LA TAIFA LEO
WAZIRI wa Kawi na Petroli, Opiyo Wandayi, jana alionya kampuni za kuuza mafuta (OMCS) dhidi ya kuhodhi bidhaa hiyo akisema kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na adhabu yake ni faini isiyopungua Sh1 milioni. Bw Wandayi alisema baadhi ya mashirika yamefanya njama kimakusudi kuhakikisha kuna uhaba kwa lengo la kuhakikisha bei inapanda kuanzia Aprili 15. Hii ni licha ya kuwa Kenya kwa sasa ina shehena ya lita 146 milioni za dizeli, lita 102 milioni za petroli na lita 167 milioni za mafuta taa katika hifadhi yake. Madai hayo yanatazamiwa kutikisa sekta hiyo, huku waziri akijizuia kutaja majina ya kampuni husika na kuthibitisha iwapo zinafanyiwa uchunguzi au la. Kulingana na sheria, kampuni za kuuza mafuta zinahitajika kudumisha kiwango cha chini zaidi cha shehena inayotosha siku 15 kwa bidhaa za dizeli, petrol na mafuta taa. Masharti hayo yanakusudiwa kulinda uchumi pale mifumo ya usambazaji bidhaa katika soko la kimataifa inapotikiswa. Kukiuka masharti haya kunavutia faini isiyopungua Sh1 milioni. “Pasipo kutaja nafasi thabiti ya usambazaji bidhaa, tumegundua kwa wasiwasi mkubwa ripoti za kuhodhi bidhaa kutoka kwa baadhi ya kampuni za kuuza mafuta. Tabia hii inakiuka kanuni za kibiashara, ni kinyume cha maslahi ya umma, na inakiuka moja kwa moja masharti ya kupatiwa leseni," akasema Bw Wandayi. “Hakuna uhaba wa mafuta nchini. Mifumo yetu kuanzia uhifadhi na usambazaji kupitia mifereji hadi kwa mtandao wa uuzaji inafanya kazi ipasavyo,” akaongeza. Taasisi inayohusika na usambazaji wa Petroli Afrika Mashariki (PIEA), inayowakilisha kampuni zote za mafuta zenye leseni nchini, haikujibu papo hapo maswali kuhusu shutuma za Bw Wandayi. Wanachama wa PIEA wanajumuisha kampuni za Vivo Energy, Rubis Energy Kenya, na TotalEnergies Marketing Kenya, ambazo pamoja zinajumuisha zaidi ya asilimia 50 ya soko la Kenya. Wanachama wengine mashuhuri ni pamoja na Ola Energy, Hass Petroleum, Lake Oil, na Be Energy. Akizungumza katika kipindi cha NTV Jumanne usiku, Mwenyekiti wa Muungano wa Mashirika ya Kawi na Petroli, Irene Kimathi, alisema usambazaji wa bidhaa hiyo umeendelea bila tatizo tangu 2022. “Lakini sasa baada ya kero hili la Mashariki ya Kati, yamkini serikali haikuwa imejiandaa vyema. Tuna mafuta ambayo ni ghali mno na ingawa kampuni za kuuza mafuta zina bei zinazofaa kutumika, haiwezekani kuuza. “Bei za sasa zilizowekwa na EPRA haziwezi kuongezwa au kuvurugwa. Hata hivyo, mfumo wa bei mwezi huu unapaswa kuratibiwa upya kwa dharura,” akasema Bi Kimathi. Licha ya haya, vituo kadhaa vya mafuta hususan Nairobi, Mombasa, na Kilifi, vimeishiwa na mafuta huku baadhi ya vituo vinavyomilikiwa na kampuni kuu, Vivo Energy, vikikabiliwa na upungufu wa bidhaa tangu wikendi iliyopita. Ununuzi wa hofu umesababisha wateja kununua kiasi zaidi cha mafuta kuliko kawaida, hali ambayo Vivo Energy inasema ilisababisha kuishiwa na bidhaa wikendi. Wanaodhibiti sekta ya kawi nao wanasema bei ya mafuta itapanda na itakuwa vigumu sana kudhibiti bei za sasa. Kwa sasa dizeli na petroli zinauzwa kwa Sh166.64 na Sh172.28 mtawalia kwa kila lita jjini Nairobi. Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya Sh6.53 kwa kila lita ya petroli na dizeli.
Go to News Site