LA TAIFA LEO
MAPEMA Januari mwaka huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres alitoa ujumbe wa kuatua moyo kwa nchi wanachama wa UN. Alionya kuhusu hali tete katika asasi hiyo ya kimataifa huku akiongeza kuwa shirika hilo lilikuwa katika hatari ya kuporomoka. Barua hiyo ilifuatia tahadhari za awali kutoka afisi za UN kwamba, shirika hilo lingelazimika kupunguza mgao wa bajeti wa kawaida kwa asilimia 15 mwaka huu. Hiyo ilimaanisha kutemwa kwa wafanyakazi 2,600. Hilo ni kosa ambalo athari zake zitadumu kwa miaka na mikaka. UN si shirika la kawaida. Ni gundi inayoshikamanisha mataifa ya ulimwengu. Ni jukwaa linaloratibu juhudi za kimataifa kuzima mizozo katika maeneo tofauti duniani, kulinda raia wanyonge, kuhakikisha mikataba ya kusitisha vita inadumishwa na kuhakikisha utawala wa kidemokrasia unakumbatiwa duniani kote. Huo ndio wajibu wake tangu 1948. Kutofadhili UN kutageuza dunia kuwa msitu usio na kanuni wala taratibu zozote. Utakuwa ulimwengu hatari kwa wanyonge na walio wachache kuishi. Hivyo, kufadhili mipango ya UN ni muhimu katika kudumisha utulivu duniani, kukuza mshikamano kimataifa, kutatua changamoto zisizotambua mipaka kama vile majanga ya kibinadamu, mabadiliko ya tabianchi na mikurupuko ya maradhi mbalimbali. Licha ya ukosoaji mkubwa kuhusu ufaafu na utendakazi wake, UN ndiyo asasi pekee ambayo inakubalika miongoni mwa nchi wanachama 193 kuendesha mazungumzo, kuweka viwango vya kimataifa na kushughulikia masuala mazito yenye athari kwa pembe zote za dunia. Hivyo basi, ni vyema kwa shirika muhimu kama hili kutegemea hisani na ukarimu wa mataifa na viongozi wa nchi wanachama kwa mipango yake? Inafaa, kimkakati, kuweka mabegani mwa wahisani wachache mustakabali wa shirika muhimu kama hili? Wachambuzi wa mahusiano ya kimataifa wanasema hali hii, ambapo mipango mingi ya UN inategemea michango ya wahisani kushughulikia mizozo hasa katika maeneo yanayokumbwa na vita, haifai kabisa. Kulemaa huku kwa UN kifedha kumesababishwa na kupungua kwa ufadhili, nchi wanachama kuwasilisha michango yao kuchelewa huku mataifa yenye ushawishi yakitoa migao yao lakini kwa masharti. Kwa mfano, ripoti za kifedha za UN zinaonyesha kwamba kufikia Februari 8, ambayo ni tarehe ya mwisho ambapo michango ya nchi wanachama inastahili kutua kwenye akaunti kufadhili shughuli za kawaida, ni nchi 55 pekee zilikuwa zimelipa. Upungufu huu wa kifedha unaoathiri afisi za UN na mamilioni ya watu wanaotegemea taasisi hiyo kujikimu umefufua mjadala kuhusu haja ya kusaka njia mbadala za kugharimia shughuli za shirika hilo muhimu. Mtaalamu wa Masuala ya Diplomasia na balozi mstaafu wa Kenya katika mataifa mbalimbali, Prof Maria Nzomo, anasema UN ni shirika muhimu zaidi kutelekezwa na nchi wanachama. Anatoa sababu ni kwa nini nchi hizo ziendelee kuwasilisha michango yao kwa UN. “Kutegemea ukarimu wa nchi wanachama kwa kampeni muhimu kama vile shughuli ya kulinda amani nchini Haiti inayoongozwa na Kenya (na kufadhiliwa na Amerika) inasababisha maruerue kwa mataifa ya kujitolea kama Kenya,” alisema. Alieleza kuwa, kwa sasa, maafisa 76,000 wa kulinda amani kutoka mataifa 120 wanahudumu katika vituo 11, wakilinda raia na kudumisha utulivu katika maeneo yasiyo salama. Msomi huyo anasema UN ndilo shirika linalotoa mfumo wa kisheria wa utekelezaji wa sheria ya kimataifa na hivyo kuzuia hali ambapo mataifa tajiri na yenye ushawishi kimataifa yanatumia mabavu kupata yatakacho. Kama ithibati ya umuhimu wa shirika hilo, hivi majuzi, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema msaada wake wa chakula na lishe, unaookoa maisha nchini Somalia, unaweza kukwama ifikapo Aprili iwapo fedha hazitapatikana kuuendeleza. Hali hiyo itawaweka mamilioni ya watu katika hatari ya kufa njaa. WFP inakadiria kuwa takribani watu milioni 4.4 wako katika hatari ya kukosa chakula cha kutosha, na takribani milioni moja kati yao wanakabiliwa na njaa kutokana na ukosefu wa mvua na kupungua kwa misaada ya kibinadamu. “Hali inaendelea kuwa mbaya kwa kasi,” alisema Ross Smith ambaye ni mkurugenzi wa maandalizi ya dharura katika WFP. “Familia zimepoteza kila kitu, na nyingi tayari ziko katika hali mbaya. Bila msaada wa chakula wa dharura, hali itazidi kuwa mbaya zaidi,” alisema Smith. Somalia ilitangaza ukame kuwa janga la kitaifa mnamo Novemba mwaka jana baada ya mvua kukosa kunyesha kwa misimu kadhaa. WFP, shirika kubwa zaidi la misaada ya kibinadamu nchini Somalia, limesema tayari limepunguza msaada kutoka kwa watu 2.2m mwanzoni mwa mwaka huu hadi zaidi ya watu 600,000 kutokana na ukosefu wa fedha. Mpango wa lishe kwa wanawake wajawazito, wanaonyonyesha na watoto wadogo pia umepunguzwa kwa kiwango kikubwa. Bw Mogire ni mhariri msimamizi wa gazeti la 'Taifa Leo' na mchanganuzi wa masuala ya kimataifa
Go to News Site