Collector
El Niño hatari zaidi yaja, UN yaonya ikisema itaanza kwa kiangazi kirefu, halafu mafuriko | Collector
El Niño hatari zaidi yaja, UN yaonya ikisema itaanza kwa kiangazi kirefu, halafu mafuriko
LA TAIFA LEO

El Niño hatari zaidi yaja, UN yaonya ikisema itaanza kwa kiangazi kirefu, halafu mafuriko

WENGI wanakumbuka uharibifu uliosababishwa na janga la El Niño mwaka 2023 na 2024. Takwimu zinaonyesha kuwa watu wasiopungua 245 walifariki, zaidi ya familia 78,000 ziliathirika na karibu familia 46,000 zilihamishwa kutoka makazi yao. Kaunti 42 kati ya 47 nchini zilipata athari za janga hilo. Sasa, wataalamu wa hali ya hewa wanaonya huenda nchi ikakabiliwa tena na El Niño. Jumanne, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) lilitangaza kuwa kuna uwezekano wa asilimia 90 kwamba El Niño itajitokeza katika nusu ya pili ya mwaka huu. Katibu Mkuu wa shirika hilo, Celeste Saulo, alisema dunia inapaswa kujiandaa kwa El Niño yenye nguvu ambayo inaweza kuongeza ukame, mvua kubwa na mawimbi ya joto. Kwa mujibu wa shirika hilo, El Niño ya mwaka 2023-2024 ilikuwa miongoni mwa tano zenye nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa duniani na ilichangia viwango vya juu vya joto vilivyoshuhudiwa mwaka 2024. Hata hivyo, kwa Kenya, El Niño haimaanishi mafuriko pekee. Wataalamu wanaeleza kuwa hali hiyo huathiri nchi katika awamu mbili tofauti. Katika miezi ya Juni, Julai na Agosti, Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya inatarajia mvua za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya nchi. Maeneo ya Magharibi mwa Kenya, Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria na Kaskazini Magharibi yanatarajiwa kupata vipindi vya ukame na mvua chache. Wakati huo huo, joto la juu kuliko kawaida linatarajiwa kushuhudiwa kote nchini. Hali hiyo inaweza kuathiri uzalishaji wa mazao hasa katika maeneo ya kilimo ambayo tayari yanakabiliwa na upungufu wa unyevu ardhini. Wakulima pia wameonywa kuhusu upepo mkali unaoweza kuharibu mazao na kuongeza kiwango cha kukauka kwa maji mashambani. Kaunti za Pwani za Mombasa, Kilifi, Kwale na Lamu ndizo zinazotarajiwa kupata nafuu kiasi, zikiwa na uwezekano wa kupokea mvua za wastani hadi nyingi zaidi kuliko kawaida. Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa kipindi muhimu zaidi kitakuwa kati ya Oktoba na Desemba. Kihistoria, El Niño imehusishwa na ongezeko kubwa la mvua nchini Kenya. Mwanasayansi wa hali ya hewa katika Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya, Dkt Chris Kiptum, amesema mvua nyingi inatarajiwa mwishoni mwa mwaka na inaweza kusababisha mafuriko katika maeneo ya mijini yenye maboma mabovu, maeneo ya mabondeni na maeneo yaliyo karibu na mito. Athari za El Niño mwaka huu pia zitategemea hali ya bahari ya Hindi kupitia mfumo unaojulikana kama Indian Ocean Dipole (IOD). Mfumo huu huathiri kiwango cha mvua kinachopatikana katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Wataalamu wanasema ikiwa El Niño itaambatana na IOD chanya, mvua zinaweza kuwa nyingi zaidi na kuongeza hatari ya mafuriko kama yale yaliyoshuhudiwa mwaka 2024. Miaka ya hivi karibuni imeonyesha kuwa Kenya bado inakabiliwa na changamoto zilezile kila El Niño inapojitokeza. Mabomba mabovu ya maji mijini, makazi katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko, pamoja na utekelezaji hafifu wa onyo ya mapema, zimeendelea kuongeza madhara ya majanga hayo. Wataalamu wa hali ya hewa wanasema El Niño si lazima iwe janga ikiwa maandalizi yatafanywa mapema. Serikali za kaunti, wakulima na wananchi wanahimizwa kutumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kupanga shughuli zao mapema ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza. Kwa sasa, ujumbe kutoka kwa wataalamu ni wazi: miezi michache ijayo inaweza kuanza kwa ukame na joto kali, lakini mwishoni mwa mwaka Kenya huenda ikakabiliwa tena na mafuriko makubwa. Wakati wa kujiandaa ni sasa, kabla ya maafa kurejea.

Go to News Site