Collector
Uhuru, Gachagua kupimana nguvu katika uchaguzi mdogo Ol Kalou | Collector
Uhuru, Gachagua kupimana nguvu katika uchaguzi mdogo Ol Kalou
LA TAIFA LEO

Uhuru, Gachagua kupimana nguvu katika uchaguzi mdogo Ol Kalou

UCHAGUZI mdogo wa eneobunge la Ol Kalou ambao umeratibiwa kufanyika Julai 16 umefichua mvutano unaozidi kuongezeka kati ya chama cha Jubilee, kinachohusishwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, na kile cha Democracy for Citizens Party (DCP) cha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Licha ya vyama hivyo kuonekana kushirikiana ndani ya muungano wa upinzani, sasa vimeingia katika mgogoro wa wazi kuhusu nani anafaa kupeperusha bendera ya muungano kwenye uchaguzi huo mdogo. Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee, Zack Kinuthia, amesema tofauti hizo zinatokana na makubaliano ya awali ndani ya muungano kwamba chama kilichokuwa kinashikilia kiti kabla ya uchaguzi ndicho kingepewa nafasi ya kuwa na mgombeaji. Alisema kwa kuwa marehemu mbunge wa Ol Kalou, Njuguna Kiaraho, alikuwa mwanachama wa Jubilee chama hicho kilitarajia kuungwa mkono na washirika wengine. “Tulishangazwa na hatua ya Gachagua kusisitiza kuwa DCP pia itatoa mgombea wake licha ya makubaliano yaliyokuwapo,” alisema Kinuthia. Muungano wa upinzani unajumuisha Jubilee, DCP, Wiper ya Kalonzo Musyoka, People’s Liberation Party ya Martha Karua, DAP-Kenya ya Eugene Wamalwa pamoja na Democratic Party (DP) ya Justin Muturi. Hata hivyo, Gachagua amesisitiza kuwa kila chama ndani ya muungano kina haki ya kujijenga kisiasa kwa kushiriki uchaguzi mdogo. “Vyama vyote vijitokeze Ol Kalou. Kila chama kinachoamini kina nguvu kijaribu bahati yake kwa wananchi ili tujue ukweli wa kisiasa,” alisema Gachagua. Alisema hatarudia kile alichoita kosa la kisiasa alilofanya katika uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini mwaka jana alipomuondoa mgombea wa DCP na kuunga wa DP. Kwa sasa chama cha UDA kimemteua Muchina Nyagah, DCP imemsimamisha Kamau Ngotho, Jubilee itampigia debe Wilson Kigwa huku People’s Liberation Party ikipepeta ngoma ya Martin Wambugu. Mvutano huo umeongeza sintofahamu kuhusu mustakabali wa muungano wa upinzani kuelekea uchaguzi mkuu 2027. Aidha, hali hiyo imechochewa zaidi na hatua ya Uhuru Kenyatta kumuunga mkono aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kama mgombea anayependelea kuwania urais 2027, wakati Gachagua naye ameonyesha nia ya kujitosa debeni mwenyewe. Wachambuzi wa siasa wanasema mvutano huo unaonyesha vita vya kuwania ushawishi wa kisiasa eneo la Mlima Kenya kati ya kambi ya Gachagua na ile ya Uhuru. Mchanganuzi Mixson Gitau amesema tofauti kubwa kati ya Jubilee na DCP ni juhudi za Dkt Matiang’i kujijenga kisiasa Mlimani, hatua ambayo inaonekana kutishia ushawishi wa Gachagua. Kwa upande wake, mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa DCP, Maina Kamanda, alisema vyama ndani ya muungano wa upinzani huo vinafaa kuruhusiwa kujijenga katika maeneo yao kabla kuamua mgombea wao mmoja wa urais. Lakini wachambuzi wengine wanaamini mvutano huo unaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa zaidi iwapo vyama hivyo vitashindwa kuelewana kuhusu mikakati ya 2027. Mchanganuzi Festus Wangwe alisema baadhi ya viongozi Mlimani wanaamini Gachagua anaweza kuzuiwa kuwania wadhifa wa umma kutokana na mchakato wa kumuondoa mamlakani mwaka 2024, jambo ambalo limewafanya kuanza kujipanga kuchukua nafasi yake kisiasa. Hata hivyo, Gachagua amesisitiza kuwa hahitaji wadhifa katika serikali ili kuwa na ushawishi mkubwa kisiasa nchini.

Go to News Site