LA TAIFA LEO
NAIROBI ndiyo kaunti hatari zaidi kutokana na mauaji ya kiholela ya vijana kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika lisilo la kiserikali la Missing Voices . Ripoti hiyo iliyotolewa Jumanne, iliangazia jinsi mauaji ya kiholela na kutoweka kwa watu kulivyotokea mnamo 2024 na 2025. Pia ripoti hiyo ilimulika idara ya polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi, ikitaja maandamano ya Gen Z ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 kama yaliyokuwa na ukatili wa juu. Ingawa hivyo, visa vya utekaji nyara na kupotea kwa watu vilipungua mwaka jana ikilinganishwa na 2024. Kati ya Juni-Julai 2025, watu 68 waliuawa kwenye maandamano Nairobi. Hii ni asilimia 54 ya mauaji yote ya kiholela yaliyoshuhudiwa mwaka huo nchini. Kwa ujumla mauaji yote ya kiholela mwaka huo yalikuwa 131. Mnamo 2024, mauaji yote ya kiholela yalikuwa 159 kiwango hicho kikishuka kwa asilimia 17.6. Kando na Nairobi, Kiambu, Nakuru na Kajiado pia zilishuhudia mauaji mengi na ziko kwenye orodha ya kaunti hatari kiusalama. Idadi ya watu ambao walitoweka kwa njia tatanishi mnamo 2025 pia ilishuka ikiwa ni watu sita pekee kutoka 55 mnamo 2024. Kushuka huku kulikuwa kwa asilimia 89. Ripoti hiyo hata hivyo imetambua kuwa hakuna sheria Kenya ambayo inapendekeza hukumu kwa wanaohusika na watu kutoweka kwa njia tatanishi. Hii ndiyo maana imekuwa vigumu kwa familia kupata haki wapendwa wao wanapotoweka kisha kupatikana wameuawa. Baadhi ya mauaji katili ambayo yamenakiliwa kwenye ripoti hiyo ni ya Boniface Kariuki, 22 aliyekuwa akiuza barakoa jijini. Alipigwa risasi alipokuwa akichuuza barakoa kwa waandamanaji. Issa Mburu, seremala na baba wa watoto watatu naye alipigwa risasi akirejea nyumbani baada ya maandamano ya Saba Saba.
Go to News Site