LA TAIFA LEO
ALIYEKUWA Waziri Msaidizi, Ken Obura ametangaza kuwa hana shughuli na chama cha ODM na atawania wadhifa wa ugavana Kisumu kama mgombeaji huru. Haya yanajiri huku wagombea tisa waking’ang’ania tikiti ya ODM kuwania wadhifa huo. Bw Obura, 43 ambaye ni mwandani wa Rais William Ruto amesema kuwa hawezi kupoteza rasilimali zake kugombea ugavana kupitia ODM. Isitoshe, amesema chama hicho hakina demokrasia na hataki kuchezewa kwenye uteuzi jinsi anavyodai alifanyiwa mnamo 2022. “Mnamo 2022 mimi ndiye nilikuwa mgombeaji maarufu lakini uongozi wa ODM uliingilia kati na nikaambiwa nisiwanie ugavana. Nitawania kama mgombeaji huru kwa sababu sitaki chochote kuhusiana na uteuzi wa ODM,” akasema Bw Obura. Katika utawala wa sasa Bw Oburu anahudumu kama mkuu wa mipango katika afisi ya Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki. “Lazima tukomeshe mtindo huu ambapo watu wanachaguliwa kisha wanawajibikia maslahi ya ODM badala ya raia waliowachagua. Mara hii siko tayari kuacha azma yangu, nitagombea kama mwaniaji huru,” akaongeza. Bw Obura alihudumu kama Mbunge wa Kisumu ya Kati kwa tikiti ya ODM kati ya 2013-2017 kabla ya kutangaza angewania ugavana mnamo 2022. Kati ya 2017-2022 alihudumu kama waziri msaidizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Anasema kuwa alijiondoa kutoka kinyáng’anyiro cha ugavana mnamo 2022 kutokana na shinikizo kutoka kwa ODM. Hii ni baada ya Profesa Anyang’ Nyongó kupewa tikiti ya moja kwa moja. Wale ambao wanasaka tikiti ya ODM kuwania ugavana Kisumu ni Mbunge wa Nyakach Aduma Owuor, Rosa Buyu (Kisumu Mjini Magharibi), Seneta Tom Ojienda, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisumu Ruth Odinga, Mbunge wa Kisumu ya Kati Joshua Oron na Naibu Gavana wa Kisumu Mathews Owili. Bw Obura alidai kuwa uongozi wa ODM umewaangusha wakazi wa Kisumu tangu kuanza kwa ugatuzi nchini na mara hii wapigakura wanastahili kufanya maamuzi ya busara. “Yeyote ambaye anawania kupitia ODM anastahili kutazamwa kama adui wa watu na asichaguliwe kama gavana. Kama watu wetu wanataka maendeleo, basi wanastahili kuyafanya maamuzi ya busara badala ya kupiga kura kwa msingi wa vyama,” akaongeza Bw Obura. Uteuzi wa ugavana wa ODM umekuwa ukishuhudia ushindani mkali na kusababisha chama kuingilia kati kutuliza hali. Mnamo 2017, aliyekuwa Gavana Jack Ranguma ambaye pia ametangaza kuwa anasaka ugavana lakini bado hajatangaza chama, alipambana na Gavana Anyang’ Nyongó kwenye uteuzi ambao ulijaa ghasia. Profesa Nyongó na Bw Ranguma wote walidai walipata ushindi kwenye uteuzi huo ila gavana wa sasa aliishia kupata tikiti na ushindi wake ukatangazwa Nyakach badala ya ukumbi wa Tom Mboya ambako matokeo yalikuwa yakisubiriwa.
Go to News Site