Collector
DC awapa jukumu wananchi kudumisha Amani, mshikamano wa kitaifa | Collector
DC awapa jukumu wananchi kudumisha Amani, mshikamano wa kitaifa
Mwananchi

DC awapa jukumu wananchi kudumisha Amani, mshikamano wa kitaifa

Dodoma. Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri amewataka wananchi wa Kata ya Mnadani kuendelea kudumisha mshikamano, amani na ushirikiano ili kuhakikisha maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 16 ya kata hiyo yanaendelea kuongezeka na kuwanufaisha wananchi wote. Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 16 ya kuanzishwa kwa Kata ya Mnadani yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mbwanga jijini Dodoma, Shekimweri alisema kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wananchi pamoja na viongozi wa kata hiyo kuhakikisha huduma muhimu za kijamii zinaboreshwa kwa lengo la kuinua hali ya maisha ya wananchi. “Katika kipindi cha miaka 16, Kata ya Mnadani imefanikiwa kupiga hatua kubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo elimu, afya, biashara, mazingira pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara na huduma za maji, hali ambayo imechangia kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo. “Tunapaswa kujivunia mafanikio haya, lakini bado tunao wajibu wa kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha maendeleo yanaendelea kupatikana. Serikali ipo tayari kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili,” amesema Alhaj Shekimweri. Aidha, Shekimweri amewataka vijana kutumia fursa zilizopo kujiajiri kupitia mikopo inayotolewa na halmashauri pamoja na kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali badala ya kujihusisha na vitendo visivyo na tija kwa jamii. Pia aliwahimiza wazazi na walezi kuendelea kusimamia maadili ya watoto ili kujenga jamii yenye nidhamu na uwajibikaji. Katika maadhimisho hayo, Mtendaji wa Kata ya Mnadani, Credo Msabaha amesema Kata ya Mnadani ilianzishwa tarehe 7 Mei 2010 na kwamba tangu kuanzishwa kwa kata hiyo, miaka 16 imepita huku kukiwa na mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma kwa wananchi. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, madiwani, wenyeviti wa mitaa, watendaji na wananchi, jambo lililoonesha uzalendo na mshikamano wa jamii katika kufuatilia maendeleo yao.

Go to News Site