LA TAIFA LEO
WAKATI Waislamu walipohitimisha mwezi wao mtukufu wa Ramadhani Ijumaa iliyopita, changamoto ya kipekee imeibuka. Katika kipindi chote cha Ramadhani, viongozi wengi wa kisiasa, mashirika ya kibiashara na wananchi wa kawaida walijihusisha na shughuli za hisani, hasa kusambaza chakula na vinywaji kwa wasiojiweza. Usambazaji wa chakula kilichoandaliwa mara nyingi ulifanyika jioni karibu na wakati wa iftar, ingawa kulikuwa pia na ugawaji wa bidhaa nyingine za vyakula uliofanyika siku nzima katika misikiti, barabarani na katika maeneo mengine. Ilibainika kuwa, hali hii ilisababisha ongezeko la familia za mitaani katika eneo la katikati ya jiji, ambazo zilikuwa na uhakika wa kupata mlo mzuri. Sasa kwa kuwa Ramadhani imekaimilika na pia shughuli nyingi za hisani zimekoma, viongozi wametakiwa kuchukua hatua kabla idadi kubwa ya familia za mitaani igeuke kuwa tatizo la kiusalama. Kwa miaka mingi, Mombasa sawa na maeneo mengine ya mijini imekuwa na changamoto ya kushughulikia familia za mitaani, ambazo mara nyingi hulaumiwa kwa kuwashambulia wapitanjia na wakati mwingine kuwadunga visu. Mbunge wa Mvita, Bw Soud Machele, ambaye eneo lake linaathirika zaidi na familia za mitaani kutokana na kuwa katikati ya jiji, alisema serikali ya kaunti lazima ichukue hatua za haraka kabla hali haijawa mbaya zaidi. “Kuna watu wamefanya makao yao barabarani. Tunaomba kamishna wa kaunti na serikali ya kaunti, mshirikiane ili watu wapelekwe makwao,” alisema. “Ramadhan ilikuwa muda wa ukarimu, sasa imeisha. Hatuwezi kukubali ukosefu wa nidhamu uharibu sifa ya Mombasa,” akaongeza. Takwimu Kulingana na sensa ya familia za mitaani ya mwaka wa 2018, Mombasa ilikuwa na watu 7,529 wanaoishi mitaani, sawa na asilimia 16 ya jumla ya kitaifa, ikishika nafasi ya pili baada ya Nairobi yenye watu 15,337 sawa na asilimia 32.9. Jijini Mombasa, ilibainika kuwa, idadi kubwa ya watu wanaoishi mitaani (5,687), walizaliwa ndani ya kaunti hiyo, huku 1,826 wakiwa wamehamia kutoka kaunti nyingine na nchi jirani. Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, alisema utawala wake kwa kushirikiana na maafisa wa utawala wa serikali ya kitaifa tayari umeanza kushughulikia suala hilo. Bw Nassir alisema watu 468 wa kuishi mitaani walikusanywa wiki iliyopita, na kubainika kuwa wote walikuwa na makazi yao. “Si wote waliokuwa wakisaidiwa wakati wa Ramadhani ni wazuri, lakini tutasaidiana,” alisema gavana. Hii si mara ya kwanza kwa wasiwasi kuibuka kuhusu uhusiano wa shughuli za hisani na ongezeko la familia za mitaani Mombasa. Mnamo 2024, mpango wa utoaji misaada ya chakula uliotekelezwa na kampuni moja katika eneo hilo ulilaumiwa kwa kusababisha changamoto za usalama katikati ya jiji. Wakati huo, maafisa wa usalama walibaini kuwa, magenge ya vijana waliokuwa wakijifanya kutafuta msaada wa chakula walikuwa wakiwashambulia wapitanjia barabarani. Hali hii ilisababisha kusitishwa kwa mpango huo. Vilevile, oparesheni nyingine za kuwaondoa watu wanaoishi barabarani zimewahi kubainisha kuwa, baadhi yao hujifanya kuwa walemavu ili kupokea misaada kutoka kwa umma.
Go to News Site