Collector
Unafahamu kuwa chakula na maji unayokunywa yanatokana na nyuki? | Collector
Unafahamu kuwa chakula na maji unayokunywa yanatokana na nyuki?
LA TAIFA LEO

Unafahamu kuwa chakula na maji unayokunywa yanatokana na nyuki?

KATIKA kipindi hiki cha mabadiliko ya tabianchi, uzalishaji wa chakula duniani unazidi kuwa kwenye njiapanda na hatarini. Lakini mbali na ukame, mvua zisizotabirika na gharama ya uzalishaji kupanda, kuna tishio jingine ambalo wengi hulipuuza—kutoweka kwa nyuki. Wadudu hawa wadogo wana mchango mkubwa mno katika uzalishaji wa chakula kuliko wengi wanavyofahamu. Bila nyuki, mazao mengi yasingeweza kuzaa kwa kiwango kinachohitajika, ubora wa matunda na mboga ungeshuka, huku mifumo ya kilimo ikiathirika. Nyuki ndio wachavushaji wakuu wa mimea (pollinators). Kupitia uchavushaji mtambuka (cross pollination), wanahakikisha maua yanageuka kuwa matunda, mbegu na mazao yenye tija. Pia, husaidia uchavushaji mtambuka wa mimea, jambo linaloongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa mazao mashambani. Kulingana na Dkt Monica Olala, Mkuu wa Maendeleo ya Raslimali za Wanyama chini ya Idara ya Maendeleo ya Mifugo inayosimamia pia ufugaji nyuki, mchango wa nyuki haupaswi kupimwa kwa asali pekee. “Watu wengi bado wanaamini nyuki yupo kwa ajili ya asali pekee, lakini ukweli ni kwamba mchango wao mkubwa uko katika uchavushaji wa mazao. Bila nyuki, uzalishaji wa chakula ungeathirika pakubwa,” anasema. [caption id="attachment_187899" align="aligncenter" width="300"] Dkt Monica Olala, Mkuu wa Maendeleo ya Raslimali za Wanyama chini ya Idara ya Maendeleo ya Mifugo inayosimamia pia ufugaji nyuki, wakati wa mahojiano Jijini Nairobi. Picha|Sammy Waweru [/caption] Anafafanua kuwa karibu asilimia 75 ya mazao yanayolimwa hutegemea uchavushaji wa nyuki kwa kiwango fulani. Hivyo, kulinda nyuki ni sawa na kulinda uzalishaji wa chakula na uchumi wa kilimo. “Tukiwekeza zaidi katika ufugaji nyuki na utunzaji wa mazingira yao, tutaimarisha sekta nzima ya kilimo,” anaongeza. Mbali na mazao ya chakula, nyuki pia wana mchango mkubwa katika uzalishaji wa malisho ya mifugo. Dkt Olala anasema nyuki huchavusha mimea inayotumika kama chakula cha mifugo, jambo linaloongeza upatikanaji wa malisho bora. “Kenya kwa sasa inakidhi takribani asilimia 40 pekee ya mahitaji ya malisho ya mifugo. Pengo lililopo linaathiri wafugaji wa ng’ombe wa maziwa, nyama na kuku. Uchavushaji bora kupitia nyuki unaweza kusaidia kuongeza uzalishaji wa malisho,” anasema. Licha ya umuhimu huo mkubwa, sekta ya ufugaji nyuki nchini bado inakabiliwa na changamoto nyingi. Takwimu za mwaka 2024 kutoka Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo zinaonyesha kuwa Kenya huzalisha karibu tani 19,000 za asali kwa mwaka, kiwango kilichoshuka kutoka tani 35,000 zilizokuwa zikizalishwa hapo awali. Kuporomoka huku kwa uzalishaji wa asali kunahusishwa na mabadiliko ya tabianchi, matumizi holela ya dawa za kemikali mashambani na uvamizi wa nzige ulioshuhudiwa kati ya mwaka 2019 na 2021. [caption id="attachment_187900" align="aligncenter" width="300"] Nyuki ni mdudu muhimu sana katika uzalishaji wa asali. Picha|Sammy Waweru [/caption] “Kipindi kirefu cha ukame, mvua zisizotabirika na uharibifu wa mazingira hupunguza mimea ya maua ambayo ni chanzo cha chakula kwa nyuki. Aidha, matumizi ya dawa za kemikali yameharibu makundi mengi ya nyuki,” anaeleza. Anakumbusha taifa kuwa kuwa wakati wa operesheni za kudhibiti nzige katika baadhi ya maeneo, makazi ya nyuki na mizinga mingi iliathirika vibaya, huku baadhi ya maeneo yakipoteza hadi asilimia 50 ya nyuki. Kwa wakulima, ujumbe wake ni wazi: hata kama hawafugi nyuki, bado wanawahitaji. “Bila uchavushaji, mavuno hupungua na ubora wa mazao hushuka. Nyuki ni sehemu muhimu ya mfumo wa uzalishaji wa chakula na uchumi wa kilimo,” anasema. Isitoshe, Dkt Olala anasema maadhimisho ya kimataifa ya Siku ya Nyuki Duniani, yaani World Bee Day ambayo huadhimishwa kila Mei 20, ni jukwaa muhimu kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kutunza nyuki na kuhifadhi mazingira yao. [caption id="attachment_187901" align="aligncenter" width="300"] Wafugaji wa nyuki katika Kaunti ya Nyeri wakiwa kwenye jengo maalum la nyuki - apiary. Picha|Sammy Waweru [/caption] Anadokeza kwamba maadhimisho ya mwaka huu, 2026, yatafanyika Mama Ngina Drive, Mombasa, yakilenga kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo pamoja na kuonyesha bidhaa zitokanazo na nyuki. “Madhumuni ni kuhamasisha jamii kuelewa kuwa nyuki si wadudu wa kawaida. Ni msingi muhimu wa uzalishaji wa chakula, lishe na uchumi,” anasema. Aidha, Kenya imepanga kuandaa mbio za nyika za kimataifa mwaka 2027 kama sehemu ya kampeni ya kuhamasisha uhifadhi wa nyuki na mazingira yao. Kadri dunia inavyokabiliwa na changamoto za usalama wa chakula na mabadiliko ya tabianchi, wataalamu wanaonya kuwa kulinda nyuki si hiari tena, bali ni jukumu la pamoja kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

Go to News Site