LA TAIFA LEO
BIASHARA haramu ya nyama na ngozi za punda imeendelea kushamiri nchini licha ya serikali kupiga marufuku uchinjaji kibiashara wa wanyama hao mwaka wa 2020. Katika tukio la hivi karibuni, wakazi wa eneo la Kimuka, Kaunti ya Kajiado, walinasa lori lililokuwa likisafirisha nyama inayoshukiwa kuwa ya punda pamoja na ngozi zake. Wakazi wenye hasira waliwachapa wanaume wawili waliokuwa ndani ya lori hilo kabla ya polisi kuwaokoa na kisha kuchoma sehemu ya mbele ya gari hilo. Kamanda wa Polisi wa Kajiado Magharibi Maureen Jepkemboi, alisema wakazi walidhani lori hilo lilikuwa limebeba mifugo yao iliyoibwa lakini walipolifungua walipata nyama ya punda iliyofungwa kwa magunia. Ripoti ya maafisa wa mifugo ilithibitisha kuwa nyama hiyo ilikuwa ya punda 30 huku ngozi zao pia zikikamatwa. Katika Kaunti ya Kitui, maafisa walikamata ngozi zaidi ya 4,000 za punda mwezi Aprili mwaka huu zikiwa zimehifadhiwa kwa chumvi tayari kwa kuuzwa sokoni. Ngozi nyingine 3,720 pia zilinaswa zikisafirishwa bila vibali.
Go to News Site