaranga-Rikendo, eneobunge la Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii kutoka eneo la Naivasha alikokuwa ameajiriwa kazi na kampuni moja. Baada ya kukaa kijijini humo kwa siku chache, aliamua kuikata miti ya mikalatusi (Eucalyptus) ambayo ilikuwa katika ekari mbili za shamba lake. Kwa kuwa wakazi wengi wa sehemu hizo hutegemea kilimo cha miti hiyo ya mikalatusi, ambayo hufanya vyema karibu na vyanzo vya maji, wanakijiji walimwona kama aliyegeuka akili punguani. Lakini baba huyo wa watoto watatu, alikuwa na nia. Alikuwa ameona jinsi kilimo cha nduma kilikuwa kinamzolea mamilioni mmoja wa marafiki zake katika mji wa Kitale na hivyo basi pia yeye akaamua kuing’oa mikalatusi na badala yake kuzamia kilimo cha nduma. Jarida la Akilimali lilimzuru Momanyi shambani mwake kujionea jinsi nduma zilivyomkweza kwenda kiwango kingine kufikia mahali ambapo hawazii kuajiriwa na mtu yeyote kwa kuwa pia anavuna mamilioni kutoka kwa nduma kama rafikiye wa Kitale. “Nilianza na miti 70 ya nduma niliyoitoa alikotoka nyanyangu lakini kwa sasa hivi nina mimea 24,000 katika shamba langu la ekari tatu,” Momanyi alitanguliza. Alihoji kuwa iwapo kuna kilimo ambacho anakifananisha na dhahabu kwa sasa hivi, basi ni nduma. Momanyi anaeleza kuwa ndumaa hufanya vyema katika udongo wenye rotuba nzuri lakini ni sharti udongo huo uwe na kiasi cha haja cha maji. Kulingana na mkulima huyo, shamba hilo pia linafaa kuwa lisilo na changarawe kwani litazuia nduma kutimiza ukubwa unaotamaniwa sokoni. Anaeleza kuwa kabla mkulima yeyote kuanza kilimo chochote, ni vyema kuwatembelea wakulima waliokubuhu kwa kilimo anachokitaka ili ajifunze mawili-matatu ya kutekeleza atakaporudi shambani kwake. Kabla ya kuanza kupanda nduma, Momanyi anasema yeye hutayarisha shamba lake vizuri na kulichimba sawasawa ili kuufanya udongo kuwa mwororo. Kisha anaondoa magugu yote na kuchimba mitaro ya karibu futi moja kwenda chini. Upana kati ya mtaro mmoja hadi mwingine usipite mita moja ili kulitumia shamba vizuri. “Mitaro ikishachimbwa, mwaga mbolea asilia ambayo imeundwa kutokana na samadi ya ng’ombe au mifugo wowote wale wanaofugwa nyumbani.” “Baada ya kuweka mbolea hiyo, leta miche ya nduma na ipande kwa kuipa nafasi katika mitaro iliyochimbwa. Nduma zinapokua, hutoa mimea mingine michanga kando yake na hiyo yaweza kung’olewa na kupandwa kwenye mitaro mingine. Pia, ukishavuna nduma, mashina yanayobaki baada ya kuondoa viazi yanaweza kupandwa tena na yakanawiri,” akaongeza mkulima huyo. Kile mkulima anafaa kuangazia pakubwa ni kuhakikisha kwamba, nduma zilizopandwa hazina udongo mwingi unaokaribia mashina. Hili kulingana na Momanyi, linasaida nduma kuwa kubwa. Momanyi anasema nduma huchukua mwaka mmoja kukomaa. Anaeleza kuwa tangu aanze kilimo hiki, hajawahi kuona nduma zikiathiriwa na magonjwa mengi kama inavyoshuhudiwa katika kilimo kingine. Lakini anaonya kwamba mkulima asijaribu kutumia fatalaiza zinazonunuliwa kwenye maduka. “Fatalaiza za kununua hazisikizani kabisa na nduma. Mbolea hiyo ina kemikali ambazo hukata mizizi ya mimea kuifanya inyauke. Ikiwa mmea ulikuwa umeweka viazi, vitaoza,” Momanyi anaongeza. Aina ya nduma alizozipanda shambani kwake ni zile za majani mabichi yaliyokolea kabisa. Kuna aina nyingine ya nduma zenye majani ya zambarau lakini mkulima huyu anadokeza zile za majani mabichi yaliyokolea zinamletea tija. Anaeleza kuwa yeye huuza nduma moja iliyotimiza uzani wa kilo mbili Sh100. “Kwa sasa hivi nina ndumaa 24,000 katika ekari tatu. Nikiuza nduma moja kwa Sh100, nitakuwa nimetia kibindoni Sh 2,400,000,” anadokeza Momanyi. Ana wateja kutoka miji mingi humu nchini. “Nina wateja kutoka majiji ya Nairobi na Nakuru. Hata kwetu mjini Kisii, nina wateja. Wao hununua hapa shambani na kujibebea wenyewe. Sigharamiki hata kidogo kuwasafirishia hadi barabarani,” anasema. Ili kuhakikisha wateja wake hawakosi nduma kila mara, ameligawanya shamba lake kusitiri mimea iliyoshindana wakati wa kupandwa. Kuna mimea ya nduma iliyomaliza miezi miwili, mingine nne na kuendelea. Hili anasema linamsaidia pakubwa kuvuna kwa wakati tofauti ili wateja wake wasisumbuke. Kutokana na ufanisi wake katika kilimo hicho, Momanyi anadokeza kuwa wakulima kutoka kaunti zingine kama vile Nyandarua, Nakuru, Migori, Laikipia na zingine wamekuwa wakimiminika shambani mwake wakitaka mafunzo kuhusu kilimo hicho. “Wao huja hapa kusoma baada ya kunifahamu kupitia mitandao ya kijamii. Wakija, mimi huwapa mafunzo hayo kwa ada fulani na wengine hununua mbegu za kujianzishia kilimo hiki na ninapata faida tele,” anaeleza. Mkulima huyo anaongeza kuwa mapato kutoka kwa nduma yamemsaidia kujiimarisha yeye pamoja na familia yake. Ndiko anakotoa hela za kuwalipia wanawe karo. Kutokana na faida ya nduma, pia amefanikiwa kununua vipande vingi vya ardhi anakofanyia ukulima mwingine kama ule wa miwa ya kutafuna na mahindi. Pia, nduma zimemwezesha kununua kipande cha ardhi katika jiji la Nakuru ambapo anapanga kujenga nyumba za kukodisha. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Momanyi anasema anataka kugeuza shamba lake kuwa kituo kikubwa cha kutoa mafunzo ya kilimo cha nduma. Anasema japo kwa sasa anatoa mafunzo hayo, kiwango hicho hakijaafikia mawaza na malengo yake. Anawarai wakulima wengine kuiga mtindo wake na kujiondoa katika lindi la umasikini kwa kulima nduma. Nduma zinaweza kutumiwa wakati wa kiamsha kinywa na zina kiwango kikubwa cha madini aina wanga. Wataalamu wa afya wanahoji ulaji wa nduma husaidia mwili kuwa na kinga tosha mwilini dhidi ya magonjwa mbali mbali.

Go to News Site