Collector
Sh3.313 trilioni zatumwa na Diaspora Tanzania | Collector
Sh3.313 trilioni zatumwa na Diaspora Tanzania
Mwananchi

Sh3.313 trilioni zatumwa na Diaspora Tanzania

Dar es Salaam. Fedha zinazotumwa na Watanzania wanaoishi nje ya nchi zimeongezeka hadi kufikia Sh3.313 trilioni katika mwaka wa fedha 2024/25, hatua inayoonyesha kuongezeka kwa mchango wa diaspora katika uchumi wa nchi. Hayo yamebainishwa na Waziri ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo bungeni jijini Dodoma, leo Jumanne, Mei 26, 2026 wakati akiwasilisha bajeji ya wizara hiyo katika mwaka 2026/2027 ya Sh359.3 bilioni. Kwa mujibu wa Kombo, fedha hizo zimeongezeka kutoka Sh2.11 trilioni mwaka 2023/24, sawa na ongezeko la asilimia 57 ikiwa ni sihara ya kuimarika kwa mazingira ya ushiriki wa diaspora katika uwekezaji, maendeleo ya ujuzi na uchumi wa nchi. “Ukuaji huu unaonyesha umuhimu wa diaspora katika kuboresha maisha ya wananchi, kuongeza uwekezaji na kuchangia ukuaji wa sekta ya fedha nchini,” amesema. Amesema ongezeko hilo linaonyesha imani kubwa ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi kwa sera za Serikali na mazingira yaliyowekwa kuwezesha uwekezaji na ushiriki wao katika maendeleo ya taifa. Waziri huyo amesema Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya mwaka 2024 imeweka msisitizo mkubwa kwenye ushiriki wa diaspora kama sehemu muhimu ya diplomasia ya uchumi, hasa katika kuvutia uwekezaji, utaalamu na mtiririko wa fedha nchini. Ili kuimarisha ushiriki huo, Serikali imekuwa ikiendesha kliniki maalumu za huduma kwa diaspora katika nchi mbalimbali ikiwemo Uholanzi, Ujerumani, Ubelgiji, Falme za Kiarabu, Oman na Botswana. Kupitia huduma hizo, Watanzania wanaoishi nje wamekuwa wakipata msaada wa masuala ya uhamiaji, uwekezaji, usajili wa vitambulisho vya taifa pamoja na ushauri wa kifedha. Aidha, Serikali imeboresha mfumo wa kidigitali wa Diaspora Digital Hub (DDH) kwa lengo la kuboresha ukusanyaji wa taarifa na mipango ya sera zinazohusu diaspora. Kombo amesema hadi Mei 14, 2026 jumla ya wanadiaspora 3,065 walikuwa wamejisajili kwenye mfumo huo, huku maboresho yanayoendelea yakitarajiwa kuongeza ushiriki zaidi. Katika hatua nyingine, Serikali kwa kushirikiana na benki za biashara imeanzisha huduma maalumu za kifedha kwa diaspora ili kurahisisha uwekezaji na miamala ya fedha kutoka nje ya nchi. Baadhi ya huduma hizo ni pamoja na TCB Nyumbani, Azania Asili Account, NBC Twiga Diaspora Banking, CRDB Tanzanite Account, Absa Mzawa Account na NMB Kwetu Account. “Huduma hizi zimewarahisishia Watanzania wanaoishi nje kuwekeza, kuweka akiba na kutuma fedha nyumbani,” amesema Kombo. Kwa mujibu wa waziri huyo, ushiriki wa diaspora katika mifuko ya uwekezaji pia umeendelea kuongezeka ambapo uwekezaji katika UTT AMIS ulifikia Sh11.712 bilioni Februari 2026 kutoka Sh7.5 bilioni mwaka mmoja uliopita. Sekta ya nyumba nayo imeendelea kunufaika na uwekezaji wa diaspora baada ya uwekezaji katika ununuzi wa nyumba na viwanja kufikia Sh4.19 bilioni mwaka 2025/26 kupitia miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na taasisi nyingine za maendeleo ya makazi. Kombo amesema Serikali pia inajiandaa kufanya zoezi la kutambua na kuainisha maeneo wanakoishi Watanzania nje ya nchi kupitia mpango wa “Diaspora Mapping” utakaotekelezwa kwa miaka miwili kuanzia Juni 2026 kwa kushirikiana na International Organization for Migration. Amesema mpango huo utasaidia kuboresha mipango, utoaji wa huduma na ushirikishwaji wa diaspora katika maendeleo ya taifa. Katika hatua nyingine, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa miaka mitano wa ukarabati na uendelezaji wa majengo ya balozi za Tanzania nje ya nchi kwa kushirikisha mifuko ya hifadhi ya jamii, benki na sekta binafsi. Miradi inayoendelea ni pamoja na ujenzi wa majengo ya biashara katika ubalozi wa Tanzania mjini Nairobi pamoja na jengo la biashara Kinshasa kwa ushirikiano na National Social Security Fund. Mazungumzo pia yanaendelea na CRDB Bank kwa ajili ya miradi mingine katika miji ya Lusaka na Bujumbura huku maandalizi ya miradi mingine yakiendelea Abuja, Kinshasa na Addis Ababa. Kombo amesema Serikali itaendelea kuwakaribisha wadau mbalimbali wakiwemo benki na wawekezaji binafsi kushiriki katika fursa hizo za kimkakati. “Hatua hizi zinaonyesha mkakati mpana wa Serikali wa kutumia nguvu ya diaspora, ubunifu wa kifedha na ushirikiano wa kimataifa kuharakisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa,” amesema.

Go to News Site