Collector
Barabara telezi kwa Orengo anaposaka ufalme wa Waluo | Collector
Barabara telezi kwa Orengo anaposaka ufalme wa Waluo
LA TAIFA LEO

Barabara telezi kwa Orengo anaposaka ufalme wa Waluo

BAADHI ya wafuasi wake humuita Nyawawa (roho ya waliokufa), wengine humuita Nyatieng (jiwe linaloweza kuua) na kwa wengine yeye ni Wuod Nyamayanga (mwana wa kiume wa Nyamayanga). Licha ya majina hayo yenye sifa za ushujaa, Gavana wa Siaya James Orengo anakabiliwa na wakati mgumu katika taaluma yake ya kisiasa. Orengo, 75, ni kati ya wanasiasa ambao wamehudumu kwa kipindi kirefu zaidi katika nafasi za uongozi kutoka eneo la Nyanza. Aliingia bungeni 1979 akiwa na umri wa miaka 28. Hii leo jamii ya Waluo itakapokutana uwanjani Kirembe eneobunge la Kisumu Mashariki ili kutangaza mwelekeo wake wa kisiasa 2027, Orengo hatakuwepo. Gavana huyo kwa sasa yupo katika mvutano wa ubabe wa kisiasa na kinara wa ODM, Dkt Oburu Oginga. Aidha, Orengo amekemewa kutokana na matamshi ya kumdhalilisha Gavana wa Homa Gladys Wanga aliyoyatoa majuzi. Pia kuna uhasama kati yake na Naibu Gavana William Oduol pamoja na Bunge la Kaunti ya Siaya. Vile vile, anapambania ubabe kwenye mrengo wa Linda Mwananchi na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Hivi majuzi tu Orengo alilalamika kuwa maafisa wa ulinzi walikuwa wameondolewa kwenye makazi yake Nairobi, akihusisha tukio hilo na msimamo wake wa kisiasa. Mnamo Ijumaa mikutano yake ya kusaka uungwaji mkono Mbita, Kaunti ya Homa Bay, iligubikwa na ghasia huku magari yake yakishambuliwa na mlinzi wake kujeruhiwa vibaya. Katika Kaunti ya Siaya, Gavana Orengo hapumui kwa sababu mchakato wa kumtimua upo njiani. Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali, Diwani Washington Booker ‘Dasani’ wa Uyoma Kaskazini alifichua kuwa anapanga kuwasilisha hoja ya kumtimua gavana huyo. “Nina hoja tosha ya kumtimua gavana, moja ikiwa kukosa kutekeleza miradi ilhali tuna bajeti kwa mwaka mzima wa fedha. Pia alitimua vibarua waliokuwa wamefanya kazi kwa mwaka mzima ilhali anasema hawajui,” akaeleza Booker. “Hazina ya fedha ya Siaya sasa inasimamiwa na mtu ambaye alikataliwa na Bunge la Kaunti. Nasaka saini 30, na jinsi mambo yalivyo hatima ya Bwana Orengo itakuwa mikononi mwa Bunge la Kaunti,” akaongeza. Hivi majuzi Orengo alijipata pabaya na shinikizo zinaendelea kumwandama kutokana na matamshi aliyoyatoa dhidi ya gavana mwenzake Wanga wakati akihutubia umma katika kituo cha mabasi mjini Homa Bay. “Orengo…wanawake kwenye siasa na uongozi wametoka mbali wala hatutarudi nyuma. Matusi na maneno ya kudhalilisha Gavana Wanga hayana nafasi katika siasa zetu,” akasema Mbunge wa Kisumu Mjini Magharibi, Rosa Buyu. Bado kwenye kaunti Orengo hapatani na naibu wake Oduol wawili hao wakikosana miezi michache tu baada ya kuingia mamlakani 2022, na sasa uhasama wao unatokota. Marehemu kinara wa ODM, Raila Odinga, ndiye aliwapatanisha kuelekea mchujo wa chama 2022 na wakawania kwa tikiti moja. Mnamo Mei 29, 2023, uhasama wao ulifikia kilele wakati Oduol alitimuliwa na madiwani ila akanusuriwa na Seneti mnamo Juni 26, 2023. Tangu wakati huo Oduol, ambaye anamezea mate ugavana, haonani uso kwa macho na bosi wake Orengo. Naibu gavana huyo pia amekuwa akitengwa kwenye shughuli za usimamizi wa kaunti. Oduol kwa sasa yuko mrengo wa Linda Ground ambao haupatani na ule wa Linda Mwananchi unaoshabikiwa na Orengo. Licha ya kutangaza kuwa atakuwa akiwania urais 2027 Gavana Orengo hajapata uungwaji mkono kutoka hata kwa mbunge mmoja wa eneo la Luo Nyanza. “Amejitenga na usimamizi wa kaunti na sasa anataka kuvuruga jamii ya Waluo. Anataka watu warejelee maandamano baada ya kifo cha Raila, lakini hatutakubali hilo,” akasema Mbunge wa Alego Usonga Samuel Atandi ‘Meli’. Hata hivyo, Orengo mwenyewe anasisitiza kuwa hatatishwa, na kwamba mkondo wa kisiasa ambao amechukua ndio utafaa Waluo. “Siasa zangu kila mtu anajua, na mara kwa mara nimekuwa upande wa wananchi. Wafanye kile wanataka lakini sitatetereka,” akasema Orengo. Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Profesa Lumala Masibo, gavana huyo wa Siaya anataka kuwa kigogo wa kisiasa za Luo Nyanza baada ya mauti ya Raila. “Hata huo urais hamakinikii, lengo lake anataka kuchukua chama kutoka kwa Oburu ili awe kigogo wa siasa wa Luo Nyanza. Kumbuka alijaribu kufanya hivyo Raila alipokuwa hai lakini hakufaulu,” aeleza Prof Masibo.

Go to News Site