LA TAIFA LEO
MWANAHARAKATI Eric Omondi Jumatatu aliachiliwa huru na Mahakama ya Milimani Nirobi baada ya kukanusha mashtaka ya kuzuia magari kwenye barabara ya Kimathi mwezi uliopita. Bw Omondi aliachiliwa kwa dhamana ya kibinafsi ya Sh100,000. Alikuwa amezuiliwa katika kituo cha polisi wikendi nzima. Stakabadhi za mashtaka zilieleza kuwa alitenda kosa hilo Mei 18 katika barabara ya Kimathi jijini Nairobi. Kwa mujibu wa mashtaka Bw Omondi aliweka vibuyu 120 tupu vya plastiki barabarani baada ya kuvishusha kutoka kwa lori. Kitendo chake kilisababisha msongamano wa magari kwenye barabara hiyo yenye shughuli nyingi. Aliomba kuachiliwa kwa dhamana akisema hawezi kutoroka, na polisi wanafahamu makazi yake jijini. Wakiomba mahakama imwachilie mshtakiwa kwa dhamana mawakili wake Danstan Omari, Martina Swiga na Babu Owino walisema mteja wao alizuiliwa na polisi kwa saa 72 kinyume cha sheria. Bw Omari alisema vibuyu hivyo vilikuwa vikipelekwa kwa wakazi jijini ili kuhifadhia maji. “Tofauti na Wakenya wachache matajiri, wakazi wengi Nairobi wanaishi kwa umaskini mkubwa na hawawezi kumudu gharama za kuweka tangi la maji juu ya nyumba zao, wanatumia vibuyu,” aliambia korti. Bw Swiga alisema mteja wao anaendesha kundi lenye ushawishi Sisi Kwa Sisi ambalo huwasaidia Wakenya wengi wakati wa matatizo, na hivyo hawezi kugeuzwa mhalifu. Bw Owino aliitaka mahakama imwachilie mshtakiwa kwa bondi ya bure akisema alikamatwa kwa njia ya kikatili wakati tayari alikuwa amepanda ndege kuelekea jijini Kisumu kuhudhuria hafla ambapo alikuwa mfawidhi wa sherehe. Bw Owino, ambaye pia ni Mbunge wa Embakasi Mashariki jijini Nairobi, alieleza korti kuwa mshtakiwa alipoteza mapato kwa kukamatwa. Pia aliomba vifaa vya kielektroniki vya mshtakiwa vilivyotwaliwa wakati wa kukamatwa kwake virejeshwe, akisema ni vifaa vyake vya kazi na kwa sasa amebaki bila ajira. Akaongeza kwamba hakukuwa na msongamano wa magari Mei 18 kwa sababu kulikuwa na mgomo wa matatu kupinga bei ghali ya mafuta. Bw Owino alieleza mahakama kuwa alifanya juhudi kubwa kuhakikisha Omondi anaachiliwa kwa dhamana ya polisi lakini hakufanikiwa. "Polisi walikiuka Kifungu cha 49 cha Katiba kinachotaka mshukiwa kuachiliwa kwa dhamana wakati uchunguzi na mashtaka yanaendelea," aliongeza. Bw Owino pia alisema kuwa hakukuwa na msongamano wa magari mnamo Mei 18, 2026 kwa sababu kulikuwa na mgomo wa matatu wa kupinga kupanda kwa bei ya mafuta.
Go to News Site