LA TAIFA LEO
WIMBI jipya la kisiasa linaendelea kuvuma uchaguzi mkuu ukitarajiwa kufanyika 2027 nchini Kenya huku wanawake wengi wakijitosa kuwania nyadhifa za ugavana. Wakati huu, wanawake hawaonekani tu kama washindani wa kujaribu bali wapinzani kamili wanaolenga kuwapa wanaume ushindani mkali katika kaunti mbalimbali. Katika Kaunti ya Kakamega, Mwakilishi wa Kike, Bi Elsie Muhanda ameweka wazi azma yake ya kumng’oa gavana wa sasa Fernandes Barasa katika uchaguzi mkuu ujao. Anaamini uzoefu wake wa biashara na uongozi unaweza kuinua uchumi wa kaunti hiyo. Azma yake imeungwa mkono na vigogo kama Mabw Wycliffe Oparanya na John Walukhe. Hata hivyo, atakabiliana na upinzani kutoka kwa Dkt Boni Khalwale na Bw Cleophas Malala. Katika Kaunti ya Kiambu, Mbunge wa Thika, Bi Alice Ng’ang’a amejiunga rasmi katika kinyang’anyiro cha ugavana akimlenga, Gavana Kimani Wamatangi. Akiungwa mkono na wabunge kadhaa akiwemo Kimani Ichung’wah, Bi Ng’ang’a anasema ni wakati wa kaunti hiyo kupata uongozi wa mwanamke. Anasisitiza kuwa matatizo yanayowakumba wananchi bado hayajapatiwa suluhu licha ya ugatuzi. Katika eneo la kaskazini mwa nchi, Mbunge wa Kike Marsabit, Bi Naomi Waqo ameandika historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kutangaza nia ya kuwania ugavana katika eneo hilo, na kuungwa mkono na wazee wa jamii ya Borana kumeongeza uzito wa kampeni yake. Atachuana na Dido Rasso, huku wachambuzi wakitabiri ushindani mkali zaidi. Mwanasiasa mkongwe Bi Sophia Abdi anaeleza kuwa hatua ya mwanamke kuungwa mkono na wazee ni ishara ya mabadiliko ya kijamii. Kaunti ya Laikipia, aliyekuwa Mwakilishi wa Kike, Bi Cate Waruguru, amejiandaa kuwania ugavana kwa tiketi ya chama cha DCP cha aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua. Ameahidi mageuzi katika sekta ya afya na kupunguza ushuru. Atakutana na ushindani kutoka kwa Mabw Ndiritu Muriithi, Koinange Wahome na Mwangi Kiunjuri. Trans Nzoia, aliyekuwa Waziri wa Afya, Bi Susan Nakhumicha ameonyesha nia ya kumng’oa Gavana George Natembeya katika uchaguzi wa mwaka ujao, akimlaumu kwa kupuuza huduma za afya. Sawa na wenzake katika kaunti nyingine, kuungwa mkono na baadhi ya wazee kumeongeza uzito wa azma yake. Ukanda wa Pwani pia haujasalia nyuma. Aliyekuwa Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa ni miongoni mwa wanawake wanaotarajiwa kuwania ugavana Kilifi, hatua inayoweza kubadilisha siasa za eneo hilo. Mwaka 2022, wanawake saba walichaguliwa kuwa magavana, akiwemo Gladys Wanga, Kawira Mwangaza, Susan Kihika, Fatuma Achani, Wavinya Ndeti, Anne Waiguru na Cecily Mbarire ikiwa idadi kubwa zaidi tangu kuanzishwa kwa ugatuzi. Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, bado Baraza la Magavana linaongozwa na wanaume wengi, na uwakilishi wa jinsia haujafikiwa kikamilifu. Wachambuzi wanasema kuwa kuongezeka kwa wanawake katika siasa za ugavana ni ishara ya kukua kwa demokrasia na kuvunjika kwa mitazamo ya jadi iliyowazuia wanawake kuwania nyadhifa za juu.
Go to News Site