LA TAIFA LEO
LONODN, UINGEREZA Chama cha Mashabiki wa Soka barani Ulaya (FSE) kimewasilisha malalamishi rasmi dhidi ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kikilalamikia “bei ghali zaidi za tiketi” za Kombe la Dunia la mwaka huu. FSE, kwa ushirikiano na Euroconsumers, inasema kuwa shirikisho hilo la soka duniani “limetumia vibaya nafasi yake ya ukiritimba” katika kupanga bei za tiketi za mashindano hayo yatakayoanza Juni 11, 2026. Mnamo Desemba, FIFA ilizindua idadi ndogo ya tiketi “nafuu zaidi” za Sh8,000 (Dola 60 au Pauni 45) kwa mechi zote 104 baada ya ukosoaji mkubwa wa bei zake. FSE imetaka FIFA kuachana na mfumo wa bei unaobadilika kulingana na mahitaji (dynamic pricing) na badala yake kuweka bei hizo wakati wa utoaji wa tiketi hapo Aprili. Pia imesisitiza kuwepo kwa uwazi zaidi kwa mashabiki wanaponunua tiketi, ikitaka angalau notisi ya saa 48 mapema kuhusu upatikanaji wa tiketi za kila kundi pamoja na maeneo ya viti. Katika malalamishi yao kwa European Commission, FSE na Euroconsumers wamedai kuwa FIFA imetumia nafasi yake “kulazimisha bei za juu zaidi za tiketi pamoja na masharti na taratibu zisizo wazi wala haki kwa mashabiki wa Ulaya”. Shirika la BBC liliambiwa katika taarifa: “Kutokana na ukiritimba wa FIFA wa kuuza tiketi za Kombe la Dunia 2026, imetumia nguvu hiyo kuweka masharti magumu ambayo hayangekubalika kamwe katika soko lenye ushindani.” FSE na Euroconsumers pia zimeorodhesha “ukiukaji sita bainifu” unaodaiwa kufanywa na FIFA. Miongoni mwa madai hayo ni kuishutumu FIFA kwa matangazo ya kilaghai; jambo haramu chini ya sheria za watumiaji za Umoja wa Ulaya, kwa kutoa tiketi za bei nafuu baadaye ambazo zilikuwa chache mno kiasi kwamba bei iliyotangazwa “haikupatikana kwa uhalisia”. Takriban tiketi 400 za Sh8,000 zimetolewa kwa mechi za hatua ya makundi za timu za Uingereza na Scotland. Mkurugenzi wa FSE, Ronan Evain, alisema hawakuwa na jingine ila kuwasilisha malalamishi kwa Tume ya Ulaya kutokana na “kushindwa kwa FIFA kushiriki mashauriano yenye maana.” “FIFA inatumia takwimu zake ambazo hazijathibitishwa za mauzo kama uthibitisho wa uhalali wa mbinu zake zisizo za haki za bei za tiketi, ilhali ukweli ni kwamba mashabiki waaminifu wanaachwa bila chaguo; ama walipe gharama hizo au wakose kushuhudia mechi,” alisema Evain. Kwa mujibu wa FIFA, takriban tiketi milioni saba zimewekwa kwa ajili ya mashindano hayo yatakayofanyika sambamba katika mataifa ya Amerika, Canada na Mexico. Kwa mtu mmoja kuhudhuria mechi nane; moja katika kila hatua, gharama itakuwa takriban Sh0.9 milioni kwa tiketi za bei ya chini, Sh1.5m kwa kiwango cha kadri na Sh2m kwa tiketi za bei ya juu zaidi. Mwaka wa 2022, gharama hizo zilikuwa takribani Sh250,000, Sh500,000 na Sh700,000 mtawalia, ingawa zilihusisha mechi saba pekee.
Go to News Site