Collector
Wetangúla asema ataridhiana na mahasimu wake Magharibi ili kurindima Tutam | Collector
Wetangúla asema ataridhiana na mahasimu wake Magharibi ili kurindima Tutam
LA TAIFA LEO

Wetangúla asema ataridhiana na mahasimu wake Magharibi ili kurindima Tutam

SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetangúla amesema kuwa yupo tayari kuridhiana na mahasimu wake kisiasa Magharibi mwa Kenya, ili kura za eneo hilo zielekezwe katika kapu moja mnamo 2027. Bw Wetang’ula alisema siasa za kurushiana cheche, kuitana majina na uhasama zimeendelea kuligawa eneo hilo, akiongeza kuwa wakati umefika kwa viongozi kuzungumza kwa sauti moja ndipo katika meza ya mazungumzo, matakwa yao yachukuliwe kwa uzito. “Wale wote ambao wamesema mambo mabaya kunihusu katika siasa na hawakujua walichokuwa wakisema, nimewasamehe,” akasema Bw Wetang’ula wakati wa mazishi ya Mzee Patrick Wangamati katika eneobunge la Kabuchai, Kaunti ya Bungoma, wikendi Marehemu aliyewahi kuhudumu kama mbunge maalum na mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Waluhya alikuwa baba wa aliyekuwa Gavana wa Bungoma, Wycliffe Wangamati. Bw Wetang’ula alihimiza umoja na kuunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais William Ruto, akisema Kaunti ya Bungoma imenufaika pakubwa chini ya serikali ya Kenya Kwanza. “Sisi ndiyo kaunti pekee yenye vyuo vitatu vya kitaifa vya ufundi ambavyo ni Sang’alo, Kisiwa na Matili. Tutajenga hospitali ya Level 6 huko Sichei yenye thamani ya Sh8 bilioni,” “Baada ya hospitali hiyo kujengwa, tumemwambia Rais kwamba barabara ya mzunguko wa Chebukaka-Khachonge-Makoto itawekewa lami ili kuihudumia,” akaongeza Bw Wetang’ula. Ndoto ya muda mrefu ya umoja wa Waluhya ilidhihirika kuwa bado ni changamoto wakati wa mazishi hayo baada ya viongozi wa upinzani kuondoka mara walipopata habari kuwa kiongozi huyo wa Ford Kenya alikuwa amewasili. Spika huyo aliwasili akiwa ameandamana na Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka, Seneta Wafula Wakoli na aliyekuwa Mbunge wa Bumula Mwambu Mabonga. Viongozi hao walizungumza na waombolezaji baada ya ibada, huku Bw Wetang’ula akisema yuko tayari kuridhiana na aliyekuwa Gavana Wycliffe Wangamati ambaye kwa muda sasa amekuwa mpinzani wake wa kisiasa. Hata mfawidhi wa sherehe na Mbunge wa eneo hilo, Majimbo Kalasinga, ambaye ana uhasama wa kisiasa na Bw Wetang’ula, aliondoka kabla ya kuwasili kwake na hakumpokea. “Kwa ndugu yangu Wycliffe, siasa ni siasa na haifai kuwa na uhasama wa kibinafsi. Hujui utakuwa nini kesho lakini afadhali mimi najua nitakuwa nani kesho,” akasema Bw Wetangúla. Spika huyo alisisitiza kuwa hatajihusisha na siasa za makabiliano na kufichua kuwa hivi karibuni ataandaa mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Posta ili kutoa mwelekeo wa kisiasa. Kabla ya kuwasili kwa Bw Wetang’ula na ujumbe wake, viongozi wa upinzani waliokwepo walikosoa serikali na kumshambulia pamoja na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi. Viongozi hao wa upinzani waliongozwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, kiongozi wa chama cha DAP-Kenya Eugene Wamalwa, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna pamoja na wanasiasa wengine wanaohusishwa na vuguvugu la Linda Mwananchi na Muungano wa Upinzani. Uhasama kati ya Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa na Bw Sifuna pia ulijitokeza wakati wa mazishi hayo, ambapo Bw Barasa, ambaye anawania ugavana wa Bungoma, aliondoka muda mfupi baada ya kuhutubu pamoja na umati mkubwa wa waombolezaji.

Go to News Site