LA TAIFA LEO
FAMILIA ya mwimbaji wa nyimbo za injili Rachel Wandeto aliyefariki baada ya kuchomwa imetoa wito kwa polisi kuharakisha uchunguzi kuhusu shambulio la kikatili lililosababisha kifo chake, na kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa mahakamani. Msemaji wa familia hiyo, Susan Wandeto, jana alisema kuwa familia imehuzunishwa sana na tukio hilo na inaomba utulivu huku Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ikiendelea na uchunguzi. “Tunaheshimu uhuru wa kujumuika kama familia; iwe ni mtu wa kuunga muhula mmoja au miwili. Hatutaki kuchukua upande wowote katika suala hili lakini tunataka DCI ipate muda wa kuchunguza na kutoa ripoti kamili kuhusu kilichotokea,” alisema. Alithibitisha kuwa baadhi ya wanafamilia tayari wamehojiwa na wapelelezi ili kusaidia kubaini chanzo na wahusika wa shambulio hilo. Wandeto alifariki akiwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta baada ya kupata majeraha makubwa katika tukio la kushambuliwa na watu wasiojulikana eneo la Mwiki, Kasarani. Ameacha watoto wawili. Inadaiwa alipata majeraha katika takriban asilimia 70 ya mwili wake. Kifo chake kimezua ghadhabu nchini, huku viongozi na wananchi wakilaani tukio hilo na kutaka haki itendeke. Jana, viongozi wa wanawake walifanya maandamano Nairobi wakitaka haki ipatikane na kukemea ghasia dhidi ya wanawake. Familia pia inataka serikali kusaidia katika mipango ya mazishi ili apate mazishi ya heshima. Serikali imetakiwa kuhakikisha waliohusika wanakamatwa haraka.
Go to News Site