Collector
Kajwang’ ataka vituo vya kupima Ebola viwekwe Ziwa Victoria | Collector
Kajwang’ ataka vituo vya kupima Ebola viwekwe Ziwa Victoria

Kajwang’ ataka vituo vya kupima Ebola viwekwe Ziwa Victoria

SENETA wa Homa Bay, Moses Kajwang’, ameitaka serikali ianzishe vituo vya kiafya vya kupima ebola kando ya Ziwa Victoria kuzima njia yoyote ambayo ugonjwa huo unaweza kuingia nchini. Bw Kajwang’ alisema kuwa Ziwa Victoria ina vijia vingi visivyotambuliwa ambavyo vinaweza kutumika kuingia na kutoka nchini. Vijia hivyo ni kando na vile vya mipakani vinavyotambuliwa rasmi. Ebola imeripotiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) pamoja na Uganda na Bw Kajwang anahofia kutangamana kwa wafanyabiashara kutoka mataifa hayo mawili na Kenya kunaweza kuleta maradhi hayo nchini. Wafanyabiashara hupitia visiwa vya Remba na Mfangano katika kaunti ndogo ya Suba Magharibi pamoja na Migingo katika Kaunti ya Migori kuingia na kutoka Uganda kuleta bidhaa. “Mbao zinazotumiwa kutengeneza boti hutoka DR Congo na wavuvi pia hupata bidhaa nyingi kutoka Uganda. Bidhaa nyingi huingizwa nchini kupitia Ziwa Victoria,” akasema Seneta huyo. Alitoa wito kwa serikali ichukue hatua madhubuti kuhakikisha kuwa maradhi hayo hayaingii nchini kupitia Ziwa Victoria. “Serikali haifai kumakinikia tu maslahi ya watu kutoka Amerika. Wakenya pia wanahitaji kulindwa dhidi ya ebola,” akaongeza. Alikuwa akizungumza wikendi katika eneobunge la Ndhiwa ambapo alimtaka Waziri wa Afya Aden Duale asema iwapo rasilimali na mikakati ya kutosha imewekwa kuhakikisha kuwa jamii zinazoishi kando ya Ziwa Victoria zimelindwa dhidi ya ebola. Aliandamana na wabunge James Nyikal (Seme) na mwenyeji wao Martin Owino (Ndhiwa) ambao walisifia mikakati iliyowekwa kuzuia ebola kuingia nchini. Dkt Nyikal alishukuru serikali kwa kuanzisha vituo vya kuwatenga wagonjwa wa ebola maeneo mbalimbali nchini, akisema vitasaidia kuzima mkurupuko wa ugonjwa huo nchini. “Vituo hivyo 23 ambavyo vipo ni sawa na lazima tuunge serikali katika vita dhidi ya ebola,” akasema. Mbunge huyo hata hivyo alipinga raia wa mataifa mengine kutengwa nchini akisema wataalamu husisitiza maradhi hayo yakabiliwe yalikoanzia.

Go to News Site