LA TAIFA LEO
KAMPENI za chama cha UDA ambacho ni chama kikubwa zaidi katika muungano wa Kenya Kwanza, ziliwapa Wakenya hasa wa tabaka la chini imani kuwa changamoto zao zimo mikononi mwa chama kinachowaelewa zaidi kama watu wa mapato ya chini. Wengi walijipachika jina ‘Hasla’, kauli iliyotumiwa na chama hicho kujinasibisha na watu wa maisha ya kiwango cha chini. Kwa wapigakura, ilikuwa ishara kuwa iwapo mapato yao ni ya chini kabisa wangeimarika kiuchumi kama walivyohaidiwa na UDA wakati wa kampeni. Ahadi za mbivu walizotarajia wananchi zimepeperuka, wananchi waking'amua ukweli kuwa dhiki zao hazitaondoka leo wala kesho. Ingawa kumekuwa na miradi inayolenga kuwainua wananchi kimapato, Wakenya wengi wangali wanahangaika kwa ukosefu wa ajira. Walio na ajira nao wanalalamika kwa sababu ya ongezeko la ushuru unaoendelea kupunguza kipato chao. Ongezeko la bei ya mafuta na ushuru unaosababisha ongezeko la bei za bidhaa ni changamoto kwa Wakenya. Hali ya kiuchumi inaendelea kuwa ngumu kuliko walivyotarajia. Tukio hilo limeishusha hadhi ya Kenya Kwanza na kuifanya vigumu kunadiwa kwa wananachi. Wiki jana, msemaji wa serikali Isaac Mwaura alipigiwa kelele na wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kenyatta alipojaribu kupigia debe rekodi ya serikali ya Kenya Kwanza na kuwauzia kauli ya ‘tutam,’ inayohusishwa na kuchaguliwa kwa pili kwa rais Wiliam Ruto. Hii ni ishara kuwa vijana hawana imani wala matumaini ya kuimarika kwa maisha yao kupitia uongozi wa sasa. Vijana ndio asilimia kubwa ya wapigakura waliojisajili katika awamu iliyokwisha kufanya hivi juzi na huenda watabadili mkondo wa jinsi kura zinavyopigwa kwenye uchaguzi wa 2027. Katika kaunti ya Uasin Gishu, Mwakilishi wa Wanawake Gladys Boss Sholei pia alipigiwa kelele na wananchi alipohudhuria mkutano wa umma. Baadhi ya wananchi katika eneo hilo, walilalamika kwa changamoto katika utekelezaji wa Bima ya Afya SHA pamoja na mfumo mpya wa kufadhili wanafunzi wa chuo kikuu. Baadhi ya Wakenya hawajaridhika na jinsi mgomo wa Matatu ulivyosuluhishwa wiki jana. Kwao viongozi wa wamiliki wa matatu hawakuwakilisha wananchi ipasavyo kwani mzigo wa bei ya mafuta uliachiwa wananchi badala ya kupunguzwa. Changamoto zinazowakumba Wakenya kiuchumi zimesababisha baadhi yao kumkimbilia rais jukwaani anapohotubia wananchi ili shida zao zitatuliwe. Iweje wananchi wanamsubiri raisi ndiposa wahatarishe maisha yao kupata suluhisho za shida zao. Viongozi katika serikali ya Kenya Kwanza wameonyesha utepetevu kwa kutowatimizia wananachi waliobanwa kiuchumi haja zao. Ikumbukwe kuwa hii si mara ya kwanza ya tukio kama hilo kutokea. Ni wazi kuwa hali ngumu ya uchumi imepunguza hadhi ya Kenya Kwanza. Serikali inahitaji mikakati ya dharura ili kurejesha imani yake kwa wananchi.
Go to News Site