LA TAIFA LEO
Tangu aondoke mamlakani mwaka 2022, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ameibuka kama mmoja wa viongozi wa Afrika wanaopewa jukumu kubwa la kuimarisha demokrasia, kusuluhisha migogoro na kuongoza uangalizi wa uchaguzi katika mataifa mbalimbali ya bara hili. Tofauti na viongozi wengi wa zamani ambao hujiondoa katika shughuli za umma baada ya kuondoka madarakani, Bw Kenyatta amekuwa akionekana mara kwa mara katika majukwaa ya kimataifa akiwakilisha taasisi za Afrika katika masuala ya uchaguzi, amani na utawala bora .Juma hili, alitua mjini Addis Ababa, Ethiopia, kuongoza Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Muungano wa Afrika (AUEOM) katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo. Uchaguzi huo unachukuliwa kuwa miongoni mwa matukio muhimu zaidi ya kisiasa barani kutokana na nafasi ya Ethiopia kama makao makuu ya Muungano wa Afrika na mojawapo ya mataifa yenye ushawishi mkubwa katika siasa za bara. Akizungumza baada ya kuwasili nchini humo, Bw Kenyatta alitoa wito kwa mataifa ya Afrika kuendeleza demokrasia kwa kutumia suluhu zinazotokana na mazingira yao wenyewe badala ya kutegemea mifumo inayoagizwa kutoka mataifa ya nje. “Hali zetu ni za kipekee. Hatuhitaji kunakili na kubandika mifumo kutoka sehemu nyingine za dunia. Tunaweza kuunda na kueneza mbinu bora za Kiafrika kama sehemu ya suluhu za Kiafrika kwa matatizo ya Kiafrika,” alisema. Kauli hiyo imeonekana kuakisi msimamo ambao amekuwa akitetea mara kwa mara tangu astaafu urais, kwamba Afrika ina uwezo wa kutatua changamoto zake kupitia taasisi zake na uzoefu wake wa pamoja.Umaarufu wa Bw Kenyatta katika masuala ya uchaguzi uliongezeka zaidi mwaka 2024 alipoteuliwa kuongoza ujumbe wa Muungano wa Afrika katika uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini. Uchaguzi huo uliingia katika historia baada ya chama tawala cha African National Congress (ANC) kupoteza wingi wake bungeni kwa mara ya kwanza tangu mwisho wa utawala wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994. Kabla ya hapo, mwaka 2023, aliongoza ujumbe wa Muungano wa Afrika katika uchaguzi wa urais nchini Nigeria uliomwingiza madarakani Rais Bola Ahmed Tinubu. Katika mwaka huo huo, aliongoza pia ujumbe wa waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika uchaguzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Majukumu hayo yameimarisha hadhi yake kama mmoja wa viongozi wanaoaminiwa zaidi na taasisi za kikanda na bara katika kusimamia michakato ya kidemokrasia. Amani Hata hivyo, mchango wake haujaishia katika uchaguzi pekee. Kwa miaka kadhaa sasa, Bw Kenyatta amekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kurejesha amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, eneo ambalo limekumbwa na migogoro ya makundi yenye silaha kwa miongo kadhaa. Kama msuluhishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mchakato wa amani wa Congo, amekuwa akiongoza mazungumzo yanayolenga kuwaleta pamoja viongozi wa serikali ya Congo, makundi ya waasi na wadau wengine wa kikanda ili kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huo. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema nafasi anayocheza sasa imebadili taswira yake kutoka kuwa kiongozi wa kitaifa hadi mwanadiplomasia wa bara mwenye ushawishi mkubwa. Kwa mujibu wa wachambuzi hao, uwezo wake wa kufanya kazi na viongozi kutoka mataifa mbalimbali pamoja na uzoefu wake wa kuongoza Kenya kwa miaka kumi umemsaidia kujenga heshima kubwa katika duru za kisiasa za Afrika. Akiwa Ethiopia, Bw Kenyatta alisema uchaguzi wa nchi hiyo una umuhimu unaovuka mipaka yake kwa sababu Ethiopia ni makao ya Muungano wa Afrika na kitovu cha shughuli nyingi za kidiplomasia za bara. Zaidi ya Waethiopia milioni 54 wamejiandikisha kushiriki katika uchaguzi huo unaolenga kuchagua wabunge wa Bunge la Wawakilishi pamoja na viongozi wa serikali za majimbo. Muungano wa Afrika umetuma waangalizi kutoka mataifa 30 ya bara ili kufuatilia mchakato huo. Bw Kenyatta alisema jukumu la waangalizi wa uchaguzi si tu kutathmini iwapo kura zimepigwa kwa haki na uwazi, bali pia kusaidia mataifa ya Afrika kujifunza kutoka kwa uzoefu wa kila mmoja. “Muungano wa Afrika hufuatilia uchaguzi kote barani kwa lengo la kuimarisha demokrasia kupitia kujifunza kutoka kwa kila mmoja wetu,” alisema.Kauli hiyo inaonyesha maono yake ya Afrika inayojitegemea katika kuimarisha taasisi za kidemokrasia bila kutegemea ushawishi wa nje.
Go to News Site