Collector
Ruth Odinga: Lazima tukiokoe chama cha ODM | Collector
Ruth Odinga: Lazima tukiokoe chama cha ODM
LA TAIFA LEO

Ruth Odinga: Lazima tukiokoe chama cha ODM

KWA miaka mingi, Ruth Odinga alisalia kivulini mwa kakake marehemu Raila Odinga, mwanasiasa aliyekuwa nguzo ya upinzani nchini kwa miongo kadhaa hadi alipofariki Oktoba 2025. Hata hivyo, nyuma ya pazia, Ruth amekuwa mmoja wa viongozi wa kudumu ndani ya Orange Democratic Movement tangu kuanzishwa kwake takriban miaka 20 iliyopita. Kabla ya kuingia katika siasa za uchaguzi mwaka 2013 kama Naibu Gavana wa Kisumu, alikuwa akiongoza kampuni ya Spectre International, inayomilikiwa na familia ya Odinga. Sasa akiwa Naibu Katibu wa Uhamasishaji wa ODM, Ruth amejikuta katikati ya mzozo unaotikisa chama hicho kufuatia kifo cha Raila. Katika mahojiano na Taifa Jumapili, alisema kinachomsumbua zaidi si mashambulizi ya kisiasa anayopokea kutoka kwa Waziri wa Fedha John Mbadi, bali hatari ya ODM kusambaratika kutokana na migawanyiko ya ndani. Kwa mujibu wake, msimamo wake umekuwa mmoja tu: chama lazima kibaki kimeungana. “Nilichosema katika mkutano wa Mombasa ni kwamba ODM inapaswa kubaki imara na yenye umoja ili iweze kusimamisha mgombea wake wa urais au kujadiliana kutoka nafasi ya nguvu katika miungano ya baadaye ya kisiasa. Huo ndio ulikuwa mtazamo wa Raila,” alisema. Ruth alisema alishangazwa na shutuma alizorushiwa baada ya kutoa wito wa umoja, akidai baadhi ya viongozi wanaonekana kutafsiri kauli hiyo kama kuunga mkono upande fulani. Alisema mashambulizi ya Mbadi dhidi yake na dhidi ya binti ya Raila, Winnie Odinga, hayakuwa ya lazima. “ODM daima imekuwa chama kinachowapa vijana nafasi ya kujieleza. Winnie alizungumza yale ambayo vijana wengi wanahisi kuhusu uongozi na mustakabali wa chama,” alisema. Ruth alisema alitarajia Mbadi, ambaye mara nyingi husema Raila alimlea kisiasa, angeonyesha uvumilivu na kumwelekeza Winnie badala ya kupuuza maoni yake. Akizungumzia mivutano ndani ya ODM, alisema kuna wakati mtu hujiuliza kama kuna maslahi mengine yanayochochea migawanyiko hiyo. Kwa sasa chama kimegawanyika katika makundi mawili makuu; kundi linalohusishwa na kiongozi wa chama Oburu Oginga ambalo hapo awali lilijulikana kama “Linda Ground”, na lile la Katibu Mkuu Edwin Sifuna linalojulikana kama “Linda Mwananchi”. “Kauli mbiu yetu inapaswa kubaki Chungwa Moja, Maisha Bora. ODM ilifanikiwa kwa sababu iliunganisha watu wa makabila, vizazi na mitazamo tofauti chini ya mwavuli mmoja,” alisema. Kuhusu jina la Odinga katika siasa, Ruth alisema wengi hudhani limekuwa chanzo cha manufaa, lakini husahau gharama kubwa ambayo familia hiyo imelipa. Alikumbuka jinsi familia yao ilivyokumbwa na mateso ya kisiasa kutokana na shughuli za baba yao, Jaramogi Oginga Odinga, aliyekuwa mmoja wa viongozi wakuu wa mapambano ya demokrasia nchini. Baada ya jaribio la mapinduzi ya mwaka 1982, alisema alilazimika kuishi uhamishoni katika Uganda, Tanzania na Zimbabwe kabla ya kwenda kusoma nchini Norway. “Maisha hayo yalinifundisha uvumilivu na kuimarisha imani yangu katika demokrasia na haki,” alisema. Ruth pia alikataa madai kwamba ODM imekuwa chama kinachozunguka mtu mmoja badala ya taasisi. Alisema historia ya chama hicho ilijengwa kupitia ushiriki wa wananchi wa kawaida tangu enzi za FORD, NDP, NARC hadi kuzaliwa kwa ODM. “ODM ni kubwa kuliko mtu yeyote mmoja. Nguvu zake zimekuwa katika kujumuisha kila mtu na kusikiliza maoni tofauti,” alisema. Kuhusu uchaguzi mkuu ujao, alisema chama kinapaswa kushauriana kwa upana kabla ya kuamua kama kitasimamisha mgombea wake wa urais au kuunga mkono mpangilio mwingine wa kisiasa. Lakini jambo analosisitiza zaidi ni maridhiano kati ya makundi yanayopingana. “Ninaamini kabisa maridhiano yanawezekana. Nimeona migogoro mikubwa zaidi ikitatuliwa kupitia mazungumzo,” alisema, akirejelea ushiriki wake katika juhudi za kidiplomasia baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007. Kwa maoni yake, migogoro ya sasa ndani ya ODM ni midogo ikilinganishwa na changamoto ambazo chama na nchi zimewahi kupitia hapo awali. Alitoa wito kwa viongozi wa chama kuwapa nafasi vijana kama Sifuna, Babu Owino na Winnie Odinga, akisema wao ni sehemu muhimu ya kizazi kitakachobeba chama siku zijazo. Akizungumzia maisha baada ya kifo cha Raila, Ruth alisema bado hajapona kutokana na majonzi ya kumpoteza kaka yake pamoja na dada yao Beryl Achieng ndani ya kipindi kifupi. “Raila alifanyia Kenya mengi. Mchango wake kwa demokrasia na haki haupaswi kusahaulika. Bado sijakubali kikamilifu hasara hiyo,” alisema. Kwa sasa, anasema lengo lake kuu ni kuona ODM ikinusurika kipindi hiki kigumu cha mpito. “ODM lazima iokolewe. Tofauti za maoni zipo katika siasa, lakini chama makini hutatua migogoro yake kupitia mazungumzo, si kupitia vita hadharani,” alisema.

Go to News Site