LA TAIFA LEO
RAIS William Ruto ameendelea kunyamaza kuhusu mipango ya kuanzisha kituo cha kuwatenga wagonjwa wa Ebola na vituo vya maabara katika Ngome ya Jeshi la Anga, Nanyuki, licha ya malalamishi kutoka kwa wakazi wa Laikipia na amri ya korti inayozuia mpango huo kati ya Kenya-Amerika unaozingirwa na utata. Katika hotuba yake kwenye maadhimisho ya miaka 63 ya Sikukuu ya Madaraka, Kaunti ya Wajir, Rais Ruto alijiepusha kabisa na utata unaohusu vituo vya Ebola, saa chache baada ya vyombo vya habari Amerika kuripoti kuwa wataalamu kutoka Amerika tayari wametua Laikipia. Taifa Leo imebaini kwamba serikali inasonga mbele na mipango ya kuanzisha kituo hicho na kwamba raia wa Amerika waliopangiwa kuendesha kituo hicho waliwasili katika Ngome ya Jeshi la Anga Laikipia, Jumamosi na wengine zaidi wanatarajiwa kuwasili wiki hii. Kitengo cha habari cha Rais Ruto hakikujibu maswali kuhusu kimya chake kwa suala tata la kituo cha wagonjwa wa Ebola wanaotoka Amerika kutengwa Laikipia. Mahakama leo hii itasikiza kesi iliyowasilishwa na Taasisi ya Katiba Institute inayodhamiria kuzuia Amerika kutuma au Kenya kupokea wagonjwa wa Ebola kutoka taifa hilo lenye uchumi mkubwa duniani. Wiki iliyopita, korti ilitoa maagizo ya muda kuzuia Amerika na Kenya kuendelea na utekelezaji wa mkataba unaohusu kuanzisha kituo cha kutengea na vituo vya maabara kwa maandalizi ya kupokea wagonjwa kutoka Amerika. Akijibu kuhusu amri ya korti, Waziri wa Afya Aden Duale alisema serikali inashirikiana. “Sasa kwa sababu tuna amri ya korti, mahakama imetupatia saa 48 kuwasilisha kesi yetu. Mwanasheria mkuu, mshauri kuhusu sheria, tayari amewasilisha,” akasema. Jana, wakili Malidzo Nyawa wa Katiba Institute alisema shirika hilo linasubiri kusoma matini ya jibu la serikali kortini kabla ya kuchukua hatua zaidi. Alhamisi iliyopita, huku ghadhabu ikitanda kuhusu mradi huo wa Kenya-Amerika, Rais Ruto aliwasiliana kwa simu na Waziri wa Masuala ya Kigeni Amerika, Marco Rubio ambapo walijadili kuhusu mkurupuko wa Ebola na juhudi za mipangilio. Bw Rubio alitangaza Sh1.7 bilioni za kufadhili mradhi huo kwenye mawasiliano hayo. Habari kuhusu ujenzi wa vituo vya kutengea na maabara zilithibitishwa kwa mara ya kwanza wiki iliyopita wakati gazeti kuu Amerika, la New York Times , liliripoti kwamba Amerika itasafirisha mtu yeyote anayegunduliwa kuwa na Ebola nchini Kenya. Mkataba huo wa Amerika-Kenya umezua hamaki huku madaktari, mawakili, watetezi wa haki za kibinadamu na wakazi wakipinga vikali kuwapa makao raia wa kigeni walioambukizwa virusi vya Ebola. Rais wa LSK Charles Kanjama alisema Ijumaa kuwa “Kenya haiwezi kuwa nyanja ya kuhifadhi magonjwa ya maambukizi kutoka nchi za kigeni zinazolenga kulinda maeneo yao binafsi kutokana na tishio.” Bw Kanjama alisema LSK imewasilisha kesi katika Mahakama Kuu ikinuia kukomesha mkataba wa Amerika-Kenya. Viongozi waliochaguliwa Kaunti ya Laikipia waliokaribisha uamuzi wa mahakama kuu, waliuliza katika taarifa ya pamoja kabla ya uamuzi huo: “Mbona Laikipia? Ni nini serikali ya Amerika inafahamu kuhusu hili hivi kwamba hawakubali raia wao wenyewe walioathirika kwenye ardhi yao lakini wako tayari kuwahamisha kwingineko?” Muungano wa Madaktari Nchini Alhamisi iliyopita ulitishia kugoma ikiwa serikali haitazungumzia kuhusu ukosefu wa uwazi, tishio la mlipuko na kuwatenga wahudumu wa afya Wakenya katika mradi wa Laikipia. Kupitia taarifa Jumamosi, serikali ya Trump ilikiri kuhusu hatua ya korti na kusema inashirikisha mamlaka ya Kenya kuangazia masuala yaliyoibuka kuhusu mradi huo. Wakazi wa Nanyuki jana walimiminika barabarani, kulalamikia ujenzi wa vituo vya Ebola mjini humo. Ijumaa, Katibu wa Wizara ya Afya, Ouma Oluga alisema akikiri ukweli wa ripoti hizo kwamba wizara ipo tayari kukabiliana na mlipuko wa Ebola. Waziri Duale Jumamosi alikana kuwa kituo cha Laikipia ni mahsusi kwa kuwatengea raia wa Amerika wanaougua virusi vya Ebola. Mkurugenzi wa shirika la Resilience Action Network Africa, Aggrey Aluso, alisema licha ya Kenya kukubali kuwapa makao raia wa Amerika wanaougua Ebola, mikakati ya Kenya kukabili mlipuko wa Bundibugyo Ebola, aina ya virusi vinavyosambaratisha DRC Mashariki na Uganda, haina uwezo wa kukabili tishio hilo.
Go to News Site