Collector
Hofu visa vya wizi wa pikipiki vikiendelea kuongezeka mpakani | Collector
Hofu visa vya wizi wa pikipiki vikiendelea kuongezeka mpakani
LA TAIFA LEO

Hofu visa vya wizi wa pikipiki vikiendelea kuongezeka mpakani

PIKIPIKI nane zilizoibwa jana zilinaswa katika vituo vya mpakani vya Namanga na Loitoktok kuelekea Tanzania huku visa vya wizi wa pikipiki kisha kuvukishwa mpakani vikiendelea kuongezeka. Vyombo vya usalama vimewataka waendesha pikipiki kuwa waangalifu na kuripoti visa vya wizi wa pikipiki mara moja ili kusaidia kuvunja mitandao ya wahalifu ambayo imeenea katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Wito huo ulitolewa wakati wa mkutano wa uhamasishaji kuhusu usalama uliofanyika mjini Kitengela mwishoni mwa wiki, ulioandaliwa na kampuni ya ufadhili wa pikipiki ya Mogo kwa ushirikiano na Chama cha Usalama wa Waendesha Pikipiki Kenya (BAK). Mkutano huo uliwaleta pamoja waendesha pikipiki, wafadhili na vyombo vya usalama kujadili tishio linaloongezeka la wizi wa pikipiki mpakani na kutafuta mbinu za kukabiliana na tatizo hilo. Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kajiado, Alex Shikondi, alisema vizuizi viwili vya polisi vilivyowekwa katika maeneo ya mpakani ndani ya kaunti hiyo vimechangia kunaswa kwa pikipiki nane zilizoibwa. Kati ya pikipiki zilizonaswa mbili zinatoka Kaunti ya Kajiado na sita kutoka Nairobi. Waliokuwa na pikipiki hizo walitoroka baada ya kusimamishwa katika vizuizi hivyo usiku. "Vyombo vya usalama vimetambua kuwa pikipiki zilizoibwa husafirishwa kwa siri hadi Tanzania ambako huvunjwavunjwa vipande. Katika miezi minne iliyopita sisi polisi tumenasa pikipiki nane zilizoibwa zikielekea katika vituo viwili vya mpakani vya Kajiado," alisema Bw Shikondi huku akiwataka waendesha pikipiki kuwa waangalifu. "Waendesha pikipiki wabuni alama ya siri na kuiweka kwenye pikipiki zao ili iwe rahisi kwa vyombo vya usalama kuzifuatilia zinapoibwa," Kutokana na ukaribu wake na Tanzania pamoja na uwepo wa vituo viwili vya mpakani vya Namanga na Tarakea, Kajiado imekuwa mojawapo ya maeneo yanayolengwa zaidi na mitandao ya wizi wa pikipiki. Mwenyekiti wa Kitaifa wa BAK, Kevin Mubadi, alisema wizi wa pikipiki na kupitishwa mpakani umekuwa moja ya changamoto kubwa zinazoikabili sekta hiyo, hasa katika maeneo ya mpakani ambapo mianya ya utekelezaji wa sheria hutumiwa na wahalifu. Alisema shirika hilo linafanya kazi kwa karibu na mashirika ya usalama ili kulinda sekta hiyo.

Go to News Site