Mwananchi
Arusha. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amewaagiza viongozi wa hospitali na waganga wakuu nchini, kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa katika vituo vya matibabu zinazingatia utu, huruma na heshima kwa wagonjwa. Waziri Mchengerwa amesema malalamiko yanayotolewa na wagonjwa kuhusu huduma wanazopata katika baadhi ya vituo vya afya yanapunguza thamani ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya. Ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Juni 10, 2026, jijini Arusha wakati akizindua bodi mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mount Meru yenye wajumbe wanane. Mchengerwa amesema ubora wa huduma za afya haupaswi kupimwa kwa kuangalia majengo mazuri, ukubwa wa hospitali au uwepo wa vifaa vya kisasa pekee, bali kwa namna wananchi wanavyohudumiwa na kuridhika na huduma wanazopata. “Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya, hivyo ni wajibu wa viongozi wa hospitali kuhakikisha uwekezaji huo unatafsiriwa kuwa huduma bora kwa wananchi,” amesema Mchengerwa. Ameongeza kuwa hospitali inaweza kuwa na miundombinu bora, mashine za kisasa na bajeti kubwa, lakini mafanikio hayo hupoteza maana ikiwa wagonjwa wanahudumiwa kwa namna isiyoridhisha. Waziri huyo ameitaka bodi mpya ya Hospitali ya Mount Meru kuongoza mageuzi yatakayoiwezesha taasisi hiyo kuwa miongoni mwa hospitali bora za rufaa nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki. Amesema bodi hiyo inapaswa kuweka mkazo katika kuimarisha ubora wa huduma, mifumo ya uwajibikaji, ukusanyaji wa mapato ya ndani na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya. “Nendeni mkatafute majibu ya maswali magumu, ikiwamo kwa nini Mount Meru isiwe hospitali bora zaidi ya rufaa katika Afrika Mashariki. Hilo linawezekana ikiwa kutakuwa na uongozi wenye maono, usimamizi madhubuti na matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo,” amesema. Mchengerwa pia amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuimarisha huduma za afya, akieleza kuwa hospitali zinapaswa kutumia mifumo ya taarifa za afya kwa wakati halisi, usimamizi wa kidijitali wa dawa na vifaa tiba pamoja na huduma za tiba kwa njia ya mtandao (telemedicine). “Changamoto za karne ya 21 haziwezi kutatuliwa kwa mifumo ya karne zilizopita. Teknolojia si nyongeza tena, bali ni hitaji la msingi katika kuboresha huduma za afya,” amesema. Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mount Meru, Dk Ernest Alex amesema bodi mpya inatarajiwa kuimarisha usimamizi wa taasisi, kuongeza uwajibikaji na kuharakisha utekelezaji wa mikakati ya kuboresha huduma kwa wananchi. Amesema hospitali hiyo imepata mafanikio mbalimbali katika miaka ya karibuni, ikiwamo kupunguza vifo vya uzazi kutoka 32 kwa mwaka hadi 11 pekee. Dk Alex amesema hospitali hiyo yenye uwezo wa vitanda 450 hupokea wagonjwa wa nje kati ya 700 na 1,200 kila siku, huku wanaolazwa kwa wakati mmoja wakifikia kati ya 200 na 300. Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuimarika kwa huduma katika idara za tiba, upasuaji, magonjwa ya watoto, uzazi, mifupa, mfumo wa mkojo, huduma za wagonjwa mahututi (ICU), watoto wachanga mahututi (NICU) pamoja na uchunguzi na matibabu ya saratani. Pia amesema matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato yameiwezesha hospitali kuongeza mapato ya ndani kutoka Sh2.8 bilioni mwaka wa fedha 2021/22 hadi Sh11.9 bilioni mwaka wa fedha 2024/25. Amesema hospitali hiyo kwa sasa ina mashine ya kisasa ya CT Scan yenye uwezo wa Slice 64, mashine za kisasa za X-Ray na Ultrasound pamoja na maabara yenye ithibati ya kimataifa ya ubora wa huduma. Aidha, imekamilisha mradi wa uzalishaji wa oksijeni unaokidhi mahitaji yake na kuzalisha ziada inayosambazwa katika hospitali za wilaya za Mkoa wa Arusha. Hata hivyo, Dk Alex amesema hospitali bado inakabiliwa na uhaba wa wataalamu wa afya, ikifanya kazi kwa asilimia 48 tu ya watumishi wanaohitajika kwa mujibu wa muundo wake. Ametaja kada zenye upungufu mkubwa kuwa ni madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo, saratani, wagonjwa mahututi na upasuaji wa ubongo, hali inayosababisha watumishi waliopo kufanya kazi kwa muda mrefu na kuongeza hatari ya uchovu wa kitaaluma.
Go to News Site