LA TAIFA LEO
WADAU katika sekta ya uchapishaji wa vitabu nchini wameitaka serikali kuimarisha sheria za kudhibiti wizi wa vitabu maarufu kama book piracy , wakisema tatizo hilo linawanyima waandishi mapato na kuhatarisha mustakabali wa tasnia ya fasihi nchini. Kulingana na Chama cha Wachapishaji Vitabu Kenya (KPA), uchapishaji haramu wa vitabu vya fasihi na masomo unasababisha sekta hiyo kupoteza zaidi ya Sh3 bilioni kila mwaka. Wadau hao pia wameitaka serikali kuondoa ushuru wa VAT kwenye vitabu, wakisema gharama kubwa ya vitabu halali inawasukuma wazazi na wanafunzi kununua nakala bandia ambazo ni nafuu. Matamshi hayo yalitolewa wakati wa hafla ya pili ya Tuzo za TBC Penmanship iliyofanyika katika ukumbi wa Jain Bhavan Auditorium, Loresho, jijini Nairobi, kwa lengo la kuwatuza waandishi wa Kenya. Hafla hiyo iliwaunganisha waandishi, wachapishaji, walimu, wanafunzi na wadau wengine wa sekta ya fasihi. Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Text Book Centre, Sachin Varma, alisema tuzo hizo zimeendelea kuwapa waandishi chipukizi nafasi ya kuonyesha vipaji vyao. “Kila mwaka tunapoandaa Tuzo za Penmanship, tunapanua nafasi kwa mwandishi mmoja zaidi ambaye huenda asingepata jukwaa hili. Hivi ndivyo mazingira bora ya fasihi yanavyojengwa,” alisema Varma. Naye Profesa Miriam Maranga-Musonye wa Chuo Kikuu cha Nairobi alisema fasihi ina nafasi muhimu katika kuhifadhi historia, tamaduni na simulizi za jamii. “Jamii hujiona kupitia fasihi yao, historia yao na hata mustakabali wao,” alisema Profesa Maranga-Musonye. [caption id="attachment_188136" align="alignnone" width="1600"] Washikadau wakati wa Tuzo za TBC Penmanship iliyofanyika katika ukumbi wa Jain Bhavan Auditorium, Loresho, jijini Nairobi. PICHA|WINNIE ONYANDO[/caption] Alihimiza wadau wa sekta hiyo kushirikiana ili kujenga mfumo endelevu utakaoimarisha ukuaji wa fasihi nchini. Nao Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji Vitabu Kenya Musyoki Muli, mwandishi Chris Madison na Sharon Banda wa East African Educational Publishers walizungumzia fursa zinazojitokeza kwa waandishi wa Afrika. Tuzo hizo ziliwatambua waandishi bora katika vitengo mbalimbali ikiwemo vitabu vya watu wazima, vijana, watoto na maktaba bora za shule. Miongoni mwa washindi waliotuzwa ni mwanahabari Janet Mbugua kwa kitabu chake My First Time, Dkt Anuradha Khoda kwa kitabu Noah and the Rainbow Promise Series 2 na Jackson Biko kwa kitabu Big Little Fights. Watoto walio chini ya miaka 13 walioandika na kuchapisha vitabu pia walituzwa. Baadhi yao ni Joseph Laight wa Potter House School kwa kitabu The Big Tomato, Joseph Yohan Ayiro wa WoodCreek Schools kwa kitabu Big Africa pamoja na Maya M. na Nia M. wa Kiota School kwa kitabu To the Land of Magic. Mkuu wa Kitengo cha Rejareja wa Text Book Centre, Joy Okumu, alisema taasisi hiyo itaendelea kusaidia ukuaji wa fasihi nchini kupitia Tuzo za Penmanship na kuwahamasisha watoto kuanza kuandika mapema.
Go to News Site