LA TAIFA LEO
JERUSALEM, Israel: ISRAEL ilisema Jumatatu kwamba ilishambulia kiwanda cha kemikali kusini mwa Iran, na vituo vingine vya kijeshi vya nchi hiyo, hatua inayoonekana kama inayovuruga mchakato wa kupata muafaka wa amani kati ya Iran na Amerika. Shambulio hilo lilitekelezwa licha ya Rais wa Amerika, Donald Trump kuripotiwa kumwambia Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akomeshe mashambulio zaidi dhidi ya Iran. Ni shambulio la kwanza kutekelezwa na Israel ndani ya Iran tangu kufikiwa kwa makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano mnamo Aprili 28. Israel ilisema ilishambulia sehemu kadhaa za kiwanda cha kemikali kilichoko mjini Mahshahr huku afisa mmoja wa utawala akiliambia shirika la habari la Fars kwamba sehemu za kiwanda hicho ziliharibiwa. Awali, Trump alisema mashambulio mapya yanayotekelezwa na Israel na Iran hayataathiri mazungumzo ya amani kati ya utawala wake na Iran, akiongeza kuwa “Netanyahu hana usemi wowote”. Trump amekuwa akihimiza Israel kusitisha mashambulio nchini Lebanon ili kutoa nafasi kwa makubaliano ya kusitishwa kwa vita dhidi ya Iran. Wiki jana, Rais huyo wa Amerika alilazimika kumkaripia Netanyahu kuhusiana na suala hilo, kwenye mawasiliano kwa njia ya simu. Hata hivyo, mapema Jumapili, Israel ilitekeleza mashambulio katika eneo la Beirut, kwa mara ya kwanza tangu Amerika kutangaza mpango wa kufanya maridhiano na Iran. Iran ililipiza kisasi kwa kurusha makombora kadhaa katika vituo vya Israel, hatua iliyotishia ufanisi wa mazungumzo ya amani kati ya Amerika na Iran. Lakini Trump alisisitiza kuwa makubaliano ya kusitishwa kwa vita, vilivyoanza Februari 28, yatafikiwa “hivi karibuni”. “Mashambulio ya Israel dhidi ya Iran hayatakuwa na athari zozote kwa makubaliano hayo. Mimi ndiye mwenye usemi. Yeye (Netanyahu) hana usemi wowote,” akaeleza. Saa chache baadaye, Jeshi la Israel (IDF) lilisema kuwa lilishambulia vituo vya kijeshi vya Iran. Jeshi la Iran lilisema Israel ilitekeleza mashambulio kwa kutumia makombora yaliyorushwa kutoka angani. Iran ilikuwa imerusha makombora 11 nchini Israel, balozi wa Israel nchini Amerika Yechiel Leiter alisema kwenye taarifa kupitia mtandao wa X, akiongeza kuwa “Kila mtu amechoka na utawala wa Iran”. Mashambulio ya hivi punde kati ya Israel na Iran yamechangia kupanda kwa bei ya mafuta kwa kima cha asilimia tatu (3) Juni 8, 2026, huku kampuni ya Brent ikiuza bidhaa hiyo kwa bei ya Dola 96 (Sh4,680) kwa pipa. Rais Trump aliongea na Netanyahu kwa njia ya simu akiwa katika kilabu cha gofu cha Bedminster, New Jersey, Amerika kwa karibu nusu saa, kulingana na afisa mmoja wa Israel. Inasemekana kuwa wakati wa mazungumzo hayo, Trump alimwambia Netanyahu kusitisha mashambulio zaidi kwa sababu “tunakaribia kufikia kitu kizuri kitakachozalisha makubaliano”. Tangu kuanza kwa mazungumzo kati ya Amerika na Iran, Israel imeendeleza mashambulio dhidi ya Lebanon, ikilenga kundi la Hezbollah. Israel inasisitiza kuwa mashambulio hayo yanapaswa kutenganishwa na makubaliano yoyote ya kusitishwa kwa mashambulio dhidi ya Iran.
Go to News Site