Collector
Giriş Yap
Msongamano, njaa kati ya hali zinazochochea vurugu shuleni – Ripoti | Collector
Msongamano, njaa kati ya hali zinazochochea vurugu shuleni – Ripoti

Msongamano, njaa kati ya hali zinazochochea vurugu shuleni – Ripoti

HUKU shule mbalimbali nchini Kenya zikikumbwa na wimbi la vurugu za wanafunzi ambazo zimesababisha kufungwa kwa muda kwa taasisi kadhaa, picha inayojitokeza inaonyesha malalamiko yanayofanana kwa wanafunzi na wadau wa elimu. Mali ya thamani isiyojulikana imeharibiwa katika baadhi ya shule baada ya wanafunzi kuzua vurugu, huku tukio baya zaidi likiwa ni vifo vya wanafunzi 16 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Utumishi, Gilgil, Kaunti ya Naivasha. Ingawa Kamati ya Kitaifa ya Ushauri wa Usalama haijatangaza matokeo ya kikao chake kuhusu hali hiyo, mahojiano na wanafunzi na walimu yanaonyesha kuwa shule nyingi zinakabiliwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi, huku changamoto zikianzia madarasani, mabweni, vyoo, sehemu za chakula na maji. Katibu wa Elimu ya Msingi, Profesa Julius Bitok, amenukuliwa akisema kuwa shinikizo la mitihani ni mojawapo ya sababu zinazochochea migomo hiyo, huku baadhi ya wanafunzi wakilalamikia pia uongozi wa shule kwa ukali kupita kiasi. “Badala ya kuwashurutisha wanafunzi kufanya mitihani, shule zinaweza kuahirisha. Tumeongeza ukaguzi, mazungumzo na mashauriano ili kuhakikisha masomo hayavurugwi,” alisema Prof Bitok. Wimbi hilo la vurugu limegusa hata shule ambazo hazikujulikana kwa migomo kama vile Alliance High School, Mang’u High School, Lenana School na State House Girls School. Serikali, hata hivyo, imesisitiza kuwa shule zitaendelea kufunguliwa hadi likizo fupi ya katikati ya muhula itakayoanza Juni 24 hadi 28, ikisema kuwa ni sehemu ndogo tu ya shule zilizoathirika. Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, amesema kutakuwa na ukaguzi wa miundombinu ya shule na kuhimiza mazungumzo bora kati ya walimu na wanafunzi ili kuzuia vurugu. Kulingana na taarifa kutoka kwa wadau wa elimu, kuna ushindani mkubwa wa rasilimali katika mabweni, madarasa, vyumba vya chakula na vituo vya maji. Katika shule nyingi, idadi ya wanafunzi imezidi uwezo wa miundombinu iliyopo. Walimu wanasema baadhi ya wanafunzi hulazimika kulala wawili kitanda kimoja kutokana na msongamano, huku wengine wakilalamika kuwa chakula hakitoshi kutokana na ongezeko la wanafunzi. “Wanafunzi wanalalamika kuwa chakula hakitoshi, na wengi hutoka vyumba vya mankuli wakiwa bado na njaa. Hili ni suala linalojirudia. Pia kuna msongamano darasani kiasi kwamba hata kufundisha ni changamoto,” alisema mwalimu wa shule moja ya kitaifa. Kiini cha changamoto hizi ni ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule nchini kufuatia utekelezaji wa mfumo unaozingatia umilisi na utendaji (CBE). Shule nyingi za kitaifa zimepokea wanafunzi wengi zaidi kuliko uwezo wao, hali iliyosababisha msongamano usio wa kawaida. Walimu wanasema licha ya juhudi za kuongeza miundombinu, idadi ya wanafunzi imekuwa ikiongezeka kwa kasi zaidi kuliko uwezo wa upanuzi. Wanafunzi wanasema maisha ya shule yamekuwa magumu kutokana na foleni kila mahali. “Unafika ni foleni ya chakula, maji, na hata vyoo. Kila mahali kuna msongamano,” alisema mwanafunzi mmoja kwa masharti ya kutotajwa. Changamoto nyingine zilizotajwa ni chakula duni, upungufu wa maji, shinikizo la mitihani, ukosefu wa ushauri nasaha, na mawasiliano duni kati ya wanafunzi na uongozi wa shule. Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi (NPA) Silas Obuhatsa, alisema tatizo kubwa ni kukatika kwa mawasiliano kati ya wanafunzi na walimu. “Wanafunzi hawasikilizwi. Wanahisi hawana sauti, na hapo ndipo matatizo huanza,” alisema.

Go to News Site