Collector
Kaunti hatarini seneti, wabunge wakivutana kuhusu kiwango cha mgao | Collector
Kaunti hatarini seneti, wabunge wakivutana kuhusu kiwango cha mgao
LA TAIFA LEO

Kaunti hatarini seneti, wabunge wakivutana kuhusu kiwango cha mgao

Wabunge na Maseneta wanavutana tena kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato wa mwaka 2026, baada ya kikao cha kwanza cha kamati ya upatanishi kushindwa kufikia makubaliano kuhusu kiasi cha fedha kinachopaswa kutengewa serikali za kaunti. Kamati hiyo maalum, iliyo na wawakilishi sawa kutoka Bunge la Kitaifa na Seneti, ilikutana kwa mara ya kwanza kujaribu kumaliza tofauti zilizopo kati ya pande hizo mbili. Hata hivyo, baada ya mjadala uliochukua takriban saa moja, hakukuwa na “moshi mweupe” wa makubaliano, ishara kwamba tofauti bado ni kubwa. Mswada wa Ugavi wa Mapato huweka hugawanya mapato ya kitaifa kati ya serikali kuu na serikali za kaunti. Bunge la Kitaifa lilipitisha mswada huo Machi 12, 2026 na kuuwasilisha Seneti. Hata hivyo, Seneti ilipendekeza marekebisho na hivyo kusababisha kuundwa kwa kamati ya upatanishi ili kupata makubaliano ya pamoja. Kwa mujibu wa mapendekezo yaliyo mezani, Bunge la Kitaifa linataka kaunti zipokee Sh420 bilioni, huku Seneti ikisisitiza kiwango cha Sh454.7 bilioni. Tofauti hiyo ya takriban Sh34 bilioni ndiyo kiini cha mvutano unaoendelea. Akizungumza baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Ugavi ya Bunge la Kitaifa ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa kamati ya upatanishi, Samuel Atandi, alisema hali ya kifedha nchini kwa sasa ni ngumu kutokana na mapato ya serikali kutofikia malengo yaliyonuia kukusanywa. Atandi alisema kuna pengo katika bajeti la takriban Sh200 bilioni, jambo ambalo linafanya serikali kuu kushindwa kuongeza mgao kwa kiwango kinachotakiwa na Seneti. Aliongeza kuwa pande zote hapo awali zilikuwa zimeafikiana kwa kanuni kuhusu Sh450 bilioni, lakini hali ya kiuchumi imebadilika. Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse, alisema kuwa ingawa wabunge wa Bunge la Kitaifa wanaunga mkono ugatuzi na ongezeko la fedha kwa kaunti, serikali lazima iwe kweli kuhusu uwezo wake wa kifedha. Kwa upande wake, Mbunge wa Endebes, Robert Pukose, alisema kuwa serikali tayari imeelekeza rasilimali nyingi katika kaunti kupitia sekta ya afya ya msingi na mipango mingine ya kitaifa, ambayo inapaswa kuzingatiwa wakati wa maamuzi ya bajeti. Mbunge wa Kitutu Chache, Japheth Nyakundi, alisisitiza umuhimu wa kupatikana kwa suluhisho la kudumu linalozingatia uhalisia wa kiuchumi nchini, akisema kuwa ugavi wa fedha lazima uwe endelevu na usiibue mgogoro wa kifedha kwa serikali kuu. Kwa upande wa Seneti, wabunge hao wameendelea kusisitiza kuwa kaunti zinahitaji fedha zaidi ili kuweza kutekeleza majukumu yao kikamilifu, kulipa madeni yaliyolimbikiza na kuboresha huduma kwa wananchi. Ali Roba alisema mapendekezo ya Seneti yanategemea takwimu na mashauriano ya kina, ikiwemo mahitaji ya miradi ya maendeleo kama vile viwanda vya kaunti, mipango ya mabadiliko ya tabianchi na miradi ya kilimo. Seneta wa Narok, Ledama Olekina, alisema hali katika kaunti ni mbaya kutokana na deni kubwa na ucheleweshaji wa malipo, akionya kuwa huduma kwa wananchi zimeathirika pakubwa. Kwa mujibu wa maseneta, kaunti zinapaswa kupewa fedha za kutosha ili kutimiza wajibu wa kikatiba wa ugatuzi na kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa ufanisi. Kamati hiyo imepanga kukutana tena Jumatatu katika jaribio la mwisho la kupata muafaka. Hata hivyo, iwapo makubaliano hayatapatikana kwa haraka, kuna hofu kwamba ucheleweshaji huo unaweza kuathiri ugavi wa fedha kwa kaunti katika mwaka mpya wa kifedha, jambo ambalo linaweza kuvuruga huduma muhimu kote nchini.

Go to News Site