LA TAIFA LEO
IKIWA imeorodheshwa kama nchi ya nne bora duniani katika uuzaji nje wa maua yaliyokatwa na ya mapambo, Kenya inaendelea kukumbatia aina mpya ya maua hatua inayoipanulia zaidi masoko ya kimataifa. Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Maua Kenya (Kenya Flower Council - KFC), Clement Tulezi, katika miaka ya hivi karibuni wakulima wa Kenya wameongeza uzalishaji wa maua aina ya waridi na mengine mapya yenye mvuto mkubwa kibiashara ngazi ya kimataifa. Aina hizo mpya ni pamoja na spray roses, waridi zilizoboreshwa kwa muda wa kudumu kwenye chombo na rangi mbalimbali, hypericum inayotumika kama mapambo hasa kwenye harusi, gypsophila (baby’s breath), na limonium ambazo zinaongezeka thamani sokoni. Hali kadhalika, maua mengine ni pamoja na alstroemeria, chrysanthemum, anthurium na maua mengine ya tropiki. “Tayari mazao haya yanazalishwa kwa minajili ya kibiashara katika mashamba kadhaa nchini na yanahamasishwa kama njia ya kupanua masoko,” Tulezi anasema. [caption id="attachment_186159" align="aligncenter" width="300"] Wafanyakazi wakitayarisha maua yaingie sokoni. Picha|Sammy Waweru [/caption] Kampuni ya Africalla Kenya, yenye asili ya Uholanzi na inayoendeleza shughuli zake Gilgil, Kaunti ya Nakuru, ni miongoni mwa wazalishaji wanaokuza aina mpya ya maua. Aidha, kampuni hiyo huzalisha zaidi ya aina 10 ya maua katika shamba lake la hekta 25 kwa ajili ya kuuza nje ya nchi. Africalla hukuza maua kama asters, lisianthus, carnations, chrysanthemums, calla lilies, phlox, tagetes, gypsophila na eucalyptus. “Lengo letu ni kuleta maua ya hadhi ambayo hayajakuwepo Kenya ili kuwahi masoko yenye ushindani mkubwa ng’ambo,” anasema Mkurugenzi wa Africalla Kenya, Geert Rooijakers. Kwa upande wa kampuni ya Wafex ya Australia, inabadilisha mboga asilia ya mchicha – maarufu kama terere na kwa Kiingereza amaranthus, kuwa maua kwa minajili ya soko la kimataifa. Meneja Mkuu wa kampuni hiyo nchini Kenya, Claris Wanjohi, anasema wanajikita katika uzalishaji wa maua ya kiangazi, huku amaranthus ikiwapa upekee. Sekta ya maua pia inalazimika kuhimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi. [caption id="attachment_186160" align="aligncenter" width="300"] Mfungo wa maua - Bouquet. Picha|Sammy Waweru [/caption] Kampuni ya Murara Plants, chini ya HilverdaFlorist, inajihusisha na utafiti na uzalishaji wa aina mpya inayostahimili magonjwa na wadudu. Kenya, ikiorodheshwa nchi ya tatu duniani kwa uzalishaji baada ya Colombia na Ecuador, huuza nje asilimia 99 ya maua yake. Waridi bado yanaongoza kwa kuchangia asilimia 65 ya mauzo ya nje, huku aina nyingine zikichukua asilimia 35 iliyobaki. Mwaka 2024, sekta ya maua ilikadiriwa kuingiza Dola milioni 835 kutoka kwa hekta 4,850 zinazolimwa. Ukuaji huu umechangiwa na ukumbatiaji wa aina mpya ya maua na upanuzi wa masoko, hasa ujio wa Asia na Mashariki ya Kati. Hata hivyo, inakabiliwa na changamoto kubwa ya gharama za usafirishaji wa anga, ambazo zimeongezeka kwa kasi. Licha ya changamoto hizo, wadau wanaendelea kushirikiana kutafuta suluhu, huku wakihamasisha matumizi ya reli na usafirishaji kwa njia ya maji, yaani meli. Maonyesho ya kila mwaka ya Kimataifa ya Maua (IFTEX) yanayoandaliwa Jijini Nairobi huendelea kuwa jukwaa muhimu kuonyesha mseto wa maua yaliyopo Kenya na kujadili mustakabali wa sekta hii.
Go to News Site