Collector
Omtatah na Wamalwa wapigania ubabe katika Bunge la Kaunti ya Busia | Collector
Omtatah na Wamalwa wapigania ubabe katika Bunge la Kaunti ya Busia
LA TAIFA LEO

Omtatah na Wamalwa wapigania ubabe katika Bunge la Kaunti ya Busia

SENETA Okiya Omtatah na kiongozi wa chama cha DAP-Kenya, Eugene Wamalwa, wamejikuta katika mgogoro wa kisheria kuhusu udhibiti wa uongozi wa upande wa wachache katika Bunge la Kaunti ya Busia, huku Mahakama Kuu ikizuia kwa muda kuondolewa kwa washirika wa Omtatah katika nyadhifa muhimu. Katika kesi iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu, chama cha National Reconstruction Alliance (NRA) cha Seneta wa Busia kinadai kuwa DAP-Kenya na Spika wa Bunge la Kaunti Frederick Odillo waliunda mpango usio halali wa “kukipokonya” uongozi wa upande wa wachache. Hii inafuatia kuondolewa kwa viongozi wake katika nyadhifa mbalimbali za wachache na nafasi zao kuchukuliwa na wanachama wa DAP-Kenya. Kwa mujibu wa stakabadhi za mahakama, diwani wa NRA, Bonventure Makokha aliondolewa kama Kiongozi wa Wachache na nafasi yake kuchukuliwa na Isaac Wamalwa wa DAP-Kenya huku Paul Okello (NRA) akiondolewa kama Kiranja wa Wachache na nafasi yake kuchukuliwa na Joy Wanga( DAP-Kenya) Mabadiliko hayo pia yaliathiri Bodi ya Huduma ya Bunge la Kaunti ambapo mwakilishi wa NRA Mercy Wanyonyi aliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Kennedy Rupiah aliyeungwa mkono na DAP-Kenya. Stakabadhi za mahakama zinaonyesha kuwa Bunge hilo lina madiwani 53, ambapo muungano wa Azimio la Umoja una 44. Azimio linajumuisha ODM (MCAs 30), DAP-Kenya (7) na MDG (7). Upande wa wachache una NRA (4), UDA (2), MCCP (1), Wiper (1) na diwani mmoja huru. NRA inasema mabadiliko hayo ni batili kwa sababu DAP-Kenya bado ni sehemu ya Azimio la Umoja na hivyo haiwezi kudai uongozi wa upande wa wachache huku ikiwa bado ndani ya muungano wa wengi. Chama hicho kinadai mabadiliko hayo yaliharakishwa kwa makusudi ili kuwanyima wanachama wake nafasi muhimu za usimamizi wa bajeti na uangalizi wa serikali ya kaunti. Kesi hiyo iliwasilishwa na Katibu Mkuu wa NRA Paul Amemba Odhiambo ambaye anasisitiza kuwa chama chake ndicho kisheria kinachopaswa kushikilia nafasi ya uongozi wa wachache. Mahakama Kuu mjini Busia imesitisha kwa muda mabadiliko hayo ya uongozi na kuagiza DAP-Kenya ijibu madai yaliyowasilishwa. Mgogoro huo ulianza baada ya Katibu Mkuu wa DAP-Kenya Dkt Eseli Simiyu kumwandikia Spika Odillo Mei 19 akielekeza mabadiliko ya uongozi wa wachache. NRA inadai mabadiliko hayo yalifanywa kwa haraka bila kufuata taratibu za kikatiba na bila kushauriana na wabunge husika au Msimamizi wa Vyama vya Siasa. NRA pia inadai DAP-Kenya ilimdanganya Spika kwa kudai imejiondoa katika Azimio mwezi Februari mwaka huu, jambo ambalo inasema halijawahi kuwasilishwa rasmi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Kesi hiyo pia inahusisha barua mbalimbali kati ya NRA, DAP-Kenya, Spika na Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu mabadiliko hayo. Mahakama imeagiza pande zote kuwasilisha hoja zao kwa maandishi kabla ya kusikilizwa tena Julai 2.

Go to News Site