LA TAIFA LEO
WAKAZI wa kijiji cha Chesongo, Baringo Kati, wamebaki wakishangaa baada ya daraja jipya la watembea kwa miguu kusombwa na mafuriko saa chache tu baada ya kuzinduliwa rasmi. Daraja hilo lilizinduliwa Jumapili na Afisa Mkuu wa Kilimo wa Kaunti ya Baringo, Milka Toromo, ambaye pia anawania kiti cha ubunge cha Baringo Kati. Hata hivyo, usiku huo huo mafuriko makubwa yalilisomba daraja hilo lililokuwa limejengwa kwa chuma na simiti. Kwa miaka mingi, wakazi walikuwa wakitumia daraja la mbao kuvuka mto huo hasa wakati wa mvua. Watoto wa shule ndio wamekuwa waathiriwa wakuu kwa kulazimika kuhatarisha maisha yao kila mto ulipofurika. Wakazi walichanga Sh500 kwa kila familia kujenga daraja jipya lakini fedha hazikutosha. Bi Toromo na wafadhili wengine walichangia zaidi ya Sh150,000 kukamilisha mradi huo. Mkazi Vincent Kiloo alisema alitumia daraja hilo kupeleka mtu hospitalini Jumapili mchana lakini Jumatatu akaarifiwa lilikuwa limesombwa. “Bado nashangaa jinsi daraja la chuma na simiti linaweza kusombwa ndani ya siku moja ilhali lile la mbao lilidumu zaidi ya miaka mitano,” alisema. Wakazi walipata mabaki ya daraja hilo umbali wa mita 200 chini ya mkondo wa mto. Baadhi ya wakazi sasa wanadai daraja hilo lilijengwa vibaya kwa kutumia vifaa dhaifu. “Hilo daraja lilikuwa janga linalosubiri kutokea,” alisema mkazi mwingine, Edwin Chacha. Alisema wakazi walikuwa wameonya kuwa chuma zilikuwa dhaifu mno kuhimili nguvu za mafuriko. Wakazi sasa wanaomba serikali ya kaunti kuwasaidia kujenga daraja jipya huku watoto wakilazimika kubebwa mgongoni kuvuka mto kwenda shule.
Go to News Site