LA TAIFA LEO
MPANGO maalum wa Rais William Ruto unaohusu kuboresha uzalishaji wa kilimo kupitia mbolea ya bei nafuu upo hatarini huku mashirika ya mabwanyenye yakiingilia na kuwatenga waliokusudiwa kunufaika kwayo. Mtandao huo unaoendeshwa nchini kote, umekuwa ukikusanya mbolea ya bei nafuu kwa mashehena, kuyasafirisha katika majengo ya kibinafsi, kuyapakia upya na kuyauza tena maradufu ya bei nafuu ya serikali. Tangu mpango huo ulipozinduliwa 2022, serikali imesambaza mifuko milioni 21 ya mbolea, ikiwemo milioni tatu katika miezi mitatu iliyopita pekee, kulingana na rekodi za Wizara ya Kilimo. Mpango huo unalenga kusambaza mifuko 12.5 milioni mwaka huu, kufuatia mifuko saba milioni iliyotolewa 2025. Chini ya mpango huo, wakulima hugawiwa bidhaa hiyo kulingana na idadi ya ekari zilizosajiliwa na Wizara ya Kilimo, zinazopatikana kupitia vocha ya kielektroniki kila msimu wa upanzi. Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, polisi wamewakamata washukiwa 10 wanaohusishwa na shughuli za uhalifu hasa maeneo ya Bonde la Ufa na Magharibi, hali inayoashiria kuwepo mtandao mkubwa uliopangwa vyema. Baadhi ya maeneo hususan Bonde la Ufa, Mashariki na Magharibi mwa Kenya yamekumbwa na uhaba huku wafanyabiashara fisadi wakielekeza mbolea kwingine kutoka vituo, duka na mabohari ya serikali katika kaunti. Idara ya Uchunguzi kuhusu Uhalifu (DCI) ilithibitisha ushirikiano kati ya maafisa kutoka stoo za Bodi ya Nafaka na Mazao (NCPB), hasa sehemu za Webuye na Voi, na mashirika ya mabwenyenye unaohujumu mpango wa serikali. Rais Ruto ameonya mara kadhaa kwamba yeyote anayejihusisha na shughuli hizo haramu atakamatwa na kushtakiwa akisisitiza kuwa mpango huo ni kiungo muhimu cha serikali yake. Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe na Katibu wa Wizara, Dkt Paul Kipronoh Ronoh vilevile alionya dhidi ya shughuli haramu zinazoweza kuhujumu uzalishaji wa mazao ya chakula na mauzo. Jumamosi, washukiwa wanane walikamatwa Kakamega kufuatia oparesheni ya kijasusi kutoka makao makuu ya DCI na maafisa eneo hilo. Katika kisa sawia wiki iliyopita, washukiwa wawili walikamatwa Kereinget, Kuresoi Kusini, na Kaunti ya Nakuru, huku mmoja akiwa hajulikani alipo. Oparesheni hiyo ya Kakamega iliyofanyika kijiji cha Ejinja, Rurambi, ilifichua kituo cha kusambazia mbolea ya magendo. Polisi walipata magari mawili yaliyojazwa mbolea aina mbalimbali, mifuko 39 ya OCP Africa TSP iliyowekwa nembo ya mbolea ya GK, mifuko 48 yenye rangi ya kubadilisha mwonekano wa bidhaa na cherahani tatu za kufunga bidhaa zilizopakiwa upya. Wapelelezi walisema wahalifu hao waliwashawishi wakulima kutwaa vocha zao kielektroniki kwa niaba yao na kuwalipa. Bidhaa hizo kisha ziliongezwa kemikali ya kuzifanya zifanane na bidhaa ghali kama vile DAP na kuuzwa kati ya Sh7,300 na Sh7,600 kwa kila mfuko wa kilogramu 50.
Go to News Site