LA TAIFA LEO
MIONGONI mwa vikwazo vikuu vinavyokabili hatima ya serikali ya Rais William Ruto pamoja na uongozi wa mashinani (kaunti), ni ongezeko la ufisadi. Ufisadi ni zimwi lililokita mizizi katika taasisi nyingi za umma ambalo linaendelea kutafuna rasilimali za wananchi huku likichangia kuongezeka kwa umaskini, ukosefu wa huduma bora na hasira za wananchi dhidi ya serikali. Mada hii imechochewa na tukio la hivi majuzi ambapo afisa mmoja wa Serikali ya Kaunti ya Nairobi alipatikana na mamilioni ya pesa taslimu nyumbani kwake. Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilisema kuwa kiasi hicho kilikuwa Sh65 milioni kinachoshukiwa kutokana na ufisadi. Hata hivyo, baadhi ya ripoti zilidai kuwa pesa zilizopatikana zilikuwa karibu Sh250 milioni. Bila kujali kiasi halisi, jambo hilo limewaacha Wakenya wengi wakijiuliza jinsi afisa mmoja wa umma anavyoweza kumiliki kiasi kikubwa namna hiyo ilhali mamilioni ya wananchi wanahangaika kujikimu kimaisha. Hakika, ufisadi ndio chanzo kikuu cha matatizo mengi yanayoikabili nchi hii. Pesa ambazo zingetumika kujenga shule, hospitali, barabara na miradi mingine ya maendeleo huishia katika mifuko ya watu wachache. Matokeo yake ni kwamba huduma za umma hudorora huku pengo kati ya matajiri na maskini likizidi kupanuka. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba serikali yenyewe inadaiwa takribani Sh0.7 trilioni na wafanyabiashara walioiuzia bidhaa na huduma mbalimbali. Wengi wa wafanyabiashara hao wamefilisika au wamekwama kifedha kwa sababu ya kucheleweshewa malipo yao. Kutokana na kisa hicho cha wiki jana, swali ambalo Wakenya wengi wanajiuliza ni, ikiwa afisa wa kaunti anaweza kuhusika katika wizi wa mamia ya mamilioni ya pesa, sembuse maafisa wanaosimamia bajeti kubwa zaidi katika serikali ya kitaifa? Hao wataiba mabilioni mangapi? Hili ndilo swali linalozidi kupunguza imani ya wananchi kwa viongozi wao na taasisi za serikali. Kauli ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kwamba serikali hupoteza takriban Sh2 bilioni kila siku kutokana na ufisadi bado inakumbukwa akilini mwa Wakenya wengi. Ikiwa tathmini hiyo ni sahihi, basi taifa hili limepoteza mamia ya mabilioni ya shilingi kila mwaka. Hivyo basi, vita dhidi ya ufisadi havifai kuwa vya maneno matupu. Wakenya wanataka kuona uchunguzi wa kina, mashtaka ya haraka na hukumu kali kwa wote wanaopatikana na hatia bila kujali vyeo vyao. Bila hatua madhubuti, ufisadi utaendelea kuangamiza uchumi, kueneza umaskini na kuchochea chuki ya wananchi dhidi ya serikali.
Go to News Site