Mwananchi
Dar es Salaam. Serikali imeanza mchakato wa kujenga magati 12 katika Bandari ya Dar es Salaam kukabiliana na ongezeko la mizigo na msongamano wa meli. Kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Serikali imesema ongezeko la mizigo na meli limeanza kuzidi uwezo wa miundombinu iliyopo, hivyo kuhitaji uwekezaji zaidi katika magati, maeneo ya kuhifadhi mizigo na usafirishaji. Mkurugenzi wa TPA, Plasduce Mbossa amesema hayo leo Mei 23, 2026 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ilipotembelea bandari hiyo. Amesema kwa sasa kuna magati 12 ya mizigo ya kawaida na mawili ya mafuta, lakini uwezo huo hautoshelezi kutokana na kuongezeka kwa biashara. Mbossa amesema Serikali tayari imeanza ujenzi wa magati mawili mapya yenye urefu wa mita 500 katika eneo la Malindi Wharf, huku mpango ukiwa kujenga mengine 10 kuongeza uwezo wa kuhudumia meli nyingi zaidi kwa wakati mmoja. “Kwa kawaida eneo la kazi linapaswa kutumika kwa asilimia 60 ili mitambo ifanye kazi vizuri, lakini sasa matumizi yamefikia asilimia 90,” amesema. Amesema msongamano huo umeathiri ufanisi wa shughuli za upakuaji na upakiaji mizigo, hali inayosababisha wakati mwingine magari kuzuiwa kuingia bandarini kupisha ushushaji wa mizigo kutoka melini. Mbossa amesema pamoja na changamoto hizo, ongezeko la mizigo linaonyesha mafanikio ya maboresho yaliyofanywa bandarini pamoja na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia makasha 1,084,719 kutoka makasha 865,329 kipindi kama hicho mwaka uliopita, sawa na ongezeko la asilimia 25.4. Shehena ya nchi jirani nayo iliongezeka kwa asilimia 25.3 kutoka tani milioni 9.76 hadi tani milioni 12.24, huku mapato yakiongezeka kutoka Sh716.2 bilioni hadi Sh907.9 bilioni. Mbali na ujenzi wa magati, TPA inaendelea kuboresha eneo la Kurasini (Ex-EPZA) lenye uwezo wa kuhifadhi makasha 700,000 pamoja na kununua mitambo ya kisasa. Mbossa amesema ifikapo mwaka 2030 bandari hiyo inatarajiwa kuhudumia tani milioni 60 za mizigo, jambo litakalohitaji uwekezaji mkubwa zaidi katika magati, reli, barabara na maeneo ya kuhifadhi mizigo. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali pia inaongeza matumizi ya reli ya kisasa ya SGR kupunguza msongamano wa malori bandarini. Amesema reli hiyo tayari imeunganishwa bandarini na maandalizi yanaendelea ili kuanza kusafirisha angalau makontena 1,000 kwa siku kwenda Kwala na maeneo mengine kuanzia Juni Mosi. Mbali na Kwala, Serikali pia inajenga vituo vya makontena katika maeneo mbalimbali ikiwemo Morogoro kwa ajili ya mizigo inayokwenda Mbeya, Iringa, Ruvuma na Zambia. Wabunge wamepongeza maboresho hayo huku wakitaka Serikali kuongeza kasi ya uwekezaji wa miundombinu. Mbunge wa Mtoni Zanzibar, Aboubakar Mohammed Mussa amesema SGR itaongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam katika kuhudumia mizigo ya nchi jirani. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Masanja Kadogosa amesema Serikali inapaswa kuongeza uwekezaji katika magati mapya kutokana na mchango wake mkubwa katika mapato ya Taifa.
Go to News Site