LA TAIFA LEO
USHIRIKIANO uliopo kati ya Jeshi la Kenya (KDF), vitengo mbalimbali vya polisi, walinda usalama wa nchi jirani ya Somalia na jamii umetajwa kufaulisha pakubwa vita dhidi ya Al-Shabaab katika Kaunti ya Lamu na maeneo ya mpakani mwa Kenya na Somalia. Kulingana na afisa wa ngazi za juu katika jeshi, ambaye pia ni Kamanda wa Operesheni ya Amani Boni (OAB) inayoendelea msituni Boni, Brigedia Jenerali, Meshack Kishoyian, nidhamu, bidii na kujitolea kikazi kwa maafisa wanaoshiriki operesheni hiyo ni miongoni mwa vigezo vinavyozidi kumaliza magaidi wa Al-Shabaab. Bw Kishoyian alikuwa akizungumza Jumanne alipotembelea wanajeshi wa KDF wanaoendeleza operesheni ya kiusalama katika kanda ya Ras Kiamboni, tarafa ya Badhaadhere iliyoko Lower Juba, nchini Somalia. Ziara hiyo ni ya kutathmini hali na utayari wa KDF katika kukabiliana na matukio mbalimbali ya kiusalama yanapojiri. Pia ililenga kuangazia maslahi ya wanajeshi wanapokuwa kazini na jinsi wanavyoshirikiana na vitengo vingine vya usalama, utawala na wanajamii wanapokabiliana na magaidi. Bw Kishoyian aliwasisitizia KDF kuwa macho na kuingiliana vyema na vitengo vyote vilivyoko eneo la operesheni ili kufaulisha zaidi azma yao ya kulemaza Al-Shabaab. “Nafurahia ushirikiano wa KDF na wadau wengine wa usalama ambao umeharibu na kumaliza kabisa uwezo wa Al-Shabaab kushambulia. Uhuru wa magaidi kuzunguka huku na kule wakitafuta njia ya majaribio ya mashambulio, hasa maeneo haya ya mpakani mwa Kenya na Somalia tumeyadhibiti kabisa. Hakuna tena nafasi,” akasema Bw Kishoyian. Pia alisifu operesheni za kijasusi na ushirikiano wa wadau katika kusambaza taarifa za haraka kwa KDF, akiitaja hatua hiyo kuwa suala linalowawekea Al-Shabaab presha zaidi na kulemaza mipango yao. Alitaja jinsi magaidi wanavyotumia mbinu mbadala na kuendeleza mabadiliko katika majaribio yao ya kushambulia, akiwashauri wanajeshi kusalia ange katika kutekeleza operesheni yao. “Kufaulu kwa operesheni si kutegemea mbinu na ujuzi wa kupigana tu bali pia ushirikiano na nia moja miongoni mwa vitengo vyote vya usalama vinavyoshiriki kampeni hii katika kummaliza adui,” akasema Bw Kishoyian. Kamanda huyo wa jeshi pia alizuru na kufanya vikao na maafisa wa utawala, wanakandarasi wa ujenzi wa miradi mbalimbali kwenye eneo la operesheni na wadau wengine wa kiusalama, ikiwemo wawakilishi wa wanajeshi wa Jubbaland. Meya wa Ras Kiamboni Lukeman Abdi, aliisifu ziara ya kamanda huyo, akiitaja kuwa hatua inayonuia kurejesha kikamilifu usalama na amani eneo hilo. “Kama wanajamii wa hapa, tayari tunafurahia matunda mema tunayopata tangu operesheni ya kiusalama ilipozinduliwa maeneo haya,” akasema Bw Abdi. Kamanda anayesimamia kituo cha Polisi cha Ras Kiamboni kilichoko chini ya walinda usalama wa Jubbaland, Bw Mohamed Abdikarim, alisifu misaada ya kibinadamu inayotolewa na KDF kila mara kusaidia jamii za eneo hilo. “Kupitia KDF, jamii za hapa zimepokea matibabu ya bure, kusambaziwa maji nakadhalika," akasema Bw Abdikarim. Ziara ya Kamanda huyo wa ngazi za juu katika jeshi ni katika harakati za kudhihirisha mwendelezo wa ukakamavu wa KDF katika kurejesha amani na utulivu kupitia operesheni inayoendelea ya kiusalama kwa lengo la kudhibiti na kuleta amani ya kudumu nchini Somalia, mpakani mwa Kenya na Somalia na msitu wa Boni kwa jumla.
Go to News Site