Collector
TPA yawataka wadau kujipanga utekelezaji tozo mpya | Collector
TPA yawataka wadau kujipanga utekelezaji tozo mpya
Mwananchi

TPA yawataka wadau kujipanga utekelezaji tozo mpya

Tanga. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imewataka wadau wa sekta ya usafirishaji na biashara kuanza kujipanga kwa utekelezaji wa Ada ya Uendelezaji wa Miundombinu Mipya ya Bandari (PID) inayotarajiwa kuanza kutumika Julai 1, 2026. Ada hiyo ni asilimia 4.5 ya kodi ya forodha ikiwa imepunguzwa kutoka asilimia 9 ya awali, ambayo ilikuwa ianze kutumika Machi 2026. Wadau walishauri ipunguzwe na TPA ikafanya hivyo na kuisimamisha hadi Jalai 1, 2026. Leo Jumapili, Mei 27, 2026, Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega amekutana na wadau wa Bandari ya Tanga kuzungumzia tozo hizo, ambazo amesema zinakwenda kufanya maboresho ya bandari. Katika kikao hicho wadau mbalimbali wameunga mkono mpango huo wakisema utasaidia kuongeza uwezo wa bandari nchini na kuboresha ushindani wa Tanzania katika biashara ya kikanda. Mbega amesema Serikali imefikia hatua ya kuanzisha tozo hiyo kutokana na ongezeko la shehena katika bandari mbalimbali nchini, jambo ambalo linahitaji uwekezaji mkubwa katika miundombinu. “Mahitaji ya huduma za bandari yanaongezeka kwa kasi kubwa, hivyo maboresho ya miundombinu ni jambo lisiloepukika kama tunataka kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi,” amesema Mbega. Amesema kwa sasa Bandari ya Tanga inahudumia takribani tani milioni mbili za mizigo kwa mwaka huku uwezo wa miundombinu iliyopo ukitarajiwa kufikia ukomo wake kabla ya mwaka 2030 kutokana na kuongezeka kwa shughuli za biashara. “Fedha zitakazokusanywa kupitia PID zitaelekezwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo ya bandari ikiwemo ujenzi wa magati mapya na kuongeza uwezo wa kuhudumia meli kubwa zaidi,” amesema Mbega. Mbega amesema mradi wa ujenzi wa gati la 12 katika Bandari ya Dar es Salaam ni miongoni mwa miradi inayotarajiwa kunufaika kupitia mapato ya tozo hiyo kutokana na umuhimu wake katika kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena nyingi zaidi kwa wakati mfupi. Kwa mujibu wa Mbega, maboresho hayo yatasaidia kupunguza ucheleweshaji wa meli bandarini ambao umekuwa ukisababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara na wananchi. “Meli inapokaa nje ya bandari hulipiwa hadi dola za Marekani 20,000 kwa siku. Hii ni gharama kubwa ambayo mwisho wake humgusa mfanyabiashara na mwananchi wa kawaida,” anesema. Aidha, amesema maboresho yaliyofanywa katika reli ya Tanga yenye thamani ya Sh429.1 bilioni yamefungua fursa mpya za usafirishaji wa mizigo kwenda Rwanda na Burundi kupitia reli hiyo ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haitumiki kikamilifu. Hata hivyo, amesema ongezeko la matumizi ya reli hiyo limeibua changamoto ya upungufu wa mabehewa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wateja wanaotaka kutumia huduma hiyo. Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TACAS), Ephraim Mwankusye amesema hatua hiyo itazifanya bandari za kisasa na zenye uwezo wa kuhudumia mizigo mingi kwa haraka zaidi na kuongeza ushindani wa Tanzania katika biashara ya kikanda. Mwankusye amesema wadau wa sekta hiyo wanaunga mkono utekelezaji wa PID kwa kuwa utaleta mageuzi makubwa katika huduma za bandari nchini. Amesema fedha zitakazopatikana kupitia mpango huo zitatumika kuboresha Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara sambamba na kuendeleza Bandari ya Bagamoyo pamoja na miundombinu ya mafuta katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa upande wake mfanyabiashara wa bidhaa za uagizaji kutoka Tanga, Asha Mwinuka amesema maboresho ya bandari yataongeza tija kwa wafanyabiashara wengi kutokana na kupungua kwa muda wa mizigo kukaa bandarini. “Kama huduma zitakuwa za haraka na meli hazitachelewa, hata gharama za biashara zitapungua kwa kiasi kikubwa. Muhimu ni kuona fedha hizi zinatumika kama ilivyopangwa,” amesema Mwinuka.

Go to News Site