LA TAIFA LEO
KIONGOZI WA ODM Dkt Oburu Oginga jana alipata ushindi hatari uliomruhusu kuendelea na Mkutano Maalumu wa Wajumbe (SDC) leo huku taharuki ikitishia kuendeleza msukosuko ndani ya chama hicho. Uamuzi wa Jopo la kutatua Migogoro ya Vyama vya Kisiasa (PPDT) ulifungua mlango wa mizozo zaidi kuhusu usimamizi na kesi za muda mrefu kati ya mirengo inayopingana—Linda Ground unaoongozwa na Dkt Oginga na Linda Mwananchi chini ya Katibu Mkuu Edwin Sifuna. Japo jopo liliruhusu chama kuendelea na SDC, pia liliamua kuwa Bw Sifuna ataendelea kushikilia wadhifa wake hadi michakato ya ndani ya chama ya kutatua mizozo itakapoisha. Kifo cha Raila Odinga aliyekuwa ameunganisha ODM kwa karibu miongo miwili, kiliacha pengo kubwa. Raila alifariki Oktoba 2025, na sasa chama kinakumbwa na mtihani wake mkubwa zaidi. Ingawa SDC inampa Dkt Oginga fursa ya kudhibiti chama, pia inachochea migogoro ya ndani na kesi za mahakama. Mrengo wa Bw Sifuna tayari umetangaza mkutano huo kuwa kinyume cha sheria kwa kutofuata taratibu, ukirejelea Kifungu cha 49 cha katiba ya chama. Wanapanga kwenda mahakamani kupinga uhalali wa maazimio yoyote yatakayopitishwa na wajumbe. Mrengo huo unaojumuisha Sifuna, naibu mwenyekiti wa chama Godfrey Osotsi, Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, na Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Antony Kibagendi, umetangaza pia mkutano wake wa wajumbe jijini Nairobi, hatua inayoonekana kama mapambano ya moja kwa moja na Linda Ground. Kifungu ambacho Bw Sifuna na wenzake wametaja kinaelekeza kuwa Mkutano Maalumu wa Wajumbe huitishwa na Mwenyekiti baada ya uamuzi wa Kamati Kuu ya Taifa au ombi lililoandikwa na angalau thuluthi tatu ya wanachama wenye haki ya kuhudhuria Mkutano wa Kawaida wa Taifa. Ilani na ajenda ya mkutano hutolewa na Katibu Mkuu. Ilani ya SDC ya leo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu Catherine Omanyo. Profesa David Monda, mchambuzi wa siasa na mhadhiri wa chuo kikuu nchini Amerika, anasema SDC inaweza kuingiza chama kwenye mzozo wa muda mrefu wa kisheria na hatari. “Ina uwezo mkubwa wa kugawanya chama na kusababisha kusambaratika kwa ODM kuelekea uchaguzi wa 2027,” anasema Prof Monda. Mgogoro ndani ya chama cha ODM umekuwa mkali kiasi cha kutishia chama ambacho kimewahi kutoa mgombea urais katika chaguzi kuu zilizopita. Kila ishara inaonyesha kuwa kwa mara ya kwanza, chama hakitakuwa na mgombea urais wake, huku Dkt Oginga na wafuasi wake tayari wakiunga mkono Dkt William Ruto na kudai wadhifa wa Naibu Rais. Moja ya migogoro hiyo ni ushindani wa kunyakua ngome za ODM. Mrengo wa Dkt Oginga unaunga mkono Dkt Ruto kwa muhula wa pili, huku Linda Mwananchi ukipinga mpango huo na kujisawiri kama wapinzani wakuu wa Dkt Ruto. Vilevile, Gavana wa Siaya James Orengo na Babu Owino wanatumia hisia za upinzani dhidi ya Ruto kuimarisha nafasi zao kisiasa. Wakati huo huo, Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi, Waziri wa Fedha John Mbadi, na Katibu wa Usalama wa Ndani Raymond Omollo wanaunga mkono Ruto. “Kinachojadiliwa ni iwapo tutaendelea kuwa katika serikali jumuishi. Iwapo kama chama, tulikubali kushiriki katika serikali jumuishi,” alisema Gavana Wanga, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ODM. Alikiri kuwa kutokuwepo kwa Raila kumechochea migogoro ya ndani, lakini chama bado kina msingi imara.
Go to News Site