LA TAIFA LEO
SERIKALI ya Kenya inaendelea na mipango ya kuanzisha kituo cha kutenga na kutibu Ebola kwa ushirikiano na serikali ya Amerika, huku ikipuuza amri ya korti katika mfano halisi wa ukaidi. Uamuzi wa kulazimisha mradi huo unaozingirwa na utata vilevile unaenda kinyume na pingamizi za umma, ikiwemo kutoka kwa wataalamu wa matibabu nchini, ambao wamezua maswali kuhusu uwezo wa mfumo wa afya nchini kukabiliana na virusi hivyo hatari. Huku kukiwa na mawasiliano finyu kutoka kwa serikali kuhusu kituo hicho, CNN, kituo cha kimataifa cha habari Amerika, kimeripoti kuwa raia wa Amerika wataendesha kituo hicho kilichoanzishwa tayari katika Ngome ya Jeshi la Angani Kaunti ya Laikipia, Jumamosi. Kituo hicho cha habari kilinukuu duru za serikali ya Amerika, iliyothibitisha mpango huo. Imekuwa kawaida kwa serikali ya Kenya kupuuza amri za korti hasa zinazohusu miradi yake mikuu. Haya yamejiri siku moja tu baada ya taasisi ya Katiba kuandikia Wizara ya Masuala ya Kigeni Amerika kufahamisha taifa hilo kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu ya Kenya kusimamisha kuanzishwa kwa kituo hicho cha Ebola. “Tunaandika kufahamisha rasmi Wizara za Masuala ya Kigeni na ya Afya ya Amerika kuhusu maagizo ya muda yaliyotolewa na Mahakama Kuu ya Kenya mnamo Mei 28, 2026. Maagizo haya yanasitisha mara moja pendekezo la kuanzisha kituo chochote kinachoungwa mkono na Amerika cha kuzuilia, kutenga au kutibu Ebola ndani ya mipaka ya Kenya,” ilisema Katiba Institute. Katika barua hiyo iliyotiwa saini na Mkurugenzi Nora Mbagathi, taasisi hiyo ilisema amri ya korti inapiga marufuku kulaza, kuhamisha au kupokea watu wowote waliotagusana au kuambukizwa virusi hivyo. “Tunatarajia Amerika iheshimu hadhi ya mfumo wa sheria wa Kenya.” Kituo hicho kinanuiwa kuwatenga na kuwatibu raia wa Amerika watakaotagusana au kuambukizwa virusi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Visa zaidi ya 1,000 vya Ebola vimeripotiwa nchini DRC, huku watu wasiopungua 246 wakiaga dunia kutokana na virusi hivyo hatari. Uganda, inayopakana na Kenya imeripoti visa tisa na kifo kimoja kufikia sasa. Kwa kupanga kuanzisha kituo hicho, serikali ya Amerika inakusudia kuwaweka raia wake kutibiwa karibu na eneo la mkurupuko badala ya kuwasafirisha kurejea nyumbani kwao, hali inayozua uwezekano wa kusambaza na kuhatarisha raia wake zaidi kutokana na virusi hivyo. Hata hivyo, ni tishio lilo hilo na kuhatarishwa ambako kumezua pingamizi ya kuwa na kituo hicho Kenya. Kenya haijarekodi kisa hata kimoja, lakini sasa inakodolea macho tishio la maambukizi kupitia mipaka yake na Uganda na kituo hicho kilichopendekezwa. Kinara wa DCP Rigathi Gachagua jana aliitaka Amerika kuheshimu sheria kwa kusimamisha kituo hicho. Bw Gachagua alidai anafahamu licha ya amri ya korti vifaa vinapelekwa Nanyuki. Alisema baadhi ya wanajeshi wamewasiliana naye na kumrai alalamike kwa niaba yao. Alidai maafisa wa jeshi wameelezea hofu wasiwasi kuhusu uwezekano wa maambukizi kwa familia zao zinazoishi kwenye kambi ya jeshi. “Wanajeshi hawajafurahi kamwe lakini hawana sauti. Watu wa Laikipia wametuomba tushiriki mkutano Nanyuki kuwapa fursa ya kujieleza ili serikali ya Amerika ijue kile inachohisi Laikipia,” alisema Bw Gachagua. Kenya ilifungua milango yake ya kuanzisha vituo vya utafiti na kutengea maradhi yaliyoorodheshwa kama tishio kibiolojia mnamo Julai 24, 2015, ilipotia saini mkataba wa ushirikiano na Amerika. Mkataba huo ulipatia Amerika udhibiti kuhusu miradi itakayoibuka ikiwemo kuteua wanakandarasi na kuondolea ushuru bidhaa zinazoagiziwa ng’ambo kwa wafanyakazi wa Amerika. Mkataba huo vilevile ulizuia nchi hizo mbili kuwasilisha kesi dhidi ya mwenzake iwapo vifo, majeraha au uharibifu utatokana na miradi chini ya mkataba huo.
Go to News Site